Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

WANUFAIKA wa Kikundi cha Asante kilichopo Kijiji cha Idumila mkoani Njombe, wameeleza namna Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulivyowawezesha kununua shamba la miti na pamoja na kuwa na miradi mbalimbali ya kiuchumi.

Wakizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari walipotembelea wanufaika wa kijiji hicho mkoani Njombe, wanakijiji hao wamesema fedha zinazotolewa na TASAF si ndogo na kwamba ili ziweze kuleta mafanikio, ⁷wanufaika wanapaswa kuwa na miradi ya maendeleo.

Mmoja wa wanachama wa a kikundi cha Asante, Rehem Kilasi amesema baada ya kupata fedha za TASAF anazigawa kwa ajili ya miradi yake ya kilimo cha parachichi na dukani.

Pia amesema kuwa ana miche 17 ya parachichi ambayo ameanza kuvuna na kuuza pamoja na shamba la nyanya.

"Mpango wangu wa kwanza nilipeleka kwenye mradi wa kuku ambao baada ya kuzaliana niliuza 40 na nina akiba ya kuku wengine. Baada ya kuuza nilianza kuuza vitenge na kisha nilifungua duka ambalo lilianza na kreti moja la soda na vitenge lakini sasa kuna kila kitu," amesisitiza.

Pia amesema fedha anazopata ananunua mbolea na dawa kwa ajili ya kuweka shambani.

Kilasi amesema anatamani aongeze mradi wa duka la jumla, kuuza mitumba na migahawa ili kuwezesha kuinuka kiuchumi.

Kuhusu kulima nyanya, Kilasi amesema lengo la kuingia kwenye kilimo hicho ni kwa kuwa kinatumia muda mfupi mpaka mavuno na kwamba ni eneo mojawapo la kumuwezesha kupata fedha kwa muda mfupi.

"Nimejenga nyumba ya bati yenye vyumba sita. Ninaishi na watoto wawili mmoja yuko darasa la tatu wote hawana wazazi hivyo natamani nije kuwasomesha kwa kiwango nitakachojaliwa," ameeleza.

Ameongeza kuwa " TASAF ilipoingia ilinipa nguvu kwani nilipoipata kwa mara ya kwanza niliona niipeleke kwenye uzalishaji.

"Viongozi wetu walitusaidia kutupa motisha kuhusu matumizi ya fedha za TASAF kwamba tunapozipata tuzitumie vizuri ikiwemo kuwekeza. Tunaishukuru waliotusaidia na kutufuatilia katika kuhakikisha miradi yetu inasimama," amefafanua.

Pia amesema wanaodhani kwamba fedha hizo ni chache wanatakiwa kujua kuwa bila kuzizalisha fedha hizo haziwezi kutosheleza hivyo, alishauri kuwatumia maofisa wao kuelekezwa matumizi sahihi na kuwa na miradi.

Mwenyekiti wa kikundi hicho, Joyce Kilasi amesema kabla ya kuingia TASAF alikuwa na maisha magumu tofauti na sasa ambapo ana nyumba.

Kilasi ambaye pia ni Mkazi wa Kijiji cha Ibumila, amesema alipopokea fedha awamu ya kwanza alishauriana na wanakikundi wenzake kuwa na shamba la miti.

Amesema waliazima shamba na walipanda miti na kwamba tayari wamevuna na kuuza na kurejesha shamba hilo kwa muhusika.

" Tumenunua shamba la heka mbili na tunatarajia kupanda miti lakini pia shamba la heka moja lililopandwa miti tulinunua Sh milioni moja na sasa kila mwanakikundi ana makazi yake," amesisitiza Kilasi.

Amesema "wanakikundi walikuwa wanaishi katika nyumba za nyasi na wamejenga; alibaki mwanakikundi mmoja ambaye baada ya kuuza miti tulimwezesha na yeye kujenga nyumba ya bati."

Kilasi anafanya biashara ya kuuza mitumba maeneo mbalimbali hivyo, anapata fedha za kulipa kwenye kikundi.

"Nawashauri wanaTasaf wenzangu wawe na vikundi kwani vinasaidia kutatua changamoto zinazotokea kwa kukopa fedha na kurudisha na riba. Kwenye kikundi kila mtu anabiashara ambayo inamuwezesha kuwa na marejesho," ameongeza.

