Na Is-haka Omar,Zanzibar.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar,kimesema kitawachukulia hatua kali za kisheria baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani wanaotumia vibaya majukwaa ya kisiasa kumdhalilisha na kumdhihaki hadharani Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Mwinyi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,wakati akizungumza na wanachama na viongozi wa Chama hicho huko Jimbo la Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja.

Alisema kuna baadhi ya wanasiasa wanatumia vibaya uhuru wa kutoa maoni na badala yake wanatoa kauli za kumdhalilisha Rais wa Zanzibar Mhe.Dk.Mwinyi huku wakipandikiza kauli za uchochezi kwa wananchi.

Dkt.Dimwa,alivitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria wanasiasa hao na watu wengine wanaovunja sheria kwa makusudi kwa kumdhalilisha Rais wa Zanzibar.


Pia amevitaka vyombo hivyo vya ulinzi kwenda mbali zaidi kwa kuthibiti upotoshaji unaondikwa katika mitandao ya kijamii nchini kwa lengo la kumdhalilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.


“Juzi Chama Cha ACT-Wazalendo wamefanya mapokezi ya Viongozi wao lakini jambo la kusikitisha mikutano yao kwa Unguja na Pemba imepambwa na kauli chafu zilizojaa chuki,visasi,uongo na fitna dhidi ya Rais wetu mpendwa Dk.Hussein Mwinyi,hatuwezi kuvumilia utovu huo wa nidhamu kwani haukubaliki kisiasa,kidini na kitamaduni.


Tabia hizo zinafanya tuanze kutilia mashaka kama kweli wenzetu wana nia ya dhati ya kuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) au wana ajenda zao binafsi kuirejesha Zanzibar katika machafuko ya kisiasa”,alihoji Dkt.Dimwa.

Katika maelezo yake Dkt.Dimwa,amesema CCM itaendelea kulinda kwa vitendo heshima,hadhi thamani ya Rais wa Zanzibar na wasaidizi wake kwani wapo katika mamlaka yanayotokana na Chama Tawala cha CCM kupitia ridhaa halali ya uchaguzi wa Kidemokrasia chini ya matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Naibu Katibu Mkuu huyo Dkt.Dimwa,alisema wananchi wanahitaji siasa za kuvumiliana na ustaarabu sambamba na kuona wananufaika kiuchumi na kijamii huku nchi ikipiga hatua kubwa za maendeleo.

Sambamba na hayo,aliweka wazi kuwa vyama vya siasa Zanzibar vimepoteza muelekeo na mvuto kwa wananchi kutokana na kasi kubwa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Kupitia mkutano huo Dkt.Dimwa,aliwasihi Wanachama na Viongozi wa CCM kujibu hoja kwa hoja huku wakitangaza na kuhamasisha kwa kasi kubwa mambo yaliyotekelezwa na Serikali Mijini na Vijijini kwa maslahi ya wananchi.
 

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akizungumza na Wanachama wa CCM Zanzibar.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...