Na Mwandishi Wetu, Zanzibar


MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ilianzisha Mpango wa Kunusuru kaya Maskini (PSSN) mwaka 2012 ili kupunguza umaskini uliokithiri katika kaya.

Amesema mpango huo unatekelezwa ndani ya Awamu ya Tatu ya TASAF, ambao una malengo ya kuziwezesha kaya zinazoishi kwenye umaskini uliokithiri kuongeza kipato, fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu na kuondoa muendelezo wa umaskini katika vizazi vijavyo kwa kuwekeza katika elimu na afya kwa watoto katika kaya za walengwa.

Abdulla ameyaeleza hayo jijini Zanzibar alipokuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa tathimini ya mwisho ya kupima matokeo ya kipindi Cha pili Cha Mpango wa kunusuru kaya masikini( PSSN) ya mwaka 2024

"Mpango wa Kunusuru kaya Maskini umefanyika kwa Awamu Mbili. Awamu ya Kwanza (PSSN I) ilitekelezwa kuanzia mwaka 2012 hadi Mwaka 2019, ikilenga kufikia takribani kaya Milioni 1.2 yaani asilimia 15 ya kaya zote za Tanzania kwa wakati huo, zikiwemo kaya zote zinazoishi chini ya mstari wa umaskini wa chakula na wale walio katika hatari ya kuangukia chini mstari wa umaskini wa chakula.

"Hivyo, Awamu ya Kwanza iliweza kufikia lengo lake la kuwafikia wananchi waliokusudiwa katika asilimia 70 ya shehia, vijiji na mitaa yote hapa nchini. Kwa sasa, Serikali ya Tanzania inatekeleza Awamu ya Pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (PSSN II) yenye lengo kuzifikia kaya milioni 1.4 katika shehia, vijiji na mitaa yote hapa nchini.

"Mpango wa kunusuru kaya masikini ni mojawapo ya mipango mikubwa inayotekelezwa nchini kwa kushirikisha kaya za walengwa katika kupambana na umaskini na kuimarisha uchumi wao. Ili kufanikisha malengo ya Mpango yaliyokusudiwa, Mpango unatoa ruzuku ya msingi kwa kaya za walengwa ambazo pia zinapaswa kutimiza masharti ya elimu na afya."amesema Abdulla.

Ameongeza pia kaya hizo zinanufaika kwa kushiriki katika miradi ya jamii yenye lengo la kutoa fursa za ajira za muda na kwamba katika utekelezaji wa Mpango wa Kuweka Akiba na Kuwekeza, kaya za walengwa wanapata mafunzo ya stadi za ujasiriamali na mbinu za kuunda vikundi endelevu vya kuweka akiba na kuwekeza.

Pia miradi ya kuendeleza miundombinu ya afya, elimu, barabara, kilimo, mazingira na maji inatekelezwa na walengwa kupitia Mpango huo.Kupitia Mpango huo takwimu zinaonesha kuanzia mwaka 2000 hadi Agosti, 2024, Serikali kupitia Mpango huu imesaidia kaya za walengwa wapatao 1,450,000 (sawa na wastani wa watu 6,960,000).

Amesema kati ya kaya hizo kaya 394,500 (sawa na wastani wa watu 1,893,600) tayari zimeshajikomboa kutoka kwenye umaskini uliokithiri. Kaya hizo zimehitimu na kutoka katika Mpango baada ya hali zao za maisha kuwa bora zaidi ukilinganisha na kabla ya kushiriki katika Mpango.

"Tathmini hii ina awamu mbili ambapo awamu ya awali ilifanyika mwaka 2022 na hii awamu ya mwisho inafanyika mwaka huu wa 2024.Jumla ya mikoa 17 yaani mikoa 14 Tanzania Bara na mikoa 3 Zanzibar yenye jumla ya shehia, vijiji na mitaa 434 itatembelewa kwa ajili ya Tathmini hii. Kati ya hiyo, vijiji na mitaa 376 ni kutoka Tanzania Bara na shehia 58 ni kutoka Zanzibar.

"Madhumuni ya tathmini hii ni kupima endapo Mpango huu unafikia malengo yaliyokusudiwa ya kuondoa umaskini kwa kaya zilizoainishwa kuishi katika umaskini uliokithiri. Katika nchi yetu, mpango huu unahusisha mikakati zaidi ya mmoja katika utekelezaji ili kuhakikisha kwamba walengwa wanafaidika na kutoka katika hali ya umasikini mapema zaidi.

"Hivyo basi, ni matarajio yangu tathmini hii itaweza kutoa taswira halisi ya hali ilivyo na kuiwezesha Serikali kuona ni eneo lipi tunafanya vizuri zaidi na eneo lipi linahitaji kuongeza mkazo,"amesema Abdulla.

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Salum Kassim Ali amesema kwa kawaida tathmini hiyo hufanyika kwa awamu mbili yaani tathmini ya mwanzo (Base-line) na Tathmini ya Mwisho (End-line).

Amefafanua tathimini ya mwanzo hufanyika kabla ya utekelezaji wa mpango kwa
kaya za walengwa na kaya nyingine katika maeneo ya utafiti na tathmini ya mwisho hufanyika miezi 24 baada ya utekelezaji wa Mpango katika kaya zilezile zilizotembelewa katika utafiti wa awali.


"Tathmini ya mwanzo katika kipindi cha pili cha mpango, ilifanyika Aprili - Juni 2022. Ripoti ya Tathmini hiyo ilizinduliwa rasmi Oktoba 2023.Kwa sasa maandalizi ya utekelezaji wa Tathmini ya mwisho yamekamilika baada kumaliza mafunzo ya wasimamizi na wadadisi wa utafiti, zoezi la kukusanya taarifa linatarajiwa kuanza rasmi baada ya kutuzindulia leo hiyo.

"Matokeo ya tathmini hiyo ya mwisho ndio yatakuwa msingi wa kufanya maamuzi ya kuboresha zaidi hali ya upatikanaji wa huduma za kijamii na vile vile kuweka mikakati zaidi ya kupunguza umaskini hapa nchini kwetu."

Amesema utafiti huo wa mwisho utafanyika katika mikoa 17 hapa nchini, ambapo mikoa 14 ni ya Tanzania Bara na mikoa mitatu (3) ni ya Tanzania Zanzibar na Zanzibar, utafiti huo utafanyika katika Mkoa wa Kaskazini

Unguja, Mkoa wa Mjini Magharibi na Mkoa wa Kusini Pemba.

Ameongeza kwa upande wa Tanzania Bara utafiti utafanyika katika mikoa ya
Mtwara, Lindi, Dodoma, Ruvuma, Iringa, Pwani, Singida, Morogoro, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Katavi, Rukwa na

Dar es Salaam.Jumla ya shehia, mitaa, na vijiji 434 kwa nchi nzima vimechaguliwa ambapo vijiji na mitaa 376 ni kwa Tanzania Bara na shehia 58 kwa Tanzania Zanzibar.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...