Amesema wao huuza vigogo baada ya kukua kwa miaka sita na mirunda kwa miaka minane na kwamba nguzo za laini ni 30,000 kwa moja na 25,000 kwa watu binafsi.

"TASAF ni muhimu kwenye maisha yetu kwa sababu tunasomesha watoto wetu mpaka sekondari na wengine wapo vyuo. Tukidaiwa ada kama fedha za TASAF hazijatoka tunaweza kukopa kwenye vikundi," amefafanua.

"Tunamshukuru Rais Samiah kwa kuendeleza TASAF na hata kama wafadhili wataondoka, tunauwezo wa kumudu maisha na vikundi vitaendelea."

Belitha Mwenda amesema TASAF iliwaahidi kuwasaidia kupata chakula na yeye alikuwa anaishi na mjukuu wake.

"Tulikuwa tunanjaa, tunateseka kwa sababu hatuna chakula. Tulianza kuchukua Sh 36,000. Tunaishukuru TASAF imetusaidia tumeondokana na njaa kwani mpaka sasa nimenunua nguruwe tumefuga na vitoto vyao tuliuza."

Amesema kuwa mara ya kwanza alikuwa anaishi kwenye nyumba ya miti lakini kutokana na mauzo ya mifugo hiyo, alijenga nyumba ya bati.

Pia amesema kwa kutumia fedha za TASAF zimewasaidia kupeleka shambani na wameongeza uzalishaji hadi malori matano hadi saba.

"Naishukuru TASAF na Rais Samia kwa kuendelea kutulea kwani iliniokota nikiwa masikini sana nilikuwa na hangaika lakini kwa sasa nina nyumba, ng'ombe ambao wanaisaidia kulima na naendelea kufuga nguruwe na kuku," ameongeza.

Naye, Mratibu wa TASAF halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Kelvin Kapungu amesema halmashauri hiyo ina Kata 12 na vijiji 45 na vilivyopo kwenye mpango ni asilimia 70.

Amesema halmashauri hiyo ina jumla ya wanufaika 3,925 na kwamba katika Kijiji cha Idumila Kata ya Kichila ina jumla ya walengwa 137.

Kapungu ameeleza kuwa wanufaika hao wanajishughulisha na shughuli mbalimbali za kukopa na kukopeshana.

"TASAF ina jumla ya vikundi 140 na faida kubwa ya kuwepo kwenye vikundi ni kuongeza mahusiano na kufarijiana. Tumeona matokeo katika kikundi hiki cha Asante,"

Amesema kikundi hicho kina miradi endelevu kwani walianza kwa kukodisha shamba la miti na kuvuna na wamenunua heka tatu na wamenunua miche ya kupanda Januari 2024.

"Kila mwanachama ana shughuli binafsi wanazofanya, vikundi huwasaidia kupata fedha kidogo kuendeleza mashamba yao na kujenga nyumba,"

Amesema wanaendelea kuhamasisha vikundi kuwa na mipango ambayo itawawezesha kuondokana na maisha magumu na kujiandaa hata pale mradi utakapokoma.
 

Mwenyekiti wa kikundi cha Asante, Joyce Kilasi akieleza jinsi walivyojikwamua na umaskini kupitia shamba la miti wanalilonunua kwa fedha za ruzuku za TASAF
 

Beritha Mwenda, mkazi wa kijiji cha Ibumira Kata ya Kichiwa, wilayani Njombe, akielezea jinsi alivyonufanika na fedha za ruzuku za TASAF
 

Nyumba ya Bertha Mwenda aliyoijenga wakati wa kuundwa kwa vijiji vya ujamaa, lakini kwa sasa imebaki kama ukumbusho baada ya kujenga nyumba za kisasa kutokana na msaada wa fedha za TASAF
 

Rehema Kilasi, Mwanakikundi wa kikundi cha Asante akiwa katika shamba lake binafsi la bustani ambalo amelianzisha kwa msaada wa fedha za ruzuku za TASAF
 

Kelvin Kapungu, Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Njombe DC akielezea mafanikio waliyopata wanufaika wa mfuko wa TASAF

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...