Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Mkamba amefanya mazungumzo na Wawekezaji kutoka nchini Ireland ambao wapo ziarani nchini kuangalia na kufanya tathimini ya fursa za uwekezaji zinazopatika katika sekta mbalimbali.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 8 Mei 2024 yalilenga kubalishana taarifa mbalimbali na uzoefu katika sekta ya biashara na uwekezaji ambazo zitawasaidia wawekezaji hao katika kufanya maamuzi kwenye utekelezaji wa mikakati ya kuwekeza nchini.
Waziri Makamba akizungumza na wawekezaji hao ameelezea mageuzi ya kimkakati yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kutengeneza mazingira rafiki ya uwekezaji chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Aliendelea kueleza kuwa licha ya mazingira tulivu ya kisiasa nchini, mageuzi yaliyofanywa katika maeneo mbalimbali ikiwemo sera na sheria za uwekezaji yameendelea kuifanya Tanzania kuwa kituo bora cha uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa upande wake kiongozi wa msafara wa ujumbe wa wawekezaji hao Bw. Miar Gunnarsson ambaye pia ni Mwanzilishi wa Kampuni ya Baridi Group Ltd amesifu uwepo wa fursa lukuki nchini walizozibaini wakati wa zaira yao, kwenye sekta mbalimbali kama vile utalii, ujenzi, uvuvi, madini, kilimo na viwanda.
Vilevile Bw. Gunnarsson ameeleza kuridhishwa kwakwe na kuvutiwa na jitihada zinazoendelea kufaywa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, ambayo yanawapelekea kuichagua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za kipaumbele kwenye mipango yao ya uwekezaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi John Ulanga ameeleza kuwa pamoja na masuala mengine kuongezeka kwa kasi ya ukuaji uchumi nchini ni moja ya kigezo kinachowavutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza.
Wakiwa nchini Wawekezaji hao watakutana na kufanya mazungumzo na viongozi na watendaji Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali.
Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi John Ulanga akifanua jambo wakati wa mazungumzo na Wawekezaji kutoka nchini Ireland yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam
Sehemu ya Wawekezaji kutoka nchini Ireland wakifuatilia
mazungumo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Mkamba (Mb.) akifanua jambo wakati wa mazungumzo na Wawekezaji kutoka nchini Ireland yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...