Afisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Limited Tanzania, Ashish Mistry akipiga mpira wakati wa uzinduzi wa Ligi ya ALAF inayotarajiwa kuanza mwezi ujao huku manahodha wa timu tano zitakazoshiriki katika ligi hiyo wakishuhudia. Uzinduzi huo ulifanyika Jijini Dar es Salaam hivi karibuni
Na Mwandishi Wetu, Michuzi Tv
KATIKA kuhakikisha tasnia ya michezo nchini inazidi kukua na kutimiza azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuongeza ushiriki katika nafasi mbali mbali za michezo duniani, kampuni ya Mabati ya ALAF imezindua ligi Kuu yao kwa wafanyakazi wake.
Akitangaza uzinduzi wa ligi hiyo itakayoanza Oktoba 5,2024 ambayo itakayohusisha wafanyakazi wa Alaf, Ofisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Tanzania Ashish Mistry amesema ligi hiyo ina dhamira kubwa ya kukuza michezo kwa wafanyakazi.
"Tumezingatia ushauri wa Rais na tumejitolea kuimarisha ushirikiano wa michezo ndani ya kampuni yetu," amesema Mistry na kuongeza kuwa baada ya kujihusisha na soka kwa miaka minne, ALAF inajitahidi sana kushirikiana na kampuni ya usimamizi wa kitaalamu katika kusimamia ligi".
"Kwenye Kampuni ya ALAF, tunatoa kipaumbele kwa afya ya wafanyakazi wetu, ndiyo maana tuliunda 'Ligi Kuu ya ALAF' inayoshirikisha timu tano za ushindani kutoka idara mbalimbali," ameeleza.
Amesema, ili kuimarisha ushindani wa ligi, ALAF imesajili Kampuni ya ‘Plus One Events Solutions Limited’ kuratibu ligi yao na kwamba ushirikiano huo unaendana na mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuimarisha ushiriki katika michezo nchini kote.
"Pia ligi hii haiishii kwenye michezo tu kwani hupelekea faida nyingi ukizingatia mazoezi ya kawaida ya mwili, yanapunguza hatari ya magonjwa sugu na uboreshaji wa afya ya moyo na mishipa." Ameongezea
"Wafanyakazi wenye afya bora hupunguza gharama za huduma za afya, na kukuza kazi ya pamoja ya vikundi vya michezo na mawasiliano, na huimarisha mahusiano mahali pakazi,"
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa ‘Plus One Events Solutions Limited’ Osman Kazi na mwamuzi mstaafu wa FIFA, ameelezea matumaini yake kwamba mpango wa ALAF utayahamasisha makampuni mengine kuiga mfano huo. "Kwa utaalamu tulionao, tunalenga kuinua Ligi Kuu ya Alaf na kuwavutia wafanyabiashara zaidi kushiriki katika shughuli zinazofanana na hizi,"
Kazi amesisitiza faida za afya ya akili ya michezo, akibainisha kwamba shughuli za kimwili hutoa homoni ya ‘endofini’ inayoweza kupunguza mfadhaiko na kuongeza ari ya kufanya kazi na kutangaza kwamba ligi inatarajiwa kuanza Oktoba 5.
Amon Mwaijage, Meneja Uzalishaji wa ALAF na mratibu wa michezo, amesema sema ligi hiyo itashirikisha timu tano: Simba Dumu, Covermax, Lifestile, Simbachuma, na SafBuild, timu zote zimepewa majina ya bidhaa za ALAF.
"Lengo letu ni kuunda timu yenye umoja, ambayo inawakilisha ALAF katika matukio mbalimbali ya michezo, huku tukikuza kazi ya pamoja ndani ya kampuni," Mwijage alisema. Aliongeza kwamba kuipa afya na siha kipaumbele kunaazisha mfano wa kiutamaduni, na kuwahimiza wafanyakazi kuupa kipaumbele ustawi wao.
"Kuwekeza katika afya ya wafanyakazi kwa njia ya michezo ni mkakati wa muda mrefu ambao unaweza kuleta ukuaji endelevu na mafanikio kwa kampuni yetu," amehitimisha
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...