MBUNGE wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu ameishauri Wizara ya Mifugo na Uvuvi kukaa na wizara za kisekta ili kusaidia wakulima na wafugaji kuondokana na migogoro.

Amesema migogoro mingi ya wakulima na wafugaji hutokana na kutotengwa maeneo halisi ya wafugaji na hali hiyo imepelekea malalamiko katika maeneo mbalimbali nchini .

Hayo ameyasema bungeni leo wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2024/25 ambapo amesema suala hilo likifanyika litafanya mfugaji asionekane ni yatima.

“Kwa sababu kuwa na mifugo mingi kama ulivyosikia wengine wakisema si laana ni rasilimali kila mmoja anajivunia alichonacho

Hivyo naomba migogoro hii iweze kutatuliwa kwa amani ili wananchi wote waweze kufurahia mifugo yao.”

“Mheshimiwa Waziri kaa na wizara zingine zinazohusiana na wizara hii ziweze kusaidia wakulima na wafugaji kuondokana na migogoro hii,lakini mfugaji wa nchi hii asionekane ni yatima, kwa sababu kuwa na mifugo mingi, kama ulivyosikia wengine si laana ni rasilimali kila mmoja anajivunia alichonacho,la pili, naomba migogoro hii iweze kutatuliwa kwa amani ili wananchi wote waweze kufurahia mifugo yao, “ameongeza.

Aidha, Mtaturu ameshauri wataalam wa uvuvi wawepo wa kutosha watakaofanya tathimini ya mifugio kwenye maeneo yao ili kuwaondolea mzigo wataalam wa kata na vijiji wanaofanya kazi kubwa kwa niaba ya wizara.

“Kwenye eneo la wataalam unaweza kuwa na mipango mizuri kwenye level ya wizara lakini kule chini kwenye halmashauri hatuna wataalam huko, wa uvuvi, leo tunalia kule kwa sababu watalaam wa kata na vijiji ndio wanafanya kazi kubwa, kwa niaba ya wizara, Niombe sana tuongeze watalaam, waende wakafanye tathimini ya mifugo kwenye maeneo yetu, “amesema Mtaturu.

Kuhusu ujenzi wa majosho, amebainisha kuwa kwenye eneo hili kuna deni kwakuwa aliomba majosho manne hata hivyo hadi sasa lipo moja tuu hivyo kushauri yaongezwe.

“Nilikuomba majosho manne, umenipa moja katika kata ya Ntuntu lakini kuna josho muhimu lipo katika kata ya Siuyu, lile josho linatakiwa liondolewe katika maeneo ya kanisa niombe sana lile josho mnijengee ili wananchi wale waendelee kupata huduma za kuogeshea mifugo yao na kuweza kusaidia inenepe vizuri.”

Pia, ameomba kujengwa majosho ya kuogeshea na kulishia mifugo katika maeneo ya Issuna, Mang’onyi, Unyahati na Siuyu kwakuwa uhitaji ni mkubwa.

PONGEZI WA RAIS SAMIA.

Mtaturu amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya katika kusimamia maendeleo ya nchi ambapo kupitia sekta zote kazi kubwa imefanyika hata kwenye sekta ya mifugo na uvuvi.

Aidha, amempongeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, Naibu Waziri Alexander Mnyeti, Katibu Mkuu Profesa Riziki Shemdoe kwa kazi kubwa wanazofanya.

“Sekta hii ni muhimu kwa uchumi wa nchi lakini chakula kama ambavyo tumekuwa tukielezwa kama siku ya protini ambayo ipo kwenye viwanja vya bunge, tumeambiwa kitakwimu tuna ng’ombe milioni 37.6 lakini tuna mbuzi na kondoo wa kutosha.”

Amesema kuwa maana yake ikitumika vizuri rasilimali hii inaweza kubadilisha uchumi wa nchi yetu na kuongeza pato la taifa kama mipango ikiwekwa vizuri.

“Ninamaani kabisa tukitumia rasilimali hii vizuri tukajipanga vizuri kulingana na mipango ambayo umetuambia, lakini tumpongeze Rais ametuongezea bajeti kutoka bilioni 169 hadi bilioni 460 ni zaidi ya asilimia 63 imeongezeka,”amesema Mtaturu.

Amebainisha kuwa maana yake ni kwamba kuna dhamira ya dhati kwa serikali kuhakikisha kwamba yale ambayo ni matamanio ya wizara hii kuwekeza rasilimali watu kupitia mipango mbalimbali ikifanyiwa kazi vizuri itaongeza uchumi wa wizara hii kwa kiasi kikubwa.

Aidha, ameipongeza wizara kwa bandari ya uvuvi kilwa masoko huku akieleza kuwa uwekezaji huo wa zaidi ya sh. bilioni 286 utawezesha meli zinazopaki eneo hilo kupeleka samaki inapotakiwa jambo ambalo litaongeza uchumi mkubwa katika sekta ya uvuvi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...