KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu, Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa wito kwa Mfuko wa Kimataifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund) kuendelea kuipatia fedha Tanzania kwa ajili ya kuendelea kutekeleza miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi inayotekelezwa maeneo nchini.
Mhandisi Luhemeja amesema hayo leo Jumatatu (Mei 13, 2024) Jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa kubadilishana uzoefu kwa Nchi Wanachama zinazotekeleza Miradi inayosimamiwa na Mfuko wa Kimataifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund) ulioshirikisha Watendaji na Watalaamu wa Serikali na sekretarieti ya Mfuko huo.
Mkutano huo utaainisha maeneo mahsusi ya kipaumbele na mikakati mbadala ya kuweza kusaidia kukabuliana na atahari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Mhandisi Luhemeja ameushukuru Mfuko huo kwa kuipatia fedha Tanzania na kuahidi Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itahakikisha kuwa fedha zinazotekelewa zitaendelea kuelekezwa katika miradi ya kipaumbele iliyoanishwa na mfuko huo hususani miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ameongeza kuwa ajenda ya mazingira ni moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita na kutokana na umuhimu huo Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kusimamia vyema miradi inayolenga kukabiliana na atahari za mabadiliko ya tabianchi iliyotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ili kuweza kuzisadia jamii.
Amesema kutokana na umuhimu wa ajenda ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi Mazingira NEMC limeialika sekretarieti ya mfuko huo pamoja na Nchi Wanachama kuja Tanzania ili kujifunza majukumu, mafanikio na changamoto inazopitia NEMC kuona miradi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini inavyoweza kukabiliana na madhara ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa vitendo,
Kwa mujibu wa Mhandisi Luhemeja amesema mkutano huo baina ya NEMC na Mfuko huo utasaidia kupatikana njia mbadala za kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi ikiwemo uchimbaji wa visima vya maji, mbinu za kisasa za umwagiliaji mashambani, ufugaji wa kisasa na jinsi mbinu hizo zinavyoweza kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa maeneo husika.
Aidha Luhemeja ameuomba mfuko huo pia kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa Baraza hilo ili kuweza kusimamia vyema miradi ya mabadiliko ya tabianchi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Nimezungumza na Sekretarieti ya Mfuko na kuwaomba umuhimu wa kuipatia fedha Tanzania hususani NEMC na pia kujenga uwezo kwa watendaji wetu…Sisi kama Serikali tumejipanga kuhakikisha tunakuwa na kampeni maalum ya kuhamasisha jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi” amesema Mhandisi Luhemeja.
Amefafanua kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha jamii umuhimu wa kuhifadhi na kutunza mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, juhudi ambazo zinaungwa mkono kwa vitendo na Viongozi Wakuu wa Kitaifa akiwemo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango.
Mhandisi Luhemeja amesisitiza wajibu wa jamii na wananchi kwa ujumla kutunza na kuhifadhi mazingira ikiwemo kujenga utamaduni wa kupanda miti kwani pamoja na miti kuzuia uharibifu wa mazingira pia upandaji miti ni fursa ya kibiashara ambayo itaziwezesha jamii kujiongezea kipato cha kaya na familia kwa ujumla.
Amefafanua kuwa katika kuhamasisha jamiii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira hususani katika kipindi hiki cha kuelekea Wiki ya Mazingira Duniani, Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kushirikisha makundi mbalimbali ya kijamii ili kuhakikisha suala la mazingira linaendelea kuwa ajenda muhimu katika Maisha ya kila siku ya jamii, familia na kaya.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mfuko huo, Bw. Farayi Madziwa amepongeza Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa juhudi mbalimbali inazoendelea kuzifanya katika kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Ameongeza kuwa Mfuko huo utaendelea kutoa fedha na kujenga uwezo wa kitaalamu kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kueleza kuwa mfuko huo umevutiwa na utekelezaji wa miradi ambayo imeweza kuleta manufaa na matokeo chanya katika jamii ya Watanzania.
“Tumeleta Mataifa mengine yaje kuona na kujifunza namna miradi ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi inavyoweza kubadili maisha ya wananchi wetu na kwa dhati tunaipongeza Tanzania kwa jinsi ilivyoweza kupiga hatua kubwa katika usimamizi na utekelezaji wa miradi hii” amesema Madziwa.
Mkutano huo wa siku tano unahusisha wataalamu mbalimbali wa Serikali kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, (NEMC, Nchi zinazotekeleza Miradi inayosimamiwa na Mfuko wa Adaptation Fund na Sekretarieti ya Mfuko huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...