WAZIRI Wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi. Hamad Masauni amezitaka jumuiya za kiraia kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia kanuni, uwazi na uwajibikaji bila kumomonyoa maadili ya kitanzania na hiyo ni pamoja na kusajili jumuiya hizo ili ziweze kutambulika.

Masauni amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa Uzinduzi wa kampeni za Usajili wa Jumuiya Nchini uliobebwa na kauli mbiu ya " Usajili na Usimamizi wa Jumuiya Kwa Maendeleo na Ustawi wa Taifa Letu.

"Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia kamati za usajili za mikoa inasisitiza usimamizi wa usajili wa jumuiya za kiraia na kuhakikisha zinafanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu." Amesema.

Masauni amesema kuwa, Serikali inatambua jitihada za jumuiya hizo katika kuleta matokeo chanya ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo afya na elimu hivyo usajili ni muhimu katika kutambulika pamoja na kujenga ushirikiano wa karibu na Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

" Usajili wa jumuiya hizo utarahisisha utekelezaji wa majukumu, ushirikiano pamoja na uwazi kwa Serikali kuhakiki mapato na matumizi ya jumuiya hizo.... Serikali kupitia Wizara tupo tayari katika kushirikiana na kutatua changamoto ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao." Amefafanua.

Pia amezitaka kamati za ulinzi na usalama za mikoa na Wilaya kufanyia kazi maoni na mapendekezo ya jumuiya hizo pamoja na viashiria hatarishi kutokana na kuibuka kwa wimbi la watu kutumia mwavuli wa jumuiya hizo kufanya shughuli haramu za usafirishaji haramu wa binadamu, silaha, kupenyeza ajenda za kigeni, uchochezi na dawa za kulevya.

"Kamati za ulinzi na usalama zitatue migogoro ya taasisi za dini pamoja na kufanyia kazi vivuli vya jumuiya zinazofanya biashara haramu kupitia jumuiya hizo...." Amesema.

Uzinduzi huo uliohudhuriwa na makatibu Tawala wa mikoa, Wilaya, wawakilishi wa Baraza la usalama wa Taifa, wanajumuiya na Wakurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi umelenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusiana jumuiya hizo zikiwemo za kidini, taaluma na jamii.

Pia Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Ally Gugu amesema, Kampeni hiyo imelenga kukumbushana kanuni, usajili na miongozo pamoja na madhara ikiwa jumuiya hizo hazitasimamia katika kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kuwa Serikali inatambua jitihada zao kupitia kazi zinazofanya katika ngazi mbalimbali za Mikoa.

Kwa upande wake Naibu katibu Mkuu TAMISEMI Sospita Mtwale ameeleza kuwa, wao ni wadau muhimu katika kusimamia utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo za kijamii kwa mujibu wa sheria pamoja na kupitia taarifa za mapato na matumizi kupitia ofisi za mikoa.

Amesema uzinduzi huo ni agenda muhimu ya kuendeleza shughuli za usajili na usimamizi wa jumuiya hizo na kuelekeza kamati za ulinzi na usalama za mikoa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kusimamia jumuiya hizo kwa kuhakikisha zinatekeleza majukumu yake kwa kufuata kanuni, taratibu na tamaduni za Tanzania.

Aidha amesema kuwa wataendelea kufuatilia na kuchukua hatua dhidi ya Jumuiya zitakazobainika zinafanya kazi kinyume na taratibu.

Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema, uongozi wa Mkoa huo inatambua jitihada za Wizara hiyo katika usajili wa vyama vya jamii pamoja na kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali wakiwemo watendaji wa Kata.

Amesema, wataendelea kuhamasisha wananchi wanaoendesha vyama vya kiraia kujisajili ili waweze kufanya shughuli zao kwa amani.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi. Hamad Masauni akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo na kuzitaka jumuiya hizo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia kanuni, uwazi na uwajibikaji. Leo jijini Dar es Salaam.

Msajili wa Jumuiya za Kiraia Nchini, Emmanuel akizungumza katika uzinduzi huo na kueleza kuwa hadi kufikia Januari mwaka huu kuna jumla taasisi za kiraia 10,690 na Wizara ya mambo ya ndani kupitia ofisi ya Msajili wa Jumuiya imekuwa iliendelea na uhakiki na uhishaji wa vyeti lengo likiwa kutambua jumuiya ambazo zipo hai na nyingine ambazo hazipo tena. Leo jijini Dar es Salaam.



Matukio mbalimbali wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...