Na Mwandishi wetu, Mirerani

Viongozi wa dini, wa Serikali, wanachama na wakereketwa wa CCM wa Wilaya ya Simanjiro, Mkoani Manyara, wamefanya maombi ya kuliombea Taifa kwa kutimiza miaka 60 ya muungano wa Tanzania.

Maombi hayo yamefanyika mji mdogo wa Mirerani yakiongozwa na viongozi wa madhehebu mbalimbali huku mgeni maalum akiwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Manyara Peter Toima.

Mwenyekiti Toima ambaye alikuwa mgeni maalum wa maombi hayo amesema wameshiriki ili kuwaombea viongozi wa Taifa waweze kuendelea kuongoza nchi kwa kumtanguliza Mungu.

"Mimi ni nani nikatae fursa ya kuwa mgeni maalum kwenye tukio hili ambalo mgeni rasmi ni Mungu mwenyewe," amesema Toima.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Fakii Lulandala amewashukuru viongozi wa dini, wa serikali, wa CCM na wananchi kwa ujumla kwa kushiriki maombi hayo ambayo kiwilaya yamefanyika mji mdogo wa Mirerani.

"Maombi haya yatafikia tamati Aprili 26 mji mdogo wa Orkesumet mbapo ndipo yalipo makao makuu ya wilaya kwa kuweka TV kubwa kwa ajili ya wananchi kusikiliza hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan," amesema Lulandala.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Manyara, Peter Toima ambaye alikuwa mgeni maalum wa maombi hayo amesema wameshiri ili kuwaombea viongozi wa Taifa waweze kuendelea kuongoza nchi kwa kumtanguliza Mungu.

Mchungaji Kefa Simon amesema Taifa linapaswa kuwaongoza wananchi wake kwa kutenda haki kwani lisipofanya hivyo litakuwa linatenda dhambi.

Mchungaji Yohana Ole Tiamongoi amesema wanawaombea viongozi wa Taifa waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo kwa kuongoza vyema.

Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) Simanjiro Warda Abeid Maulid amesema maombi hayo pia yameshirikisha watumishi wa serikali na wananchi kwa ujumla.

"Tunawapongeza wote waliofanikisha maombi haya wakiwemo viongozi wa madhehebu ya dini, viongozi wa serikali, viongozi wa CCM na wote walioshiriki hadi mwisho," amesema DAS Warda.

Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Anthony Jacob amesema tukio hilo limevuta hisia za wananchi wa eneo hilo kwani wameshiriki na kuomba kwa pamoja na viongozi.

Sheikh wa Wilaya ya Simanjiro, Ibrahim Idd amewaasa wakazi wa mkoa wa Manyara, kuwalinda watoto kwa kuwaepusha na vitendo vya ukatili kwani vimekithiri hivi sasa.

Sheikh Idd amesema wazazi na walezi wanapaswa kuwa makini na malezi ya watoto ikiwemo kutowaruhusu watoto wa kiume kulala na ndugu zao wakubwa wa kiume.

"Mambo ya mjomba kulala chumba kimoja au kitanda kimoja na mtoto wa kiume yamepitwa na wakati kwani anaweza kufanyiwa vitendo vibaya na kusababisha matatizo," amesema sheikh Idd.

 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...