Na. Dennis Gondwe, CHANG’OMBE


HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imesikia kilio cha wakazi wa Mtaa wa Kishoka, Kata ya Chang’ombe cha kero ya kuziba kwa korongo linalopitisha maji ya mvua na kusababisha mafuriko katika makazi yao.

Katika utatuzi wa kero hiyo Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepeleka mtambo (JCB Backhoer) kwa ajili ya kufukua korongo hilo na kuondoa taka ngumu zilizotupwa kwenye korongo na kusababisha maji ya mvua kushindwa kupita.

Akiongea wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Ally Mfinanga alisema kuwa lengo la zoezi la kusafisha korongo hilo ni kuyawezesha maji ya mvua yaweze kupita vizuri na kutosababisha mafuriko katika makazi ya watu.

“Kama mnavyoona hapa tunaendelea na shughuli ya siku tatu ya usafishaji wa korongo la maji ya mvua katika Mtaa wa Kishoka, Kata ya Chang’ombe. Lengo kubwa ni kuhakikisha tunatoa mchanga, tope pamoja na taka ngumu zote ili kutoa urahisi wa maji ya mvua kupita vizuri kwenye korongo hili na kuzuia mafuriko katika makazi ya wananchi.

Wananchi wa eneo hili walitoa malalamiko kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kuhusiana na kero wanayoipata wakati wa mvua. Walisema kuwa kina cha korongo kimepungua na hivyo, kufanya maji kutuhama kwa muda mrefu na kusababisha yasambae kwenye makazi yao” alisema Mfinanga.

Mfinanga aliwataka wakazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuacha tabia ta kutupa taka ngumu katika makorongo ili kuyaruhusu maji ya mvua kupita kwa urahisi. “Wito kwa wakazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wakati halmashauri inachukua hatua ya kusafisha eneo hili kwa kuondoa mchanga, tope na taka ngumu wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma hususani wa Mtaa wa Kishoka hakikisheni hamtumii makorongo kama sehemu ya kutupia taka ngumu. 

Leo hii wote ni mashuhuda tunaona hapa korongo limeziba kwa sababu tunatupa taka ngumu. Halmashauri imeweka utaratibu wa makampuni na vikundi kwa ajili ya kubeba taka ngumu. Shime kwa wakazi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha makampuni na vikundi vinatumiwa ipasavyo” alisema Mfinanga.

Kwa upande wake Mkazi wa Kisima cha Nyoka Mtaa wa Kishoka, Vanesa Robert alisema kuwa kero kubwa wanayoipata wakati wa mvua ni maji huingia katika makazi yao. “Shida tunayoipata mvua ikinyesha yaani maji yanajaa ndani tunakosa pa kulala. 

Watoto wanaoenda shule wanashindwa kwenda kwa sababu njia zinakosekana. Tunaomba mtuwekee daraja kubwa na kina cha korongo mkirefushe ili maji yawe yanapita kwenda siyo kutuama na kuingia kwenye makazi yetu. Kufukua mchanga huu ni usaidizi mkubwa kwetu maana mvua ikianza kunyesha maji yatapita vizuri” alisema Robert.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...