Na Mwandishi Wetu,Tunduru

KATI ya vijana 240 walioteuliwa na Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma mwaka 2024 kwenda kujiunga na chuo cha Ufundi Nazareth kilichopo Mbesa wilayani humo ni vijana 6 tu ndiyo walioripoti hadi kufikia tarehe 31 Julai na kati ya hao mmoja amekimbia na hivyo kuwa na vijana 5.


Aidha,walioteuliwa kwa mwaka wa masomo uliopita 2023 walikuwa 114, lakini wanaoendelea hadi sasa na mafunzo ya ufundi ni 8 huku wengine 106 wameingia mitini hawajulikana walipo na hivyo kushindwa kutumia vema fursa ya uwepo wa Chuo hicho kwenye wilaya hiyo.


Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya Tunduru iliteua wanafunzi waliohitimu darasa la saba na kidato cha nne mwaka 2023 na 2024 ili kujiunga kwenye mafunzo ya ufundi ili waweze kupata ujuzi katika fani mbalimbali zitakazo wawezesha kupata ujuzi ambao utawasaidia katika maisha yao.


Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa chuo hicho Ezekiel Mapunda,wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kumalizika kwa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya chuo cha Nazareth Mbesa kinachomilikiwa na Wamisionari wa Kanisa la Bibilia Duniani.


Mapunda alisema,chuo cha Ufundi Nazareth Mbesa kilianzishwa kwa lengo la kuwapa vijana wa Kitanzania elimu ya ufundi ili waweze kujitegemea katika maisha yao na wakati kinaanzishwa mwaka 1974 walianza na fani ya Useremala na ilipofika mwaka 1976 waliongeza fani ya magari na mwaka 1994 walianzisha fani nyingine ya uchongaji na ukelezaji vyuma na uchomeaji.


Kwa mujibu wa Mapunda,ilipofika mwaka 2017 fani mbili mpya za umeme wa majumbani,ushonaji nguo na mapambo zilisajiriwa ili kupanua wigo zaidi kwa watoto wa kike kujiunga na chuo ili nao waweze kujitegemea mara watakapomaliza mafunzo na kozi hizo zinatolewa kwa muda wa miaka mitatu.

Alisema, mwaka 1974 wakati chuo kinaanzishwa walianza na wanafunzi 8,lakini kwa sasa kuna wanafunzi 150 kati yao 110 wanaishi bweni na 40 wanatoka nyumbani.


Alisema,walifundisha kwenye mazingira magumu kwa kutumia chaki kwa sababu walimu wengi walikuwa Wazungu,hivyo suala la mawasiliano la lugha lilikuwa gumu kwa wanafunzi waliokuwepo wakati huo.


Hata hivyo,kwa sasa wamepiga hatua kubwa katika suala la ufundishaji kwani wanafundisha kwa kutumia projekta na wamefunga mtandao wa Internet wenye kasi unaowawezesha kupata vifaa vya kufundishia kwa ajili ya kuongeza uelewa kwa wanafunzi badala ya kufundisha kwa chaki.

“uelewa wa mtu unapanuka zaidi anapoona na kusikia,kwa hiyo utaratibu wa uwasilishaji wa mada nyakati hizi ni bora na nzuri sana kuliko mwanzoni kulingana na mazingira ya sasa hivi na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia”alisema Mapunda.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa pili wa Shirika la misaada la Makanisa ya Bibilia Dunian Klaus Brinkmann,amewataka Wanafunzi wa chuo hicho kutumia ujuzi na elimu wanayoipata kufikiria kwenda kujitegemea kwa kujiajiri badala ya kuwaza kuajiriwa Serikalini.

Brinkmann alisema,zaidi ya wanafunzi 1000 wamehitimu mafunzo ya fani mbalimbali tangu chuo kilipoanzishwa mwaka 1974,ambapo wengi wa vijana waliohitmu wamepata kazi kwenye taasisi na idara za Serikali na wengine kujiajiri.


Alisema,mafanikio hayo yametokana na malengo waliyokuwa nayo na kutumia vizuri elimu waliyopata wakiwa katika chuo hicho ambacho ni mojawapo ya vyuo vikongwe hapa nchini.

Pia amewataka kwenda kufanya kazi kwa weledi,kuwa wabunifu,waaminifu na kutengeneza bidhaa bora pindi watakapomaliza mafunzo yao ili kujenga imani kwa wateja kwenye maeneo yao iwapo wanataka mafanikio.

Akitoa salamu za Mkuu wa tatu wa Misheni Mbesa Karl Warth,Mkuu wa sita wa Misheni hiyo Helga Armbruster alisema,wakati wanaadhimisha miaka 50 ya chuo hicho baadhi ya watu wametoa fedha na michango yao ili kufanikisha malengo ya kuwawezesha vijana wa Tunduru kupata ujuzi utakao wasaidia katika maisha yao.

Karl Warth,amewapongeza wafanyakazi wa chuo kwa kazi nzuri wanazozifanya katika kuimarisha na kuboresha elimu ya ufundi ambayo imewasaidia baadhi ya vijana wa Kitanzania hususani wanatoka wilaya ya Tunduru kujitegemea.

Kwa upande wa wahitimu wa chuo hicho mwaka 1993 walisema,chuo cha Ufundi Nazareth Mbesa kimewapa mafanikio makubwa na wamekuwa tegemeo kwa familia,jamii na Taifa ikiwemo kuwapa ufundi vijana wenzao wa Kitanzania katika fani mbalimbali.

Hata hivyo katika risala yao iliyosomwa na Selestine Kalo,wameshauri chuo kuleta vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia kutokana na kukua kwa teknolojia hasa uwepo wa magri yanayotumia gesi.


Vile vile,wameiomba jamii,kukiamini na kutumia fursa ya uwepo wa chuo cha Ufundi Misheni Mbesa kupeleka watoto wao kupata ujuzi utakaowasaidia kufanya kazi za kujiletea maendeleo na kujikwamua na umaskini.







 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...