Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Albogast Kajungu, amesema WMA ina mchango mkubwa katika sekta ya kilimo hususani katika mazao ya kimkakati ambayo ni korosho, ufuta, kahawa, tumbaku na pamba.
Amebainisha hayo Agosti 3, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo maarufu kama NaneNane yanayoendelea katika viwanja vya Nzunguni jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa kazi kubwa ya Wakala wa Vipimo katika sekta hiyo ndogo ya mazao ya kimkakati ni kuhakikisha Mizani zinazotumika katika ununuzi wa mazao hayo zinahakikiwa ili kujiridhisha kuwa ziko sahihi.
“Lengo ni kuhakikisha kwamba mkulima anapouza mazao yake anapata thamani ya pesa sawasawa na mazao aliyouza,” amefafanua Kajungu.
Akieleza zaidi, Mkurugenzi huyo wa Huduma za Ufundi amesema zoezi la kuhakiki Mizani hufanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza huhusisha uhakiki wa mizani kabla ya msimu wa kila zao kuanza ilhali awamu ya pili huhusisha ukaguzi wa kushtukiza wakati wa msimu kwa kila zao ili kujiridhisha kama vipimo vilivyohakikiwa awali vinatumika kwa usahihi.
“Kwahivyo kabla ya msimu tunapita kuhakiki mizani zote zinazotumika kununulia mazao na wakati wa msimu tunapita kujiridhisha kama zinatumika kwa usahihi.”
Aidha, Kajungu ameeleza kuwa, mbali na zoezi la ukaguzi, Wakala wa Vipimo pia hutoa elimu kwa wakulima na wananchi kwa ujumla ili wafahamu sifa za mizani ya kununulia mazao iliyohakikiwa.
Ametaja mojawapo ya sifa za mizani iliyohakikiwa kuwa ni uwepo wa stika ya Wakala wa Vipimo inayoonesha tarehe ambayo mizani husika ilihakikiwa pamoja na tarehe ya mwisho ambayo stika hiyo itakuwa imekoma matumizi yake.
“Kwahiyo mwananchi akiiona ile stika inampa uhakika kuwa mizani hiyo imehakikiwa na Wakala wa Vipimo,” amesisitiza Kajungu.
Vilevile, akizungumzia kuhusu ufungashaji wa mazao ya shamba, ameeleza kuwa kwa mujibu wa sheria, kufungasha mazao ya shamba kwa uzito unaozidi kilo 100 unatafsiriwa kama lumbesa ambayo ni kosa kisheria.
Amesema, kumekuwa na mkanganyiko wa tafsiri ya neno lumbesa ambapo baadhi huitafsiri kama kufungasha mazao ya shamba kwa kuongeza kishungi, ambapo tafsiri hiyo siyo sahihi.
Kajungu ametoa wito kwa wakulima na wananchi kwa ujumla kufahamu kwamba mazao yote ya shamba ni lazima yafungashwe kwa uzito unaokubalika kisheria ambao ni kilo 100.
Akisisitiza kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria ya vipimo, Kajungu amesisitiza umuhimu wa kuwepo vituo vya kununulia mazao ambavyo ni rahisi kuweka mizani iliyohakikiwa na WMA ili itumike kwa wakulima kuhakiki mazao yao na kujiridhisha kwamba yamefungashwa katika uzito wa kilo 100 bila kuzidi ili kupata faida stahiki kwa pande zote mbili yaani muuzaji na mnunuzi.
Wataalamu wa Wakala wa Vipimo wanashiriki katika Maonesho ya NaneNane kitaifa jijini Dodoma na kikanda katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kutoa elimu kwa wadau wa kilimo na wananchi kwa ujumla.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) Albogast Kajungu (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Wakala hiyo, wanaoshiriki katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima NaneNane (2024) yanayoendelea jijini Dodoma.WMA inatoa elimu kwa wadau wa kilimo na wananchi kwa ujumla kuhusu matumizi ya vipimo sahihi.
Afisa Vipimo Mwandamizi kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) akitoa elimu kuhusu umuhimu wa kuhakiki dira za maji katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo Nanenane (2024) yanayoendelea jijini Dodoma.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Wakala wa Vipimo (WMA), Veronica Simba akitoa elimu kuhusu matumizi ya vipimo sahihi katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo NaneNane (2024) yanaoendelea jijini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...