Mkutano wa 14 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Uratibu wa Sera za Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika leo tarehe 30 Aprili 2024 jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo wa ngazi ya Mawaziri umepokea taarifa ya utekelezaji wa maelekezo na maazimio yaliyofikiwa katika Mikutano iliyotangulia ya Baraza hilo katika Sekta ya Uratibu wa Sera za Nje, iliyowasilishwa baada ya Mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 27 Aprili 2024.
Mbali na kupokea taarifa hiyo Mawaziri hao pia wamejadili mapendekezo ya maeneo ambayo Nchi Wanachama zinaweza kuwa na msimamo wa pamoja katika majukwaa ya kimataifa, utoaji wa hadhi maalum ya uangalizi kwa kamisheni na mashirika ya kimataifa, Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Uratibu wa Sera za Nje na suala la kuwa mwakilishi wa Jumuiya katika Umoja wa Afrika.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliohudhiriwa na Nchi zote Wanachama wa Jumuiya, umeongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato.
Aidha Mkutano huo ulifuatiwa na Mkutano wa 12 wa Pamoja wa Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri wa Ushirikiano katika Ulinzi, Mambo ya Ndani na Uratibu wa Sera za Mambo ya Nje.
Akifungua Mkutano huo uliohusisha sekta tatu Naibu Katibu Mkuu, Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia miundombinu, uzalishaji, jamii na siasa Bw. Andrea Ariik Malueth, ameeleza kuwa mkutano huo pamoja na masuala mengine una jukumu kubwa la kuhakikisha unalinda misingi, uhuru na kuimarisha ulinzi na usalama katika Jumuiya.
Hali kadhalika Mkutano huo ngazi ya Mawaziri ulikuwa makhususi kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa iliyowasilishwa kwao na mkutano ngazi ya Makatibu Wakuu wanaosimamia masuala ya Ulinzi, Mambo ya Ndani na Sera za Mambo za Nje katika nchi Wanachama.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato achangia mada kwenye Mkutano wa 14 wa Baraza la Kisekta Mawaziri wa Uratibu wa Sera za Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Dar es Salaam, 30 Aprili 2024
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax akichangia mada kwenye Mkutano wa 12 wa Pamoja wa Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri wa Ushirikiano katika Ulinzi, Mambo ya Ndani na Uratibu wa Sera za Mambo ya Nje wa EAC uliofanyika jijini Dar es Salaam, 30 Aprili 2024
Mkutano wa 14 wa Baraza la Kisekta Mawaziri wa Uratibu wa Sera za Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukiendelea
Meza kuu wakiongoza Mkutano
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...