-Nishati Safi ya Kupikia yapigiwa chapuo
-Wananchi wafurahia kuuona mradi wa JNHPP kupitia kifaa cha Uhalisia Pepe
-TANESCO yatoa huduma moja kwa moja ikiwemo ya Nikonekt
-Wananchi wajulishwa haki zao kupitia EWURA CCC

Wizara ya Nishati pamoja na taasisi zilizo chini yake imeshiriki kwa mafanikio katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi yaliyoanza tarehe 16 Juni 2024 katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma ambayo yatahitimishwa tarehe 23 Juni 2024.

Katika Maadhimisho hayo, Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zake wamejipanga kikamilifu kuhudumia wananchi wanaohitaji huduma mbalimbali kuhusu Sekta ya Nishati.

Pamoja na kutoa huduma kwa wananchi, Wizara ya Nishati pia inatoa elimu kuhusu utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa za Nishati Safi ya Kupikia, utekelezaji wa miradi ya umeme, Mafuta na Gesi Asilia.

Aidha, katika Banda la Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC) Wananchi wanajionea moja kwa moja shughuli za uchimbaji wa Gesi Asilia, usafirishaji na uchakataji wake kupitia teknolojia ya Uhalisia Pepe ( Virtual Reality) pamoja na kuelezwa juhudi za Serikali katika uendelezaji wa Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia.

Vilevile, katika banda la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wananchi wanaona moja kwa moja utekelezaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere ( JNHPP) kupitia kifaa cha Uhalisia Pepe, wanapata huduma ya kuunganishwa umeme kupitia mfumo katika simu janja wa Nikonekt, wanapata elimu ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia majiko ya kupikia yanayotunza umeme, kushughulikiwa changamoto za mita pamoja na kupata elimu ya mabadiliko ya mita za LUKU.

Kupitia Banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wananchi wanapata huduma moja kwa moja za Nishati Safi ya Kupikia kupitia wadau wa usambazaji na waendelezaji wa teknolojia husika, elimu ya usambazaji umeme vijijini na vitongojini na uendelezaji wa miradi midogo ya umeme.

Taasisi nyingine za Wizara ya Nishati zinazoshiriki Maadhimisho husika ni Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli ( PURA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ambao wanatoa elimu kwa umma kuhusu shughuli za udhibiti.

Aidha, Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA CCC) wameshiriki maonesho husika ambapo wanatoa elimu kuhusu haki na wajibu wa watumiaji wa huduma za nishati na maji, ikiwa ni taasisi inayosimama kama sauti ya watumiaji wa huduma husika

Maadhimisho ya mwaka 2024 yamebebwa na kauli mbiu isemayo “Kuwezesha Utumishi wa Umma Uliojikita kwa Umma wa Afrika ya Karne ya 21 Uliyojumuishi Na inayostawi; Ni Safari ya Mafunzo Na Mabadiliko ya Kiteknolojia"Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...