Na Mwandishi wetu, Mirerani


MWEKEZAJI wa mgodi wa madini ya Tanzanite,  Jun Fang amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan amsaidie ili aweze kupata haki yake ya fedha na mali venye thamani ya shilingi bilioni 8.5 baada ya kutaka kudhulumiwa kwenye mgodi wa madini ya Tanzanite.

Meneja wa Fang, Dk Alfred Nguma akizungumza mji mdogo wa Mirerani amesema mwekezaji Fang aliingia ubia na mchimbaji Saniniu Laizer wa miaka 10 tangu mwaka 2011 hadi 2021 kwa mwekezaji kumiliki hisa asilimia 70 na mzawa kumiliki asilimia 30 kwa makubaliano kuwa Fang kuleta vifaa vyote vya uchimbaji vya kisasa, mtaji, teknolojia na miundombinu na alifanya hivyo bila ya kipingamizi.

Dk Nguma amesema yeye ndiye aliyemleta mwekezaji kutoka China kwani alikuwa huko katika masomo na alifanya hivyo baada ya serikali ya Rais Samia kufungua milango kwa wazawa kutafuta wawekezaji wa nje, kuja nchini kuwekeza na alifanya hivyo katika sekta ya madini.

Dk Nguma amesema walifanya shughuli za uchimbaji kwa kipindi chote na uzalishaji mkubwa ulifanyika na kila mmoja alikuwa akipata mgao wake na malipo halali ya kodi ya serikali yalikuwa yakilipwa bila ya matatizo.

Amesema mwaka 2016 mwishoni changamoto zilianza kutoka kwa Laizer na kuamua ghafla kumtafuta mtu mwingine aliyetajwa kwa jina la Godluck Mollel maarufu kwa jina la Kaka na kuingia naye ubia wa asilimia 50 bila kumshirikisha Fang.

"Mwaka 2017 hadi 2021 mgodi huo ulikuwa ukichimbwa na Mollel, Fang na Laizer na mgao wa hisa ulikuwa Mollel hisa asilimia 50, Laizer hisa asilimia 30 na Fang hisa asilimia 20 hali hiyo ilifanya mwekezaji Fang kushindwa kuelewa na alipoulizwa Laizer hakuwa na majibu sahihi na kusema kuwa kitengo chake cha mahusiano serikalini kimekuwa na gharama kubwa hivyo alihitaji msaada," amesema.

Amesema alifanya kila jitihada katika ofisi za madini Mirerani na Wizara ya Madini kueleza hali hiyo ila hakuweza kupata majibu stahiki na sasa wameamua kumwomba balozi wa China hapa nchini awasaidie kwani anaona kabisa kuna kila dalili ya yeye na Fang kudhulumiwa fedha na mali bila ya kuwa na sababu za msingi.

Amesema wakati anaingia Ubia na Laizer mwaka 2011, Laizer hakuwa na utajiri alionao wa kuendesha shughuli za mgodi huo na hakuwa na hata kifaa kimoja cha kisasa kwani vifaa vyote vililetwa nchini kutoka China na mwekzaji Fang na utajiri wote umetokana na mtaji na vifaa vilivyoletwa na mwekezaji kutoka China.

‘’Serikali ina nia njema na wachimbaji wa madini ya Tanzanite ila kuna wamiliki wachache wa migodi wanaichafua sekta hiyo na kuitangaza nchi vibaya nje hivyo ni wakati wa serikali kukemea hilo na kuchukua hatua ili iwe fundisho kwa wengine’’ amesema Dk Nguma.

Hata hivyo, Kiria Laizer ambaye ni meneja wa Bilionea Laizer amekiri kumfahamu Fang kwa kufanya naye kazi kwa miaka 10 tangu mwaka 2011 hadi 2021 na baada mkataba kumalizika raia huyo wa China aligoma kusaini makubaliano ya awali{MOU} ili waweze kuingia tena mkataba mpya.

Kiria amesema kabla ya mkataba kumalizika Fang alileta mwekezaji mwingine aliyekuwa akiitwa Godluck Mollel maarufu kwa jina la Kaka na walifanya kazi naye hadi mwisho wa mkataba na baadaye aliondoka baada kugoma kusaini MOU na haijulikani mahali alipo.

Amesema wao hawana shida na mchina ila yeye ana shida maana hataki kukubaliana masharti ya MOU ambayo hayakuyataja na kusisitiza kuwa anayepaswa kujua hayo masharti ni mchina mwenyewe na siyo mtu mwingine.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...