6 Machi 2024, Kibaha Pwani

Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimeiomba Serikali kufanya mabadiliko katika sheria zake ili kuwaongezea muda wa Siku za Likizo ya Uzazi Wafanyakazi Wanawake wanaojifungua watoto njiti ili kutoa fursa ya kuwahudumia watoto hao sambamba na kupata muda wa kupumzika ili wanaporejea kazini waweze kulete tija katika maeneo yao ya kazi.

Wito huo umetolewa na Afisa Elimu Kazi wa TUGHE, Cde. Nsubisi Mwasandende alipoambatana na ujumbe wa wawakilishi kutoka Kamati ya Wawake TUGHE Makao Makuu pamoja na uongozi wa TUGHE Mkoa wa Pwani walipotembelea na kutoa msaada katika wodi ya Wanawake waliojifungua Watoto njiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi leo Jumanne 5 Machi 2024.

Cde. Mwasandende ameeleza kuwa sheria ya sasa ya Ajira na mahusiano kazini imekuwa ikitoa siku 84 kwa wanawake wanaojifungua mtoto mmoja na pia siku 100 kwa wanaojifungua zaidi ya mtoto mmoja na wala haisemi chochote kuhusiana na wanawake wanaojifungua Watoto njiti ndio maana TUGHE imeona ni vyema mara kwa mara kuendelea kuikumbusha Serikali kufanya mabadiliko ambayo wataongeza kipengele kuhusiana na kuongezewa Siku za Likizo ya Uzazi kwa Wanawake wanaojifungua Watoto njiti.

“Wapo wanawake wengi watumishi wamekuwa wakijifungua watoto njiti na muda wanaopata kukaa na watoto unakuwa hautoshi kwa kuzingatia watoto hao huitaji sana uangalizi wa karibu kutoka kwa mama zao ili waweze kukua na pia afya zao kuimarika hivyo tunaomba sana serikali iweze kuliangalia upya jambo hili kwa kufanya mabadiliko katika sheria zake” alieleza Cde. Mwasendende.

Kwa upande wa Sekta Binafsi, Cde. Mwasandende amewaomba waajiri nchini katika mikataba yao ya hali bora kuingiza kipingele hiki cha kuongeza muda kwa siku za likizo ya uzazi kwa wanaojifungua watoto njiti kama ambavyo mwishoni mwa mwaka jana 2023 Chama cha TUGHE waliweka kipengele hicho katika Mkataba wake wa Hali Bora na kuwa Chama cha kwanza cha Wafanyakazi Nchini kufanya hivyo katika Mkataba wake wa hali bora.

Naye Mwenyekiti wa Wanawake TUGHE Makao Makuu, Cde. Agness Ngereza amesema katika kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani wameona ni vyema kuwatembelea na kutoa msaada katika wodi ya wanawake wanaojifungua watoto njiti sambamba na kuzungumza nao kufahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili na kutoa wito kwa wadau wengine kufanya matendo ambayo yataigusa jamii yenye uhitaji. Pia ameushukuru uongozi wa hospitali ya Tumbi kwa kuwakaribisha sambamba na kuwapongeza kwa huduma nzuri wanayotoa hospitalini hapo.

Akizungumza kwa niaba ya wanawake waliolazwa wodini hapo ambao wamejifungua watoto njiti, Dada Sikitu ameushukuru uongozi wa TUGHE kwa kuwatembelea na kuwapa msaada na kuwaomba waendelee kuwasemea changamoto zao pasipo kuchoka mpaka pale zitakapopatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wa Uongozi wa Hospitali hiyo umeipongeza TUGHE kwa kuwakumbuka watoto hao ambao wanahitaji msaada na kutoa rai kwa Watanzania wote kujitoa kwa hali na mali ili kuwawezesha watoto hao kukua.

Imetolewa na:

Idara ya Habari na Uhusiano kwa Umma

TUGHE Makao Makuu




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...