Na. WAF - Dar Es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya imevitaka vituo vyote vya Afya nchini kuanzisha kliniki maalum za kupima Magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa Kisukari, Shinikizo la Juu la Damu (Presha) pamoja na kuwapima Selimundu (Sikoseli) watoto wanaozaliwa katika vituo hivyo.

Hayo yamebainishwa leo Machi 7, 2024 na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alipofanya ziara katika Kituo cha Afya Chanika kwa lengo la kuangalia hali ya utoaji huduma ambapo ameridhishwa na huduma za Afya zinazotolewa katika kituo hicho kilichopo Jijini Dar Es Salaam.

“Nawapongeza sana wataalam wa kituo hiki cha Afya cha Chanika kwa huduma nzuri mnazozitoa, lakini pia kuwa na kliniki za magonjwa yasiyoambukiza, Sasa hivi tunataka kuona kila kituo cha Afya nchini kuwa na kliniki za magonjwa hayo hususan upimaji wa ugonjwa wa Kisukari, Shinikizo la Juu la Damu pamoja na Sikoseli.” Amesema Waziri Ummy

Aidha, Amesema watoto wanaozaliwa na ugonjwa wa Sikoseli wakianza kupata matibabu mapema inasaidia kuondoa fikra potofu kwa baadhi ya wazazi kuwa na imani za kishirikina kwa kudhani watoto wao wamerogwa kwa kuwa mtoto asipogundulika mapema huwa anaumwa mara kwa mara.

Aidha, Waziri Ummy amesema miondombinu ya majengo itaongezwa katika Kituo hicho cha Afya Chanika ili iweze kupadishwa hadhi na kuwa Hospitali ya ngazi ya kwanza kwa kuwa kituo hicho kinafanya kazi kubwa ya kuwadumia wananchi wengi zaidi.

“Katika kituo hiki kwa siku wanatoa huduma za kuzalisha wanawake 30 hadi 50 kwa siku hali ambayo ukifananisha na baadhi ya Hospitali za Wilaya idadi hiyo ndio wanaozalishwa kwa mwezi, pia kituo hiki kwa mwezi kinaona wagonjwa kati ya 700 hadi 800, hii ni kazi kubwa na nzuri inayofanywa ma kituo hiki cha Chanika.” Amesema Waziri Ummy

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Jiji Dkt. Zaituni Hamza ameishukuru Serikali na kuipongeza Wizara ya Afya chini ya Waziri Mhe. Ummy Mwalimu kwa kuendelea kuwatia moyo watumishi wa Afya kwa kuthamini kwa kile wanachokifanya hasa kutoa huduma bora kwa wateja.

“Lakini pia tunamshuku Mhe. Waziri kuelekeza kituo hiki kuwa na hadhi ya Hospitali baada ya kukamilisha vigezo vilivyobakia ikiwemo kuongeza baadhi ya majengo, kitu hiki kikiwa Hospitali itasaidia kupunguza msongamano wa wateja kwenda katika Hospitali nyingine kama Muhimbili na Amana.” Amesema Dkt. Zaituni









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...