Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi kilichopo Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro kimeanza kuingiza faida zaidi ya shilingi bilioni 36 kutokana na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali wakati uzalisha wa sukari ya majaribio yaliyofanyika mwezi Disemba 2023.

Akibainisha hayo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu Mh, Patrobas Katambi (Mb) wakati wa ziara ya kamati ya kudumu ya bunge ya Ustawi na Maendeleo ya jamii ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mh, Fatma Toufiq ilipotembelea na kujionea maendeleo yaliyofikiwa katika kiwanda hicho.

Naibu Waziri Katambi alisema kiwanda hicho tayari kimeanza kupata faida ya shilingi bilioni 36.36 kutokana na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo molasses (Molasi) ambayo hutumika kama mbolea na mabaki ya nyuzinyuzi (Bagasse) ambayo yanatumika kwa shughuliza uzalishaji wa umeme unaotumiwa katika kiwanda hicho.

Aidha Katambi alikipongeza kiwanda hicho kwa kuendelezea kuwa bega kwa bega na Serikali kwa kuzalisha ajira ambapo mpaka sasa tayari kimeajiri vijana wa Kitanzania 2,600 huku matarajio yakiwa kutoa ajira za kudumu na zisizo za kudumu jumla ajira 11,260.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya jamii Mh, Fatma Toufiq alisema Kiwanda hicho cha Kimkakati kitaenda kupunguza nakisi ya sukari iliyopo ya tani 250,000 kwa kuchangia asilimia 20% ambapo mkakati wa kiwanda hicho ni kuzalisha sukari tani 50,000 kwa ajili ya matumizi ya sukari za viwandani na matumizi ya majumbani.

“Huu ni mradi wa Kimkakati, na kweli ni mkakati mkubwa, kwasababu mwisho wa siku utasaidia kupunguza upungufu wa sukari hapa Nchini, Tumeona miundombinu, Tumeona sukari ambayo imeanza kuzalishwa, lakini pamoja na changamoto ya mvua za Elnino lakini tunaona kabisa kwamba huko mbele kuna mwanga kwa Watanzania” Alisema Fatma Toufiq.

Akizungumza katika ziara ya kamati hiyo, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa NSSF Masha Mshomba ambao ndio wabia wa mradi huo kwa 96% alisema NSSF imepata faraja kuona uwekezaji huo kufikia hatua ya kuanza uzalishaji, kwani lengo la mradi huo ni kuona unaanza kuleta faida ili kurudisha fedha za Wanachama wa mfuko huo.

“Niwaahidi Watanzania wote hususani wanachama wa NSSF, kwamba pesa zao zipo salama, mradi huu utalipa kwa kadiri tulivyokusudua, lakini kikubwa zaidi utasaidia kupunguza nakisi ya sukari hapa Nchini, Ndio maana tunahimizwa tujenge utaratibu wa kuwekeza katika viwanda kama hivi.” Alisema Mshomba.

Kwaupande wake Mtendaji Mkuu wa Kampuni hodhi ya Mkulazi Selestine Some alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa kutoa miongozo ya uwekezaji wa mradi huo uliogharimu shilingi bilioni 344 ambapo umeshaanza kutoa matunda kwa Watanzania.

“Mradi unafaida kubwa sana kwa jamii, mradi umejenga Zahanati inayoweza kuzihudimia jamii zinazozunguuka mradi huo, lakini pia ukipita maeneo ya Dumila utaona shughuli za kiuchumi zikiendelea na kutoa fursa za vijana kujiajiri kutokana na uwepo wa mradi huu. Alisema Some

Sambamba na uwekezaji huo wenye faida za kiuchumi kwa Watanzania, Pia Kampuni hodhi ya Mkulazi imeweza kuzingatia usalama wa Wafanyakazi wake mahala pa kazi kwa kuwapatia vifaa kinga vya kuzuia ajali (PPE)wafanyakazi wake, ambapo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mh, Patrobas Katambi alitoa cheti kwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo kwa kujali usalama wa wafanyakazi mahala pa Kazi.

Meneja wa Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi Mhandisi Aron Mwaigaga akitoa maelezo ya kina juu ya hatua za uzalishaji wa Sukari kiwandani hapo kwa wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na maendeleo ya Jamii wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bi, Fatma Toufiq mapema baada ya kutembelea na kufanya ukaguzi katika Kiwanda hicho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...