Watumishi wa kada mbalimbali wa Wilaya ya Mvomero wakiongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Bw. Saidi Nguya wameunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha na kutangaza vivutio vya utalii hapa nchini kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Julai 6, 2024 Bw. Saidi Nguya amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani amekuwa mtu wa kwanza kuhakikisha kuwa Sekta ya utalii inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa ndiyo maaana amekuja na program ya Royal Tour kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii hapa nchini.

Aidha, ameongeza kuwa Rais Samia amefanya kwa nafasi yake hivyo, watumishi wa Wilaya hiyo nao wanawajibu wa kuhamasishana ili kuonesha mchango wao katika kutanga na kuhamasisha utalii.“...sisi kwa nafasi yetu hapa kwenye ngazi ya Wilaya, Kata, Tarafa na ngazi ya Vijiji tunawajibu wa kuhamasishana sisi kwa sisi tuoneshe mchango wetu...” amesema Katibu Tawala.

Sambamba na hilo Bw. Saidi amebainisha kuwa moja ya majukumu yao kama wasaidizi wa Rais ni kutafsiri maono ya Rais Samia kulingana na mazingira waliyopo.

Katika hatua nyingine Katibu Tawala huyo amesema kuwa lengo mojawapo la ziara hiyo ni kuwapa nafasi wahudumu, waandishi waendesha ofisi na watunza kumbukumbu kutoka Taasisi mbalimbali za Wilaya hiyo ili wapumzike na kufurahia kutokana na kwamba kundi hilo limekuwa halitazamwi vizuri.

Bw. Saidi ameongeza kuwa ubora wa ofisi unaanzia kwa kundi hilo kwa sababu ni kundi linalopokea wateja wengi, hivyo kundi hilo linatakiwa kupewa kipaumbele ili kupunguza ama kuondoa kabisa malalamiko ya wateja kuhusu ofisi au Taasisi husika.

Naye Afisa Uhifadhi wa hifadhi ya Taifa ya Mikumi Bw. David Kadomo amewapongeza watumishi hao kwa ziara yao kwani wanahamasisha utalii wa ndani na kutoa rai kwa Wilaya zingine kuiga mfano wa Mvomero.

Aidha, ameongeza kuwa Sekta ya utalii inachangia zaidi ya asilimia 17 kwenye pato la taifa hivyo kuna umuhimu wa kutunza hifadhi. Sambamba na hilo amepongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutangaza utalii ndani na nje ya nchi hali ambayo imechangia kuongezeka kwa idadi ya watalii kufikia 100033 katika hifadhi ya Mikumi kwa mwaka huu.

Kwa upande wao Watumishi wa Wilaya ya Mvomero akiwemo Bw. Issaya Ramson ambaye ni Mtunza Kumbukumbu amesifu juhudi za Rais Samia kwa kuhamasisha utalii hapa nchini huku akitoa wito kwa Wilaya zingine kutembelea hifadhi hiyo.

Pia, amebainisha kuwa hifadhi hiyo ina wanyama mbalimbali kama vile Tembo, Twiga, Swala, Pundamilia, nyoka na ndege mbalimbali.Naye Bi. Raheli Mgoni ambaye ni Mwandishi Mwendesha Ofisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero amesema jambo la watumishi hususani wa kada za waandishi waendesha ofisi, wahudumu na watunza kumbukumbu kutembelea hifadhi ya Mikumi halijawahi kufanyika, hivyo siku ya leo wamepata nafasi ya kubadilishana uzoefu na watumishi wengine lakini pia kujifunza masuala ya kitalii.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...