Na. Dennis Gondwe, DODOMA

WAZAZI wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Kisasa wametakiwa kuwa kiungo muhimu baina ya walimu na wanafunzi katika malezi bora na kuwasaidia wanafunzi kufaulu.

Kauli hiyo ilitolewa na Mjumbe wa Bodi ya Shule ya Sekondari Kisasa, John Komba kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo katika mahafali ya shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo.

Komba alisema “niwashukuru ninyi wazazi kwa kufika kwenu na kutoa ushirikiano kwa wanafunzi wetu kwa ajili ya kuwapatia elimu. Ninyi ni sehemu na msaada mkubwa kwa ajili ya kuwawezesha walimu waweze kutimiza majukumu yao ya kuwalea na kuwafundisha wanafunzi wanapokuwa shuleni. Na kwa wale wanaoshindwa kutimiza majukumu yao kama wazazi ndio usumbufu ambao walimu wanaupata kutokana na ushirikiano mdogo kati ya wazazi na walimu na kupelekea matokeo yasiyo mazuri kwa wanafunzi kuanzia malezi hadi taaluma. Niwaombe wazazi tuendelee kutoa ushirikiano kwa walimu kwa ajili ya kumsaidia mwanafunzi kupata elimu bora na malezi bora”.

Aliwataka wanafunzi wanapokuwa shuleni kufuata sheria na taratibu zilizowekwa. “Sisi kama Bodi ya shule tutaendelea kufuata taratibu zilizowekwa na tutaendelea kuwa wakali kwa wale watakaokiuka sheria na taratibu za shule” alisema Komba.

Akiongea na wahitimu watarajiwa wa kidato cha Nne, aliwapongeza kwa uvumilivu na kusoma kwa bidii kwa miaka minne. “Niwapongeze sana tangu mmeanza kidato cha kwanza hadi kufika leo wanafunzi 233, ni kweli baadhi yenu walishindwa kufikia hatua hii. Niwaombe sana wanafunzi wetu mnaoenda kuhitimu na wale wanaoendelea na masomo kufuata sheria, kanuni na taratibu za shule. Hatutamuonea aibu mtu, hatutarudisha nyuma msimamo wetu wa kisheria, tutaendelea kuchukua hatua kali kwa wale wote watakaokwenda kinyume na utaratibu wa shule” alisisitiza komba.


Aidha, aliwaombea heri katika mitihani yao inayofuata. “Niwapongeze na niwatakie kila la keri katika siku zijazo za mitihani yenu. Mwenyezi Mungu awatangulie awabariki sana asiwepo mtu wa kuugua mpaka ndoto zenu zitakapokuwa zimetimia. Ninaona nyuso za madaktari hapa, wauguzi, wahandisi na walimu hapa” aliongeza Komba.


Akiwasilisha taarifa ya Shule ya Sekondari Kisasa, Mkuu wa shule hiyo, Mwl. Fredy Nyandoro alisema kuwa wahitimu hao walianza masomo mwaka 2020. “Kwa heshima naomba kuwahudhurisha kwako wanafunzi 233 ambao ni watahiniwa kwa mwaka huu 2023. Ndugu mgeni rasimi, shule yetu tumekuwa na mafanikio kadhaa tangu kuanzishwa. Mafanikio hayo ni kuongeza ufaulu mwaka hadi mwaka, kuongeza idadi ya watahiniwa na idadi ya vijana wanaojiunga elimu ya juu na vyuo vya kati imeongezeka” alisema Mwl. Nyandoro.


Maeneo mengine aliyoyataja ni kuongeza miundombinu mwaka 2019 walianza kujenga jengo la utawala ambalo limekamilika. “Mwaka 2021 tukapata mradi wa kuongeza madarasa kwa fedha za Uviko- 19 tulikuwa na madarasa matatu na kufanya madarasa kufikia 23. Tunaishukuru sana serikali yetu na mama yetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa ambao ameufanya katika sekta ya elimu na Shule ya Sekondari Kisasa ni mnufaika mkubwa wa uwekezaji huo” alisema Mwl. Nyandoro.


Mwanafunzi wa kidato cha Nne, Nasra Waziri alifurahia kuwa mwanafunzi wa shule hiyo. “Mimi nafurahia kuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kisasa inaonekana kuwa na sheria na taratibu zinazowalea wanafunzi vizuri. Mimi tangu mwaka 2020 hadi sasa 2023 nimejifunza mambo mengi shuleni hapa. Mimi nimeweza kuwa kiongozi na kujifunza “confidence” niliyojenga kuanzia chini, hata hawa wabunge walianzia chini” alisema Waziri.

Akiongelea maandalizi yake kwa mtihani wa taifa wa kidato cha Nne, alisema kuwa amejiandaa vizuri na kupata ufaulu wa kiwango cha juu. “Tumeweza kujenga taswira nzuri katika shule yetu. Nimeweza kufurahia mazingira ya shule yetu na jinsi walimu wanavyotoa ushirikiano kwetu” aliongeza Waziri.

Ikumbukwe kuwa Shule ya Sekondari Kisasa ilianza mwaka 2006 ikiwa na wanafunzi 20 na walimu watatu sasa ina wanafunzi 869 na walimu 55.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...