Na Muhidin Amri,
Newala

SERIKALI imetoa Sh bilioni 1.3 kwa ajili ya upanuzi wa mradi wa maji wa Miyuyu-Mnima ili
kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa kata tatu ya Chilangala,Mnyambe na Mkoma 11 wilaya ya Newala mkoani Mtwara.


Hayo yamesemwa jana na kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Newala Mhandisi Juma Malilo,wakati akitoa taarifa ya upanuzi wa mradi huo unaofanywa na mkandarasi Kampuni ya Mlimi International Tanzania Ltd.


Malilo alitaja kazi zinazofanyika ni ujenzi wa matenki mawili ya lita 250,000 kila moja,ulazaji wa bomba na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji katika vijiji 14 vinavyokwenda kunufaika na mradi huo.

Amevitaja baadhi ya vijiji vitakavyonufaika na upanuzi huo ni Namangudu,Nangujane,Lihanga Malachi,Mkongi na Chilende ambavyo havina maji ya uhakika,badala yake wananchi wanategemea kupata maji kupitia miradi ya zamani na vyanzo vya asili ambavyo havitoshelezi mahitaji yao.

Aidha alieleza kuwa,wakati Ruwasa inaendelea na kazi ya upanuzi wa mradi huo, wameamua kufunga tenki la plastiki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 10,000 na kukarabati mfumo wa zamani katika kijiji cha Mikumbi ili kuwapunguzia adha ya maji wananchi wa kijiji hicho.

Hata hivyo alisema,licha ya kufanya maboresho hayo bado tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji siyo rafiki na hali hiyo inatokana na mgao mkubwa wa umeme katika wilaya ya Newala,hivyo kuathiri sana utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi.


Katika hatua nyingine Malilo alisema,kwa mwaka wa fedha 2023/2024 wanatarajia kutekeleza jumla ya miradi 8 katika vijiji 60 vilivyopo Halmashauri ya wilaya Newala na Halmashaur mji Newala.
Alisema kuwa,miradi hiyo itakapokamilika itaongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji katika wilaya ya Newala kutoka asilimia 58 hadi kufikia asilimia 84 na watu 82,037 watanufaika.


Kwa upande wake msimamizi wa ujenzi wa mradi wa maji Miyuyu-Mnima kutoka kampuni ya Mlimi International Ltd Abdala Mahabo,ameishukuru serikali kuwajali wakandarasi wa ndani katika kutekeleza miradi ya maji hapa nchini.


Alisema,kazi inaendelea vizuri na watakamilisha kazi zote ifikapo mwezi Disemba mwaka huu kama ilivyo kwenye makubaliano ya mkataba,hata hivyo ameiomba serikali kutoa fedha zilizobaki ili waweze kuongeza nguvu kazi katika utekelezaji wa mradi huo.


Mwenyekiti wa kijiji cha Miyuyu kata ya Chilangala Raibu Bakari,ameiomba serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kuharakisha ukarabati na ujenzi wa mradi huo ili kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.

“pia naomba wenzetu wa Tanesco waboreshe mfumo wa umeme ili kuwezesha huduma ya maji ipatikane muda wote,kwani bila ya umeme wa uhakika serikali itakuwa inafanya kazi isiyokuwa na tija”alisema.

 

Ujenzi wa tenki la lita 250,000  katika kijiji cha Miyuyu wilayani Newala ukiendelea.
 

Baadhi ya akina mama wa kijiji cha Mikumbi wilayani Newala wakichota maji katika kituo cha kinachotoa huduma ya maji baada ya wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kufunga tenki moja la plastiki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 10,000 kama hatua za kuwanusuru wananchi na adha ya huduma ya maji safi na salama wakati ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wa Miyuyu ambao utakwenda kumaliza changamoto ya maji katika vijiji mbalimbali ikiwemo kijiji hicho ukiendelea.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...