Na Mwandishi maalum Tunduru

Serikali kupitia bodi ya Korosho Tanzania,inatarajia kuaanza kusajili wakulima wa korosho  ili kuwatambua na kupata idadi kamili  ya wenye sifa  kabla ya kupata  pembejeo za ruzuku kwa msimu wa kilimo 2024/2025 katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.

Hatua hiyo inalenga kurahisisha uendeshaji wa zao la korosho,kupata idadi ya pembejeo zinazotakiwa kwenda kwa wakulima,kupunguza upotevu wa pembejeo na kuondoa adha  kwa wakulima kutafuta na kuuzia pembejeo hizo kwa bei kubwa.

Hayo yamesemwa  na afisa kilimo wa bodi ya Korosho Tanzania Tawi la Tunduru Samwel Kambona,alipokuwa akizungumza na wakulima, wajumbe wa bodi ya chama kikuu cha ushirika(Tamcu) pamoja na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika(Amcos)mjini Tunduru.


Kwa mujibu wa Kambona,hatua hiyo itasaidia bodi hiyo kuwa na takwimu sahihi za wakulima,idadi ya mikorosho na kupima mashamba kwa mfumo wa kidigitali ili kurahisisha utoaji wa huduma za ugani kwa wakulima.


“ Wakulima lazima tuwatambue,mahali walipo na utambuzi huu utakuwa wa kidigitali  ambao utasaidia sana kuwatambua wakulima wanaojihusisha na kilimo cha korosho  katika wilaya yetu ya Tunduru”alisema.

Alisema,zoezi la uhakiki wa wakulima litaanza mwishoni mwa mwezi huu na taarifa hizo zitatumika katika ugawaji wa pembejeo ili kuwaondolea  wakulima  changamoto ya upatikanaji wa pembejeo wakati wa maandalizi ya uzalishaji wa zao hilo.

Amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ruzuku ya asilimia 100 kwa wakulima wa korosho ambapo alisisitiza kuwa,nje ya mfumo huo hakuna mkulima atakayepata viautilifu hivyo badala yake watalazimika kwenda kununua kwa wafanyabiashara.

Kambona,amewaomba wakulima kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi  pindi zoezi  litakapoanza ili kutoa taarifa zao,zitakazo saidia kuondoa malalamiko yaliyojitokeza katika msimu uliopita ambapo baadhi ya wakulima hawakupata viuatilifu vilivyotolewa na serikali.


Mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika wilayani humo(Tamcu Ltd)Mussa Manjaule alisema,kuanzia msimu huu maafisa ugani wa chama hicho watakwenda kwa kila mkulima ili kutoa elimu ya kilimo cha kisasa.

Manjaule,amewataka wakulima wanaolima korosho,ufuta,mbaazi na mazao mengine yanayouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kuhakikisha wanajiunga na ushirika ili waweze kupata huduma za ugani kwa urahisi.

Amewahimiza vijana wa wilaya hiyo kuacha tabia ya kukaa vijiweni na kucheza kamali,badala yake kutumia muda wao kwenda mashambani kulima korosho ili waweze kuondokana na umaskini.

Kwa upande wake afisa kilimo wa Tamcu Grace Evody,amewashauri wakulima kuzingatia na kufuata maelekezo ya wataalam wa kilimo ikiwemo kuokota korosho zilizoanguka ili kupata soko la uhakika na siyo kuchuma zilizo juu ya miti.


Amewataka kutumia mbegu za kisasa zilizothibitishwa na taasisi za serikali zinastahimii magonjwa na hali ya ukame,na kuepuka kununua mbegu za mitaani zinazotoa mavuno kidogo.Afisa kilimo wa chama kikuu cha ushirika wilayani Tunduru(Tamcu)Grace Evody,akitoa elimu ya kilimo bora cha korosho  na mazao mengine ya kimkakati  jana kwa wakulima wa kijiji cha Luginga wilayani humo  kama mkakati wa chama hicho wa kuongeza uzalishaji wa korosho bora zitakazopata soko la uhakika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...