Baadhi ya majengo katika soko jipya la madini ya vito yanayoendelea kujengwa na Halmashauri ya wilaya Tunduru kwa kushirikiana na wadau wa madini wilayani humo.
Na Mwandishi Maalum,Tunduru
BAADHI ya wazee wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kufungua soko jipya la madini ya vito ili kudhibiti utoroshaji wa madini na mapato ya serikali unaotokana na uwepo wa masoko holela.
Walisema,iwapo soko hilo litafunguliwa litakuwa na mchango mkubwa kiuchumi na litaongeza mzunguko wa fedha na kuharakisha maendeleo ya wilaya ya Tunduru na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla na vijana wengi watapata ajira za muda na za kudumu.
Abdala Kawanga alieleza kuwa,soko hilo linalojengwa na Halmashauri ya wilaya kwa kushirikiana na baadhi ya wadau wa madini licha ya kutoa ajira kwa wananchi wa Tunduru,Serikali itarudisha gharama haraka zilizotumika katika ujenzi kupitia pango la ofisi na ushuru wa madini.
Hassan Kindamba alisema,kuna fedha nyingi za Serikali zimetumika katika ujenzi wa soko hilo,kwa hiyo ni vema likafunguliwa haraka ili fedha zitakazopatikana zitumike kwenye miradi mingine ya maendeleo iliyosimama kutokana na uhaba wa fedha.
Kwa mujibu wa Kindamba,wananchi wa Tunduru wana shauku kubwa kuona soko linafunguliwa kutokana na umuhimu wake kiuchumi na linatajwa kuupendesha mji wa Tunduru uliojengwa tangu mwaka 1904.
Aidha ameshauri kuwa,ujenzi wa soko jipya utakapokamilika,wanunuzi wote wa madini wahamishiwe katika soko hilo ili kudhibiti mianya ya utoroshaji wa madini na kudhibiti mapato ya Serikali yanayopotea kutokana na kuwepo kwa masoko mawili ya Tudecu na Generation na masoko mengine yasio rasmi.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas,ameipongeza Halmashauri ya wilaya Tunduru kutenga zaidi ya Sh.milioni 81 ili kujenga soko hilo ambalo litakapokamilika na kuanza kutumika litakuwa chanzo kikubwa cha mapato.
Alisema,ameunda Tume maalum ya wataalam ili kufanya utafiti wa hoja zilizotolewa na wadau wa madini ambayo tayari imemaliza kazi yake juu ya uwepo wa soko moja au masoko matatu na kilichobaki ni Serikali kutoa uamuzi nini kifanyike na mua wa kufungua soko jipya.
Hata hivyo Rc Abbas, amewaagiza wasimamia wa ujenzi wa soko hilo kuhakikisha wanaongeza kasi ya ujenzi kutokana na muda waliopewa wa mwezi mmoja ili ifiapo mwezi Septemba soko hilo liweze kufunguliwa na wadau wa madini walitumie kwenye shughuli zao.
Kwa upande wake Mhandisi wa ujenzi wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Aidan Mtega alisema,ujenzi wa soko hilo hadi sasa umefikia asilimia 95 na zimebaki kazi ndogo ndogo ambazo ni kufunga madirisha kwa baadhi ya vyumba na mfumo wa umeme.
Alisema,hadi kufika mwezi Oktoba mwaka huu kazi zote zitakamilika kwa asilimia mia moja ambapo amewakaribisha wafanyabiashara na wadau mbalimbali kwenda Tunduru kuwekeza katika sekta ya madini kwani bado kuna fursa kubwa ya kufanya biashara hiyo.
Wilaya ya Tunduru ina utajiri mkubwa wa madini ya vito na madini ya shaba yaliyogundulika kwa wingi katika kata ya Mbesa tarafa ya Nalas,na kugundulika kwa madini hayo kunaifanya wilaya hiyo kuwa wilaya pekee nchini na Afrika Mashariki na kati kuwa na madini aina nyingi.
Baadhi ya vijana waliopata kazi ya ujenzi katika soko hilo walisema,ujenzi wa mradi huo umewasaidia kupata kazi zinazowangizia vipato,hivyo kupunguza changamoto kubwa ya ajira.
Islam Ibrahim,amewapongeza viongozi wa Halmashauri ya wilaya Tunduru kuwa na wazo la kujenga soko la kisasa la madini,lakini amewaomba wafanyabiashara kulitumia soko hilo badala ya kufanya shughuli zao kwa kificho.
Yazidu Hassan,ameitaka Serikali kuongeza nguvu katika udhibiti wa madini kwani inapoteza fedha nyingi zinazotokana na kodi zinazostahili kulipwa na wanunuzi kutoka nje ya nchi wanaonunua madini kwenye nyumba wanazoishi kwa kuwatumia Watanzania wachache wasiokuwa na uchungu na nchi yao.
Hassan alieleza kuwa,soko hilo litavutia na kuhamasisha wafanyabiashara wengi kwenda Tunduru kwa ajili ya kuwekeza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuwa tayari Serikali imeanza kuifungua wilaya hiyo kwa kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.
MWISHO.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...