Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), jana Mei 16 ameshiriki na kuchangia katika Mkutano wa Jumuiya ya Ulaya (EU) unaojadili upatikanaji wa Madini adimu (Critical Minerals ) huko Brussels nchini Ubelgiji.

Akichangia kwenye Mkutano huo, Prof. Mkumbo amesema kuwa Tanzania ina sehemu muhimu katika kufanikisha agenda ya dunia katika kuyafikia mabadiliko ya matumizi ya nishati ya kijani kwani imejaaliwa kuwa na rasilimali zinazohitajika.

Hivyo, Prof. Mkumbo ametumia fursa hiyo kuwatoa hofu wadau wa maendeleo wa nchi za Jumuiya ya Ulaya na washiriki wa Mkutano huo kuwa ni vyema wakaondoa hofu za kimtazamo kwamba, uwekezaji wa viwanda vya uchakataji wa madini adimu ni ghali kufanyika Afrika ukilinganisha na Ulaya.

“Kuna idadi kubwa ya rafiki zetu kutoka upande wenu (Magharibi), ambao bado wanafikiri kuwa ni vigumu na ghali kuwekeza viwanda vya uchakataji na uongezaji thamani wa madini adimu Afrika na Tanzania, ninawaambia kila vilivyo vizuri ni ghali, ni vigumu lakini vinawezekana, ninawakaribisha kuwekeza Tanzania na mtafurahi”, Alisema Prof. Mkumbo.

Aidha, katika mchango wake Waziri huyo mwenye dhamana ya Mipango na Uwekezaji nchini amesisitiza kuwa Tanzania ina Sera zilizo wazi zinazolenga kujenga uchumi shindani.

Prof. Mkumbo amesema kuwa, utekelezaji wa Sera hizo unalenga kuleta mapinduzi katika sekta ya uzalishaji ili kukabiliana na mahitaji makubwa ya ajira akitolea mfano kwa Tanzania ambayo takribani aslimia 76 ya wananchi wake ni vijana chini ya miaka 35 na kwamba kundi hili linahitaji kuhudumiwa kupitia uwekezaji wa viwanda vya uzalishaji vikiwemo vile vya uchakataji wa madini adimu.

“Ninachowaambia washirika wetu wa maendeleo, ni kwamba wakati huu tubadili fikra kutoka kuagiza Nikeli kutoka Afrika badala yake kuingiza Betri kutoka Afrika” Alisema Prof. Mkumbo na kuongeza kuwa, tutakuwa na furaha ifikapo 2050 Dunia itakaposhinda vita dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi, Afrika nayo ishinde vita dhidi ya umasikini.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Umoja wa Ulaya (EU) unaojadili upatikanaji wa Madini ya Kimkakati (Strategic Minerals), Brussels nchini Ubelgiji unaongozwa na Warizi wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), alieyembatana na Katibu Mkuu, Dkt. Tausi Kida, Bw. Kheri Mahimbali, Katibu Mkuu- Wizara ya Madini, pamoja na wataalamu na wawekezaji mbalimbali kutoka sekta binafsi na sekta ya Umma kutoka nchini Tanzania.
 

Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji (aliyevaa Suti nyeusi) katika picha na Bw. Koen Doens, Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Ulaya pembezoni mwa Mkutano wa Jumuiya ya Ulaya kuhusu Upatikanaji wa Madini ya Kimkakati. Mei 16, 2024, Brussels Ubelgiji.
 

Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji (wa pili kushoto), Katibu Mkuu, Dkt. Tausi Kida (wa kwanza kushoto), Bw. Kheri Mahimbali (wa pili kulia) Katibu Mkuu Wizara ya Madini na Mhe. Jestas Abuok Nyamanga, Balozi wa Tanzania nchini Ubeligiji, katika picha ya pamoja pembezoni mwa Mkutano wa Jumuiya ya Ulaya kuhusu Upatikanaji wa Madini ya Kimkakati. Mei 16, 2024, Brussels Ubelgiji.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...