SHAHIDI wa tatu wa upande wa mashtaka, Kiran Lalit Ratilal katika kesi ya kujeruhi na kutoa lugha ya matusi inayowakabili wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54), ameshindwa kutoa ushahidi wake mahakakani kwa sababu wakili wa utetezi anayewatetea watuhumiwa hao anahudhuria kesi nyingine mahakama ya Rufaa.

Wanandoa hao ambao ni raia wa Tanzania wenye asili ya kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanakabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kujeruhi wanayodaiwa kuyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.

Kesi hiyo iliitwa mahalamani leo Juni 3, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa mashtaka lakini iliahirishwa.

Mapema Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga alidai kuwa wanaye shahidi mmoja na wapo tayari kuendelea na kusikiliza ushahidi lakini upande wa utetezi ulidai kuwa ni kweli kesi ipo kwenye hatua ya kusikilizwa ila kwa bahati mbaya siku ya ijumaa walipata barua kutoka Mahakama ya Rufaa.

"Mheshimiwa hakimu ni kweli kesi imekuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa lakini kwa bahati mbaya siku ya ijumaa tulipokea barua kutoka Mahakama ya Rufaa, kwa hiyo wakili ameenda huko,"alidai Wakili Mwanaisha Mshobozi

Kufuatia taarifa hiyo kutoka kwa Mwanaisha, Wakili Grace alidai kutokana na maombi hayo hawana pingamizi, wanaomba wapangiwe tarehe nyingine ya usikilizwaji ambapo alipendekeza iwe Julai, mwaka huu.

Hata hivyo Hakimu Lyamuya alisema Julai ni mbali sana na ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 25, 2024 kwa ajili ya usikilizwaji, ambapo shahidi Kiran Lalit alionywa na mahakama kufika tarehe hiyo kwa ajili ya kutoa ushahidi.

"Shahidi kwa bahati mbaya Wakili wa washtakiwa hayupo, tumeelezwa hapa yupo Mahakama ya Rufani, unatakiwa tarehe tutakayopanga uwepo mahakamani,"alisema Hakimu

Awali, Fundi Seremala, Dominic Mpakani (43) aliileza mahakama jinsi mshitakiwa Bharat Nathwan allivyomshambulia jirani wake, Lalit Ratilal kwa kumpiga kichwa kifuani kisha akadondoka chini na nakupoteza fahamu kwa muda.

Aidha, alidai kuwa kulikuwa na ugomvi kati ya mke wa Bharat (Sangita Bharat) na mke wa Lalit, (Kiran) ambao walikuwa wakirushiana maneno kwa ukali kwa lugha ya kihindi huku, baada ya muda kidogo waume zao walifika kwa pamoja na kuingilia ugomvi huo.

Alidai kuwa Julai 21,2023 alikuwa nyumbani kwa Lalit Ratilal maeneo ya mtaa wa Mrima katika jingo la Lohana, alimuita kwa ajili ya kuifanyia kazi zinazohusiana na mbao na kazi zingine ndogo ndogo.

Alidai kuwa alifika katika jengo hilo saa tatu asubuhi ambapo bosi wake huyo anakaa floor ya tatu, wakati anaendelea na kazi alidai kuwa Sangita alikuwa amesimama kwenye mlango lake na Kiran alikuwa amesimama kwenye mlango wake, ambapo Sangita Bharat alianza kuzungumza kwa ukali na kwa jaziba akitumia lugha ya kihindi.

"Lakini nilimsikia mke wa Bharat, Sangita akimwambia mke wa Lalit kwamba uchafu wake apeleke huko ambapo vitu vyote vilikuwa vimewekwa katika eneo la Lalit na hakuna kitu chochote kilichokuwa katika eneo la Sangita. Baada ya dakika kadhaa sijui walipiga simu au vipi waume zao walikuja kwa wakati mmoja na malumbano ya maneno yakaendelea kwa wote wanne," alidai Fundi Mpakani

Shahidi huyo alidai kuwa, wakati malumbano ya maneno hayo yanaendelea wote walikuwa wamesimama kwenye mlango wa Lalit, baada ya muda Bharat akampiga kichwa Lalit na Lalit akadondoka chini na kupoteza fahamu.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao ambao ni raia wa Tanzania jinsia ya kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jingo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashitaka manne waliyoyatenda Julai 21,2023.

Katika shitaka la kwanza la kujeruhi linalomkabili Nathwani peke yake, ambapo anatuhumiwa Julai 21,2023 akiwa eneo la mtaa wa Mrima-Kisutu, jingo la Lohana, ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kinyume cha sheria alimsababishia madhara makubwa Kiran Lalit kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo la saruji iliyochanganywa.

Pia, katika shitaka la pili la shambulio la mwili linalomkabili Nathwani peke yake, ambapo tarehe hiyo na eneo hilo alimsababishia madhara Lalit Ratilal katika mwili wake kwa kumpiga kichwa, ngumi na mateke kichwani.

Ilidaiwa kuwa katika shitaka la tatu na la nne linalomkabili Sangita peke yake, ambapo anatuhumiwa kutoa matusi makubwa dhidi ya Lalit na Kiran kitendo ambacho kilileta fujo kwa namna ambayo inaweza kuleta uvunjifu wa amani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...