Afisa Habari Mkuu DART Bw. Elias Malima (kulia) akitoa maelezo jinsi ya kutumia Programu tumizi ya Mwendokasi App kwa Kaimu Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa Dkt. Yusuph Mashala, Agosti 06 2024 pale alipotembelea banda la Oisi ya Rais TAMISEMI kwenye maonyesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Muonekano wa utumiaji wa APP ya mabasi yaendayo haraka

Na.Mwandishi Wetu,Dodoma.
Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART umeendelea kutoa Elimu ya Matumizi ya Programu tumizi ya Mwendokasi App kwenye viwanja vya maonyesho ya Kitaifa ya Nanenane Nzuguni Dodoma kwa lengo la kupanua wigo wa matumizi mifumo ya kidigitali katika usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka.

Akizungumza katika Banda la Ofisi ya Rais TAMISEMI ambalo Wakala wa DART ni moja ya Taasisi zilizo chini yake, Afisa Habari Mkuu wa Wakala huo Bw. Elias Malima alisema wakati huu ambapo Wakala unaendelea kukamilisha usimikaji wa mageti janja katika vituo vya Mabasi Yaendayo Haraka wananchi wanashauriwa kuipakua programu hiyo ili iwarahisishie katika ukataji wa tiketi za safari.

“Mwendokasi App inarahisisha sana ukataji wa tiketi kwa kutumia simu janja wakati huu ambapo tunaendelea kukamilisha usimikaji wa Mageti janja (smart gates) yatakayoruhusu matumizi ya Kadi janja (Smart card) katika mabasi yaendayo haraka. Ukataji wa tiketi kupita simu unasaidia kupunguza foleni na kuondoa kero ya kukosekana kwa chenchi” Alisema.

Aidha, alisema kwakuwa Tanzania ya sasa ni ya kidijitali DART kama moja ya Taasisi za Serikali haiko nyuma katika kuhakikisha inaendelea kuboresha mifumo yake ya TEHAMA ili kupunguza usumbufu kwa watumiaji wa Mabasi lakini pia kudhibiti uvujaji wa mapato ya serikali unaoweza kujitokeza kutokama na matumizi ya tiketi za karatasi.

“Sasa hivi dunia imebadilika na mifumo ya TEHAMA imerahisisha ufanyaji wa malipo mbalimbali ya Serikali ndiyo maana kila mara Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan anasisitiza taasisi kuongeza matumizi ya mifumo, hivyo nasisi tumejikita katika kuimarisha mifumo ya kidijitali ili kusimamia ukusanyaji wa mapato” Alisema.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa - LGTI Dkt. Yusuph Mashala alitembelea Banda la Ofisi ya Rais TAMISEMI katika maonesho hayo aliwapongeza DART kwa ubunifu na namna ambavyo wanatumia mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa nauli.

“Nawapongeza kwa namna ambavyo mnatumia teknolojia katika ukusanyaji wa nauli. Nashauri muongeze ubunifu zaidi na kubuni mifumo mingi ambayo itasaidia katika kurahisisha ukataji wa tiketi za Mabasi Yaendayo Haraka Pamoja na kurahisisha usafiri kwa ujumla”Alisema.

Ofisi ya Rais TAMISEMI Pamoja na taasisi zake ambazo ni DART, TARURA, Tume ya Utumishi wa Walimu, Chuo cha Serikali za Mitaa ,Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa, na Shirika la Elimu Kibaha wameshiriki Maonyesho ya Kilimo Nanenane mwaka 2024 yakibeba kaulimbiu ya “Chagua viongozi bora wa Serikali za Mitaa kwa maendeleo endelevu ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...