Na Jane Edward, Arusha
Umoja wa wauza Vinyago kwenye soko la Masai Market Mjini Arusha wenye wanachama zaidi ya 200 wamemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi wa Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda na kumuomba awabakizie Mkoani hapa kutokana na namna alivyoimarisha uwajibikaji kwenye ofisi za umma mkoani Arusha.
Wajasiriamali hao wametoa kauli hiyo mapema leo wakati walipokuwa wakimshukuru Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha mara baada ya kufanikisha kurejeshewa kiwanja chao kilichopo Meserani Juu ambacho waliporwa na mmoja wa Wanachama wao wa zamani kwa takribani miaka 20 iliyopita.
Kulingana na Wajasiriamali hao, kiwanja chao walichokuwa wamechangishana fedha, walikusudia kujenga soko kubwa la vinyago ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya soko litakalopatikana wakati wa mashindano ya kandanda kwa timu za mataifa ya Afrika maarufu kama AFCON yanayotarajiwa kufanyika kwenye nchi za Tanzania, Uganda na Kenya mwaka 2027.
Wajasiriamali hao wameonesha kushangazwa na umahiri wa Mhe. Makonda katika utatuzi wa kero mbalimbali na kumuomba kuendelea kuwa na kliniki za mara kwa mara ili kuweza kuwasaidia wakazi wa Arusha wenye kukabiliwa na changamoto na kero mbalimbali.
Katika Hatua nyingine mjasiriamali Priscila Godson ametangaza kuanza mfungo wa kutokula na kunywa kwa siku 10 ili kuanza maombi maalum ya kumuombea Mhe. Mkuu wa Mkoa akisema anayoyafanya yanawasirisha wasiopenda haki na hivyo amemua kumkabidhisha Mhe. Makonda mikononi mwa Mungu anayemuamini ili aweze kumlinda na kumtunza kwa maslahi ya wahitaji na maskini wa Mkoa wa Arusha.
Wajasiriamali hao wamekaririwa wakisema kuwa aliyekuwa Katibu Mkuu wao na mtunza nyaraka wa Umoja wao Bi. Elizabeth Lumuniko Mengele ndiye aliyebadilisha nyaraka za kiwanja walichokuwa wamekinunua miaka 20 iliyopita na kwa kipindi chote hicho waliikosa haki yao licha ya kuwa na misururu ya kesi mahakamani na vikao kadhaa vilivyokuwa vinaitishwa na kusimamia na viongozi mbalimbali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...