Katika jitihada za kuwafikia wadau wa ununuzi wa umma hususan wazabuni, Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeweka mkakati wa kutoa elimu kwa wazabuni katika kanda zote nchini.
Akiongea na waandishi wa Habari kuhusu mkakati huo, pembezoni mwa Kongamano la 16 la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki Jijini Arusha, Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), Bw. James Sando amesema Mamlaka imeweka mkakati huo ili kuweza kuzifikia kanda nne (4) ambazo hazijapatiwa elimu ya jinsi ya kuwasilisha mashauri yao pale ambapo hawakuridhishwa na mchakato wa ununuzi.
“Mkakati tulio nao katika mwaka huu wa fedha 2024/25 ni kuhakikisha kuwa tuwafikia wazabuni katika kanda nne ambazo hatujazifikia, katika kufika kwetu katika kanda hizo kanda tutakuwa tumewafikia wazabuni wengi,” amesema Bw. Sando
Bw. Sando ametaja kanda hizo kuwa ni kanda ya kati, kanda ya kaskazini, kanda ya nyanda za juu kusini na kanda ya kusini.
Wakati huohuo, Naibu Katibu Mtendaji wa PPAA, Bi. Florida Mapunda amezitaja faida za kuanzishwa kwa moduli ya kuwasilisha rufaa/malalamiko kwa njia ya kieletroniki na kueleza kuwa imesaidia kupunguza gharama na muda.
“Moduli hii itasaidia kupunguza gharama na muda kwa kuwa utaratibu wa zamani ulikuwa unamlazimu mzabuni kuwasilisha malalamiko yake katika ofisi za Mamlaka ya Rufani,” amesema Bi. Florida na kuongeza kuwa moduli hiyo itaboresha na kuimarisha uwazi.
Amesema Moduli hii itamwezesha mzabuni au mfanyabiasha kuona hatua kwa hatua jinsi rufaa yake inavyoshughulikiwa hadi utoaji wa hukumu na kuongeza kuwa italeta uwazi na uwajibikaji na hivyo kuwapa imani wazabuni ya kuamini katika mifumo ya utoaji haki kwenye michakato ya zabuni za umma.
Kongamano la Wadau wa Ununuzi wa Umma limewakutanisha wadau wa ununuzi wa ndani ya Tanzania na Nje zaidi ya 1,500. Kauli mbiu ya kongamano hilo ni: “Matumizi ya Dijitali kwa Ununuzi wa Umma Endelevu.
Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), Bw. James Sando akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) pembezoni mwa Kongamano la 16 la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki Jijini Arusha
Naibu Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), Bi. Florida Mapundaa akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) pembezoni mwa Kongamano la 16 la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki Jijini Arusha
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...