NA MWANDISHI WETU
MSIMU wa Nne wa Kampeni ya fungua Akaunti, Weka Akiba na Ushinde inayoendeshwa na Benki ya NMB ‘NMB Bonge la Mpango,’ umezinduliwa Dar es Salaam leo, na kwa wiki 12 wateja wa benki hiyo watajishindia mamilioni ya pesa na bidhaa mbalimbali kila wiki, huku mshindi wa jumla akitarajiwa kujizolea Sh. Mil. 100.
Licha ya kuhamasisha wateja wa NMB kuendelea kuweka fedha na akiba kwenye akaunti zao kwa dharura mbalimbali na ustawi wa maisha ya baadaye, NMB Bonge la Mpango ni sehemu ya mpango mkakati wa kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia Huduma Jumuishi za Kifedha.
Kampeni ya NMB Bonge la Mpango ilianza mwaka 2021, kabla ya mwaka uliofuata (2022) kurejea tena kwa kampeni hiyo ikitumia kaulimbiu ya ‘2merudi Tena,’ na baadae ya mwaka 2023 kuitwa NMB Bonge la Mpango ‘Moto Ule Ule’ na mwaka huu kuwa NMB Bonge la Mpango ‘Mchongo Nd’o Huu.’
Kampeni hii imezinduliwa na Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Toba Nguvila na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, mbele ya Mkuu wa Mtandao wa Mauzo na Matawi ya NMB, Doantus Richard na Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Seka Urio.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mponzi alisema kampeni hiyo ya miezi mitatu (Septemba 25 hadi Desemba 19), itahusisha wateja wenye akaunti na wateja wapya watakaofungua akaunti na kuwa na akiba inayoanzia Sh. 100,000, ambako droo zitachezeshwa kila wiki, mwezi na fainali.
“Lengo la kampeni kuongeza idadi ya Watanzania wanatumia huduma za kibenki, lakini pia kuhamasisha utamaduni chanya wa kujiwekea akiba, ambapo sisi kama taasisi bora ya kifedha nchini, tunawazawadia wateja wetu wanaojiwekea akiba zao wenyewe,” alisema Mponzi.
Alibainisha ya kuwa zawadi kuu ya mshindi wa jumla ni Sh. Mil. 100 itakayotolewa katika ‘grand finale’ ambayo washindi wengine 6 watajitwalia trekta za kulimia ‘power tiller’, huku washindi wengine 10 wakijishindia pikipiki za mizigo ya magurudumu matatu maarufu ‘toyo.’
“Lakini tutakuwa na washindi wa kila wiki, ambako wateja wetu 10 watajishindia fedha taslimu Sh. 100,000, huku washindi wengine 9 watajinyakulia kimoja kati ya Friji, Tv ya kisasa, mashine ya kufulia na jiko la gesi kulingana na matakwa ya mteja,” alisema Mponzi.
Kwa upande wa zawadi za droo za kila mwezi, Mponzi alisema benki hiyo itakuwa ikiwazawadia washindi wanne wa kila mwisho wa mwezi Sh. Mil. 5 kila mmoja, ikiwa na maana wateja wanane katika miezi miwili ya kwanza watajizolea Sh. Mil. 40 kwa wote.
Naye Dk. Nguvila, kwa upande wake aliishukuru NMB kwa kuzindulia kampeni hiyo katika eneo la Kariakoo ambalo ni kitovu cha biashara nchini, lakini pia kwa namna inavyojitoa katika masuala ya kijamii, ikiwemo misaada ya vifaatiba na vifaa vya elimu katika hospitali na shule mbalimbali nchini.
Alisisitiza kuwa suala la uwekaji wa akiba ni jambo muhimu katika maisha ya kila siku, ili kumuwezesha mwekaji akiba hususani benki, kumudu kuyakabili masuala ya dharura, lakini pia kujiepusha na upotevu, wizi na hata majanga kama ya moto na uharibifu mwingine.
“NMB ndio benki bora, ndio benki yenye pato kubwa, ndio benki inayotoa gawio kubwa sana kwa Serikali, lakini zaidi ya yote wanayo Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ambayo inasaidia sana utatuzi wa changamoto katika Sekta za Elimu na Afya,” alibainisha Nguvila.
Katibu Tawala huyo alishngazwa na ukubwa wa zawadi zilizowekwa na NMB kwa washindi wa kampeni hiyo, tena kwa kuweka tu akiba itakayomsaidia mwenyewe, huku akiwataka wafanyabiashara wa Kariakoo, kuchangamkia fursa hiyo muhimu ili kukua kibiashara na kiuchumi.
Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo (JWK), Martin Mbwana, aliishukuru NMB kwa kupeleka uzinduzi wa Bonge la Mpango Kariakoo, eneo ambalo lina kumbukumbu kubwa za udhamini mnono wa benki hiyo katika Tamasha la Kariakoo Festival 2024.
“Tunaishukuru sana NMB kwa mambo mengi inayotufanyia, hata ukiangalia ukusaji wao wa madeni ya mikopo, haitumii nguvu badala yake inatuelimisha na hii maana yake ni benki inayopenda uhai na ustawi wa wafanyabiashara na biashara zetu,” alisema Mbwana.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...