Mwenyekiti wa Bodi ya wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMeT), Bi. Faraja Nyalandu akitoa hotuba yake kwenye kilele cha Madhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa (Global Action Week for Education au GAWE) kwa mwaka huu 2024 yaliyofanyika katika Viwanja wa CCM, Kalangalala, mkoani Geita.

Baadhi ya Wanafunzi wakiimba na kufurahia shughuli za Madhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa (Global Action Week for Education au GAWE) kwa mwaka 2024 yaliyofanyika katika Mkoa wa Geita.

Sehemu ya Wanachama wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), wakiwa katika ziara kutembelea shule mbalimbali mkoani Geita, ikiwa ni shughuli za GAWE 2024.

Kaimu Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Martha Makala akizungumza kwenye moja ya ziara za wadau wa elimu katika Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa (GAWE) kwa mwaka huu 2024.

MTANDAO wa Elimu Tanzania (TEN/MET) umechangia fedha kiasi cha shilingi 18,650,000 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya ufundishaji mkoani Geita ikiwa ni kuguswa na changamoto za elimu zilizobainishwa kwenye Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa (Global Action Week for Education au GAWE) zilizofanyika katika mkoa huo.

Akizungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa (Global Action Week for Education au GAWE) kwa mwaka 2024 yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM, Kalangalala Mkoa wa Geita, Mwenyekiti wa Bodi ya TEN/MET, Bi. Faraja Nyalandu alisema fedha hizo zimetolewa na Sekretariati ya Mtandao wa Elimu Tanzania kwa kushirikiana na wanachama wake, zikielekezwa kwenye maeneo yenye changamoto walizozibaini.

Akifafanua namna fedha hizo zitakavyotumika, Mwenyekiti huyo wa Bodi alisema wadau hao wa elimu wametengeneza darasa la mfano la elimu ya awali lililopo katika Shule ya Msingi Nyanza lilogharimu takribani Tshs 5,650,000, pamoja na kugharamia uezekaji wa mabati kwenye madarasa mawili ya wanafunzi wa awali na vyumba vya walimu Shule ya Msingi Chabulongo kiasi cha Tshs 7,000,000. 

Mtandao pia unachangia gharama za kuweka umeme kwenye nyumba saba za walimu na madarasa sita kwenye shule ya Sekondari Bung’wangoko kiasi cha Tshs 6,000,000 hivyo jumla ya fedha yote iliyotolewa na wanachama hao wa Mtandao wa Elimu kufikia Shilingi 18,650,000,” alisema.

Pamoja na hayo aliwataka viongozi wa Mkoa wa Geita na wadau wengine kuangalia namna ya kuzitatua baadhi ya changamoto ambazo zimebainishwa katika Maadhimisho ya Juma la Elimu mkoani Geita, ikiwemo wanafunzi wengi wa shule za msingi na sekondari kutembea umbali mrefu kufika shuleni na kurejea nyumbani, hali inachangia utoro shuleni.

“…Changamoto nyingine ni utolewaji wa chakula shuleni, ambapo muamko wa wazazi wengi ni wa kusuasua, hali inayopelekea watoto wengi kukosa chakula wawapo shuleni na kupelekea mahudhurio hafifu udhoofu wa kiafya na akili kwa wanafunzi wanaoshinda njaa. Wakiwa shuleni, Mfano mmojawapo ni kuwa tulipotembelea Shule ya Sekondari Mgusu hapa Geita tulijulishwa kuwa kati ya wanafunzi 700, wanafunzi 30 pekee ndio wazazi wao wamechangia chakula shuleni. 

“…Hali kadhalika, Ipo changamoto ya upungufu wa walimu; takwimu zinaonyesha kuwa Mkoa wa Geita una upungufu wa walimu 7,770 kwa shule za msingi na walimu 1,725 kwa shule za sekondari. Hali hii pia  tumeishuhudia katika shule ya Sekondari Mgusu yenye jumla ya wanafunzi 700 na walimu 12 tu. Pia tulibaini kuwa kuna upungufu wa walimu wa kike katika shule tulizotembelea,kwa mfano Shule ya Sekodari Bung’wangoko ina walimu 19 kati yao walimu wa kike ni  2 tu,“ alibainisha Mwenyekiti wa Bodi ya TEN/MET, Bi. Nyalandu.

Pamoja na changamoto zingine, wadau hao wamependekeza Serikali na wadau wengine kuhakikisha kuwa majengo yote yanayojengwa yanazingatia miundo inayowezesha watoto wenye ulemavu kupata elimu bila shida yeyote, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu kuhusu namna ya kuwahudumia watoto wenye ulemavu. 

“Pamoja na hatua nzuri iliyochukuliwa na serikali pamoja na jamii katika kutatua changamoto ya uhaba wa walimu,tunashauri jamii,azaki za kiraia kuendelea kuchangia posho za walimu wa kujitolea ili kupunguza Uhaba wa walimu uliopo mkoani Geita ukilinganisha na idadi kubwa ya wanafunzi waliopo shuleni. Tunawahimiza wazazi na walezi kuendelea kuchangia chakula shuleni ili wanafunzi wapate chakula wakiwa shuleni na kusoma bila njaa ili kuongeza ufaulu wao na kupunguza utoro shuleni.” Alisisitiza Bi. Nyalandu katika hotuba yake.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...