NA. MWANDISHI WETU

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema hali ya lishe nchini imeendelea kuimarika kwa kwa kuzingatia Takwimu zinaonesha kupungua kwa viwango vya utapiamlo kwa baadhi ya viashiria ikiwemo kiwango cha udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambacho ndio kiashiria kikuu cha utapiamlo kimepungua kutoka asilimia 32 mwaka 2018 hadi asilimia 30 mwaka 2022 (DHS 2022). 

Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe nchini unaofanyika ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Malaika Jijini Mwanza tarehe 02 Oktoba, 2024, uliowakutanisha wadau wa afua za lishe kwa lengo la kupokea na kujadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha mwaka wa tatu 2023/2024 katika maeneo mahsusi yaliyoanishwa kwenye Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe (2021/22-2025/26).

Alieleza kuwa Mkutano huo unatoa fursa kwa wadau wote wa lishe kujadili namna utekelezaji ulivyofanyika, changamoto na mikakati ya kufanikisha utekelezaji katika kipindi kilichobaki cha utekelezaji wa mpango huo hususan mwaka 2025/26. Pia Mkutano huu unatazamiwa kuongeza msukumo mpya wa utekelezaji wa afua za lishe miongoni mwa wadau kama moja ya nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Akiongelea kuhusu hali ya lishe amesema kuwa kiwango cha ukondefu pia kimepungua kutoka asilimia 3.8 mwaka 2014 hadi asilimia 3.5 mwaka 2018, ingawa takwimu hizi zilibadilika mwanzoni mwa mwaka 2023 baada ya kupata matokeo ya utafiti uliofanywa Machi - Julai 2022 na Taasisi ya Chakula na Lishe na Ofisi ya Taifa ya Takwimu. 

Dkt. Yonazi alisema kuwa, uwepo wa wadau katika mkutano huo ni uthibitisho tosha wa ushirikiano uliopo na utayari wao katika kuboresha hali ya lishe kwa Watanzania, hususan makundi yanayoathirika zaidi ambayo ni watoto wadogo na wachanga, watu wenye mahitaji maalum, wanawake wajawazito na wale walio katika umri wa uzazi. 

“Naomba ushirikiano huo uendelee wakati wote wa utekelezaji wa mpango na hususan wakati kama huu ambao tunakutana kujadili utekelezaji Sote tunajua kuwa ili tuweze kuwa na maendeleo ya kiuchumi na kijamii ni lazima Taifa liwe na watu wenye lishe na afya bora ili kuwa na uwezo wa kufikiri, kutenda na kufanya kazi kwa bidii. Hivyo, juhudi hizi na nyingine ni muhimu kuwa endelevu ili kutuwezesha kufikia malengo,” alisisitiza Dkt. Yonazi.

Aidha Dkt. Yonazi alitumia mkutuno huu kuiasa  jamii kuendelea kushiriki kikamilifu na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha hali ya lishe kwa Watanzania inaendelea kuimarika huku akisema kuwa Serikali inaahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zilizopo na nyingine za wadau ili kuhakikisha Taifa linapata mafanikio dhidi ya mapambano ya tatizo la utapiamlo. 

Kwa upande wake Mheshimiwa Mizengo Pinda Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema, Serikali imeendelea kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha jamii inaendelea na mapambano haya ya lishe duni na kuhakikisha Taifa linaendelea kuwa na watu wenye afya bora, na kukumbusha jamiii kuwa mstari wa mbele katika masuala ya afua za Lishe.

“Jambo hili la mapambano dhidi ya lishe ni Mtambuka, hakuna Wizara itakwepa, hivyo ni wakati sahihi na tuone njia sahihi za kutumia katika mapambano haya,ifike mahali tuizungumze dhana ya lishe katika wizara na kuhimiza agenda hii iwe ya kila mmoja,” alisema Mhe. Pinda

Aliongezea kuwa, masuala ya lishe yawekewe mkazo zaidi kuanzia katika elimu ya  msingi hasa kupitia uwepo wa Klabu maalum zinazochagiza masuala ya afua za lishe nchini lengo ni kuwajengea uelewa watoto kuwa na elimu ya kina kuhusu masuala haya.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka alizungumza wakati wa mkutano huo alieleza jitihada zinazofanywa na mkoa wake katika mapambano dhidi ya Utapiamlo na masuala yote ya lishe amesema ni wakati sahihi kuwa na mikakati inayotekelezeka ili kuwa na jamii yenye lishe na afya bora.

Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe nchini umeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, na umebebwa na kauli mbiu isemayo “Kuchagiza Mchango wa Wadau wa Kisekta ili Kudumisha Matokeo Bora ya Hali ya Lishe Nchini Tanzania” ukilenga kufanya tathmini ya  utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa pili wa Taifa wa Lishe ili kuendelea kukabiliana na changamoto za utapiamlo nchini.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akihutubia wakati wa Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe nchini uliofanyika ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Malaika Jijini Mwanza tarehe 02  Oktoba, 2024.
Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda akizungumza jambo na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (wa pili kutoka kulia) mara baada ya kuwasili kwa katika viwanja vya hoteli ya Malaika Jijini Mwanza kwa lengo la kushiriki Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe wakifuatilia mada wakati wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Malaika Jijini Mwanza.
Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Taznania Mhe. Mizengo Pinda akizungumza kuhusu masuala ya afua za lishe wakati wa Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe uliofanyika Jijini Mwanza. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt.Germana Leyna
Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt.Germana Leyna akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe uliofanyika Jijini Mwanza tarehe 02 Oktoba, 2024.
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda (kushoto) pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (katikati) wakipata maelezo kuhusu tiba lishe(mchanganyiko wenye virutubisho mbalimbali) wakati wa maonesho katika Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe uliofanyika Jijini Mwanza.Anayetoa maelezo ni Bw. Selemani Hamisi wa kampuni ya Enjoy your life.
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo akipata maelezo ya virutubisho mbalimbali kutoka kwa Bi. JaneRose Mtayoba wa Kampuni ya JEM Product wakati wa maonesho katika Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe uliofanyika Jijini Mwanza.
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda (katikati waliokaa) pamoja na meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe uliofanyika Jijini Mwanza.
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda (katikati waliokaa) pamoja na meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau walioshiriki wakati wa Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe uliofanyika Jijini Mwanza.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (katikati) pamoaj na meza kuu wakifuatilia mada wakati wa Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe nchini uliofanyika ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Malaika Jijini Mwanza, kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt.Germana Leyna

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU) 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...