Na Beatus Maganja, Dar es Salaam

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema Serikali inatarajia kupata mapato yanayokadiriwa kufikia dola za Kimarekani milioni 314 katika kipindi cha miaka 20 kutokana na uwekezaji mahiri katika maeneo saba (7) yaliyo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA

Mhe. Kairuki ameyasema hayo leo Januari 03, 2024 katika hafla ya utiaji saini mikataba ya uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment Concession Areas - SWICA) kati ya TAWA na Makampuni manne ya uwekezaji yanayofanya shughuli za utalii ndani na nje ya nchi iliyofanyika chuo cha utalii cha Taifa (NCT) Jijini Dar es Salaam.

Amesema kupitia uwekezaji huo unaokadiriwa kuwa na thamani ya TZS bilioni 696 wawekezaji watawajibika kuwekeza kwenye miundombinu katika maeneo yao ya uwekezaji na kuhakikisha wananchi wanaozunguka maeneo hayo wananufaika na kuona umuhimu wa aina hiyo ya uwekezaji.

Aidha amempongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania kwa kufanya filamu maarufu ya Tanzania The Royal Tour ambayo imeleta matokeo makubwa kwa kuleta ongezeko kubwa la watalii nchini

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda amesema baada ya upembuzi yakinifu uliofanywa katika nchi za SADC kuhusu uwezekano wa modeli hii ya biashara (SWICA), uzoefu ulionesha kuwa modeli hii inajulikana kwa uwezo wake wa kuwezesha Mamlaka za eneo lililohifadhiwa kuzalisha mapato endelevu kwa ajili ya uhifadhi na maendeleo.

Aidha amesema mapato yanayotarajiwa kuzalishwa kwa mwaka ni mara tisa (9) ya mapato yaliyokuwa yakipatikana awali kwa shughuli za utalii zilizokuwa zikifanyika maeneo hayo, hivyo ongezeko hili la mapato linaashiria kwamba mpango wa biashara wa SWICA ni chaguo zuri la kufikia matumizi bora na endelevu ya rasilimali ya wanyamapori kwa manufaa ya kiuchumi

Aidha amesisitiza kuwa TAWA imejipanga vyema kuhakikisha inatekeleza vyema miradi yote ya SWICA katika maeneo husika kwa kushirikiana na wawekezaji

Maeneo ya kimkakati ya uwekezaji mahiri yanayotajwa kuwekezwa ni Pori la Akiba Mkungunero (Dodoma), mapori ya akiba Ikorongo na Grumeti (Mara) pamoja na Pori la Akiba Maswa (Kimali, Mbono na Kaskazini) Mkoani Simiyu.

Aidha, Makampuni yaliyowekeza katika maeneo hayo ni Bushman Safari Trackers Ltd (Maswa GR North), Grumeti Reserves Ltd (Grumeti na Ikorongo GR), Mwiba Holdings Ltd (Maswa GR Mbona na Maswa GR Kimali) pamoja na Kampuni ya Magellan General Trading LLC (Mkungunero GR).

Hafla hiyo imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula(Mb), Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko

Wengine ni Makamishna wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya Uhifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), baadhi ya watendaji na maafisa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na TAWA pamoja na wadau mbalimbali wa uhifadhi.



Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) akizungumza wakati wa utiaji saini wa mikataba sita ya uwekezaji katika Maeneo Maalum ya Uwekezaji wa Wanyamapori (Special Wildife Investment Concession Areas – SWICA).
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Dunstan Kitandula akizungumza katika hafla hiyo kabla ya kumkaribisha Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Angella Kairuki.













Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwindaji ya Bushman Safari Trackers Ltd, Talal Abood akitoa shukurani zake kwa serikali kwa kampuni yake kusaini mkataba huo na wizara ya Maliasili akisema hiyo inafungua milango kwa wafanyabiashara kuwekeza katika sekta ya Utalii.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...