Na. Dennis Gondwe, DODOMA


MKOA wa Dodoma unatamani kuona zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa linafanikiwa kwa asilimia mia moja kwa kuhakikisha kila mwananchi anashiriki kikamilifu katika uchaguzi huo.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri wakati akifungua Bonanza kubwa la kihistoria la kuhamasisha umma kushiriki mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa lililofanyika katika uwanja wa Shule ya Sekondari Dodoma.

Alhaj Shekimweri alisema “Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma anatufundisha kujitambua na kujithamini kupitia kaulimbiu yake isemayo ‘Dodoma Fahari ya Watanzania’. Pia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatekeleza miradi mkubwa katika Dodoma ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa kimataifa Msalato. Ujenzi wa Barabara ya Mzunguko na ujenzi wa Treni ya Kisasa ya Mwendo kasi SGR ambayo stesheni ya Dodoma ndiyo kubwa ikiwa na uwezo wa kupokea watu 2,500 kwa mara moja”.

“Kwa uzito huo ni lazima muamko wetu wakazi wa Dodoma kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uwe mkubwa sana. Tumuunge mkono mkuu wetu wa mkoa kwa kuhakikisha habaki hata mtu mmoja bila kuandikishwa ili malengo yetu tusishuke chini ya asilimia 100”.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi kufungua bonanza hilo, Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alisema kuwa maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa yamekamilika. Vifaa vyote vinavyohitajika vimefika na upande wa rasilimali fedha, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha kwa asilimia 100, aliongeza.

Bonanza la kuhamasisha umma kushiriki mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 lilitanguliwa na ‘jogging’ iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma pamoja na watumishi wa umma kwa kupita katikati ya Jiji la Dodoma kuelekea Shule ya Sekondari Dodoma chini ya kaulimbiu isemayo “Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi”.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...