NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR

Asasi ya NMB Foundation kwa kushirikiana na kampuni ya Mwani Zanzibar (ZASCO) wamezindua mafunzo endelevu kwa Wakulimwa wa Mwani Unguja na Pemba, ambapo Serikali ya Mapunduzi ya Zanzibar (SMZ) imeipongeza na kuitaja asasi hiyo kama mbia wa karibu, wa kimkakati na wa muda wote wa maendeleo Zanzibar.

Mafunzo hayo ya miezi mitatu kwa wakulima zaidi ya 1,300 kutoka vikundi 72 vya wakulima, yamefunguliwa na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban, yakiwa ni zao la makubaliano ya ushirikiano yaliosainiwa Machi mwaka huu kati ya NMB na Kampuni ya Mwani Zanzibar (ZASCO).

Akifungua mafunzo hayo, Waziri Omar alizipongeza NMB Foundation na ZASCO kwa kuyaingiza makubaliano yao katika vitendo kwa lengo la kuelimisha wakulima juu ya kilimo cha kisasa, upatikanaji mikopo nafuu ya kilimo na kuwajengea uwezo wa elimu ya fedha kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Machi mwaka huu tulikutana Dar es Salaam kusaini makubaliano haya, tunaposimama hapa leo tunaingia kwenye utekelezaji wa lile. Nawapongeza kwa sababu taasisi nyingi zinasaini makubaliano, lakini ‘perfomance’ hakuna, NMB na ZASCO mmeenda mbali zaidi katika hili.

“Mafunzo haya yanalenga kujikita katika maeneo matatu ya elimu ya fedha, elimu ya kilimo na uzalishaji na mwisho uwezeshaji wa kifedha kwa maana ya mikopo nafuu kwa wakulima wetu, mambo yatakayowaongoza kulima kwa tija, kutunza fedha zitokanazo na mazao, lakini kupata mitaji.

“Nawapongeza sana NMB kwa jitihada zenu zisizokoma katika kuunga mkono Ajenda ya Serikali ya Zanzibar ya Uchumi wa Buluu. Hakika sote ni mashahidi wa namna mnavyosaidiana nayo katika utatuzi wa changamoto mbalimbali za Wazanzibar.

“Kama kuna mbia wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambaye ni mbia wa karibu zaidi, mbia wa kimkakati, lakini pia mbia ambaye wazungu wanamuita ‘of the all seasons,’ iwe mvua, kiangazi au masika, basi ni Benki ya NMB, imekuwa ikishirikiana na Serikali katika mazingira yoyote yale,” alisema Waziri huyo.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ZASCO, Masoud Rashid Mohammed, alisema mafunzo hayo sio tu zao la makubaliano ya taasisi zao katika kukuza uzalishaji wa mwani, bali ni uthibitisho wa mlinganyo wa kimalengo waliyonayo, huku akizitaka taasisi zingine za fedha kuiga mfano wa NMB.

“Mheshimiwa Waziri alisisitiza vipaumbele vitatu vya awali kuwa ni Ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata Mwani Pemba, alisisitiza hilo akisema ndio kipaumbele chake cha kwanza, cha pili na cha tatu, lengo linalokaribia kutimia kwa sababu ujenzi unaendelea kwa kasi na kufikia mwakani kitaanza kazi.

“Na katika kuhakikisha kiwanda hakikosi malighafi za kuchakata, ndipo yalipozaliwa makubaliano yetu na NMB na leo tuko hapa kuzindua mafunzo kwa wakulima 1,300 ili kuhakikisha tunakuza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya kiwanda hiki, tukianza na vikundi 33 vya Pemba na 39 vya Unguja,” alibainisha Masoud.

Naye Meneja Mkuu wa NMB Foundation, Nelson Karumuna, alimshukuru Waziri Omar Shaaban kwa kuwa sehemu ya hafla ya awali ya kusainiwa makubaliano na hatimaye ufunguzi wa mafunzo hayo, akisema ushiriki huo unaakisi dhamira ya SMZ katika kuwaletea maendeleo ya Wazanzibar.

“Mafunzo haya yamelenga kuwezesha wakulima kupata elimu ya fedha, uwezo wa kimtaji kwa maana ya mikopo ya fedha na zana za kilimo. Unaweza kujiuliza kwanini tumechagua kuwapa na elimu ya fedha wakulima hawa, jibu ni kuwa ndio muongozo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

“Benki Kuu imesema wazi kuwa elimu ya fedha ni nguzo muhimu sana katika kukuza uelewa wa kufanya KilimoBiashara, sasa sisi tunajielekeza katika hiyo elimu ya fedha, NMB Benki wao watawezesha katika suala zima la mikopo na ZASCO watafikisha elimu sahihi ya kilimo.

“Sisi tunaamini kuwa Programu hii ya mafunzo tunayoizindua leo, itaenda kuwa chachu ya kukuza uzalishaji wa zao la Mwani hapa Zanzibar. Mafunzo yataanza hivi punde tuna omba ushirikiano mkubwa tutapoenda huko kuwapa mafunzo, yushirikiano kutoka Serikalini, kutoka ZASCO na Wakulima wenyewe,” alisema.

Awali, Mkuu wa Idara ya KilimoBiashara wa NMB, Nsolo Mlozi, alisema taasisi yake inajisikia fahari kufanikisha uanzishwaji wa mafunzo hayo kwa Wakulima wa Mwani ambao ni sehemu ya mnyororo wa thamai wa kilimo unaohusisha kilimo chenyewe, ufugaji, uvuvi na misitu.

“Sekta ya Kilimo ni kati ya Sekta za Kimkakati na za kipaumberle kwa NMB, na ndio sababu iliyotusukuna kushirikiana na NMB Foundation katika kuwanoa wakulima hawa, nasi tunaahidi mikopo nafuu ya fedha na zana za kilimo ili kukuza uzajilishaji wa zao hili hapa Zanzibar,” alisema.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...