WAZIRI wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa utoaji wa leseni za madini kwa kampuni za Nyati Mineral Sands na Kampuni ya Tembo Nickel Refining yenye kiwanda cha uchenjuaji wa madini ya metali, unatarajiwa kukuza uchumi wa nchi kupitia ukusanyaji wa mapato, kodi na tozo mbalimbali, kutoa ajira na kuongeza fursa za biashara.

Ameyasema hayo leo Machi 21, 2024 jijini Dodoma wakati wa hafla ya kukabidhi leseni hizo na kufafanua kuwa kabla ya leseni hizo mbili kutolewa leo, nchi ilikuwa na jumla ya leseni 19 za uchimbaji mkubwa wa madini na leseni za viwanda vya usafishaji wa madini 6, hivyo kwa kutolewa kwa leseni hio kunaongeza idadi ya leseni za uchimbaji mkubwa kufikia 20 na leseni za viwanda vya usafishaji wa madini kufikia 7.

”Katika kampuni ya ubia ya Nyati Mineral Sands Limited zitawekezwa dola za marekani milioni 127.7 na mradi utaanza kuzalisha faida baada ya miaka 4 na miezi 6. Kutokana na uwekezaji huu Serikali itanufaika na kukusanya mapato takribani dola za marekani milioni 437.96 kutokana na gawio la hisa za Serikali, kodi na tozo mbalimbali, fursa za ajira za moja kwa moja zipatazo 150 ikijumuisha ajira 140 za Watanzania na 10 za wageni, kuongezeka kwa fursa za biashara, na kuimarika kwa hali ya kiuchumi na ustawi wa jamii kutokana na uwepo wa miradi ya huduma za jamii zitakazotolewa kupitia utaratibu wa Corporate Social Responsibility (CSR)”, alisema Mhe. Mavunde.

Ameongeza kuwa, Wizara katika kuhakikisha kuwa inatatua changamoto zinazojitokeza kwenye sekta ya madini nchini, inaendelea kufanya mazungumzo na wawekezaji wa nyanja mbalimbali ikiwemo utafutaji, uchimbaji na ujenzi wa viwanda vya usafishaji madini ili kwa njia ya kuingia ubia na Watanzania, hivyo kuongeza wigo wa upatikanaji wa mitaji, utaalam pamoja na uhaulishaji wa teknolojia.

“Kiwanda cha usafishaji wa madini kitawekezwa kwa dola za marekani milioni 500 ambapo kiwanda hicho kinatarajiwa kutatua changamoto iliyokuwepo kwa wachimbaji wa madini nchini kulazimika kusafirisha makinikia ya metali kwenda kwenye viwanda vya nje ya nchi kwa ajili ya uchakataji ili kupata zao la mwisho au kuuza madini katika hali ya makinikia kwa bei ya chini. Aidha, makinikia yatakayozalishwa kwa njia ya ‘flotation’ katika mgodi wa Kabanga na mingine nchini yataweza kuchakatwa na kuzalisha metali zenye ubora wa asilimia 99.9”, alimalizia Mhe. Mavunde.

Akimuwakilisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Mhe. Constantine Kanyasu amempongeza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga mazingira mazuri kwa wawekezaji yanayotoa fursa ya kuendelea kuwekeza na kufanya sekta ya madini iendelee kuwa bora katika uchangiaji wa mapato ambapo utolewaji wa leseni hizo unaonesha dhahiri kuwa azma ya Rais Samia kuhusu sekta ya madini inaendelea kufikiwa. Pia, ametoa rai kwa wawekezaji hao kuanza kazi katika muda uliopangwa.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Lifezone Metals, Chris Showalter akizungumza wakati wa kukabidhiwa Leseni ya Uchenjuaji madini kwa niaba ya Kampuni ya Tembo Nickel, amesema kuwa makabidhiano hayo ni zaidi ya suala la uchimbaji madini pekee kwani inaandaa jukwaa pana litakalobeba kitovu cha uchimbaji, uchakataji na uchenjuaji wa madini ndani ya Ukanda Maalum wa Kiuchumi wa Buzwagi wilayani Kahama mkoani Shinyanga. Vile vile, Kampuni hiyo itaendeleza utekelezaji wa maono ya kuleta manufaa na ongezeko la thamani ya madini ndani ya Tanzania kwani ni lengo la pamoja kuhakikisha Tanzania inanufaika moja kwa moja na rasilimali zake zilizo ndani ya nchi.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni za Nyati Mineral Sands, Jozsef Patarica amesema kuwa anaamini kuwa miradi yao nchini Tanzania italeta ajira, uhamisho wa ujuzi, mapato kwa nchi, pamoja na manufaa mengine mengi na leseni hiyo mpya ya madini itatoa njia kwao kuendeleza awamu inayofuata ya mradi wa Fungoni na Tajiri kwani wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii juu ya chaguzi mbalimbali za ufadhili kwa miezi mingi, hivyo kwa ruzuku ya Leseni Maalum ya Uchimbaji Madini, kampuni hiyo inatarajia mijadala ya ufadhili kuekelezwa kwa haraka.


 Serikali kupitia Wizara ya Madini imekabidhi Leseni Kubwa ya Uchimbaji wa Madini Tembo ( Heavy Mineral Sands) kwa Kampuni ya Nyati Mineral Sands Limited na Leseni ya Usafishaji wa Madini ya Nickel kwa Kampuni ya Tembo Nickel Refining Company Limited. Makabidhiano hayo yamefanyika jijini Dodoma na kushuhudiwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde. Aidha, tukio hilo pia limekwenda sambamba na uhuishaji wa Leseni ya Uchimbaji wa Madini ya Dhahabu kwa Mgodi wa Bulyanhulu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...