Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Joel Lawrent akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhumisho ya Siku Mbolea Duniani yatayofanyika mwaka huu jijini Dodoma.
Na Chalila Kibuda,Michuzi TV
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imesema maadhimisho ya siku ya mbolea duniani kwa mwaka 2024 yatafanyika kwa namna ya tofauti ikilinganishwa na miaka iliyopita ambapo kwa mwaka huu mamlaka imeandaa kongamano la aina yake la Kimataifa la kwanza la mbolea litakalofanyika Oktoba 11 na 12 jijini Dodoma.
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 1, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Joel Lawrent wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani ambayo kilele chake kitakuwa Oktoba 13 mwaka huu ambapo Mgeni Rasmi anatarajia kuwa Waziri wa Kilimo Hussein Bashe.
Kwamba Kongamano hilo litakalofanyika katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma litawakutanisha pamoja wadau wa tasnia ya mbolea kitaifa na kimataifa na linatarajiwa kuja na majibu ya changamoto zinazoikabili tasnia ya mbolea na wakulima kwa ujumla.
"Mgeni rasmi wa kongamano hili atakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Ndugu Gerald Mweli na Kongamano hili litahudhuriwa na washiriki 250 kutoka ndani na nje ya nchi watakaojadili mada mbalimbali kuhusu tasnia ya mbolea kwa ujumla wake," amesema Lawrent na kuongeza,
"Hii itatoa fursa kwa wadau hao kujadili kwa pamoja mabadiliko chanya ya tasnia ya mbolea, kubadilishana uzoefu na kujadili namna bora ya kutatua changamoto zinazoikabili tasnia hiyo,".
Kwamba mada zitakazojadiliwa na pamoja na usimamizi na udhibiti wa mbolea, tathmini ya mifumo na udhibiti bora wa mbolea, mchango wa afya ya udongo katika kuimarisha usalama wa chakula nchini na matumizi ya tehama katika kusimamia tasnia ya mbolea.
Mada nyingine ni nafasi ya wanawake na vijana katika kukuza tasnia ya mbolea, kuhamasisha uzalishaji wa ndani, matumizi sahihi ya mbolea na biashara ya mbolea katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Hata hivyo amesema kuwa jioni ya Oktoba 11, 2024 Waziri wa Kilimo Hussein Bashe atazindua Mkakati wa Maendeleo ya Tasnia ya Mbolea nchini Tanzania.
Amebainisha kuwa wakati kongamano likiendelea jijini Dodoma ni kwamba mkoani Manyara maadhimisho hayo yataendelea kuanzia Oktoba 10, 11 na 12 na yatazinduliwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga ambapo yatahusisha maonesho kutoka kwa wadau mbalimbali wa Sekta ya Kilimo, hususan kwenye mnyororo wa thamani wa mbolea.
Amebainisha, maonesho yatafanyika katika viwanja vya Stendi ya Zamani iliyopo Babati Mjini, mkoani Manyara na yatahusisha wazalishaji na waingizaji wa mbolea, wasambazaji wa mbolea, kampuni za mbegu, kampuni za viuatilifu, mashirika ya umma na binafsi, taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo pamoja na taasisi za fedha ambapo siku ya nne itakuwa ni kilele cha cha maadhimisho hayo.
Kwamba hadi kufikia leo waoneshaji 45 wameshathibitisha kushiriki ambapo wataonesha bidhaa mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa mbolea na kilimo kwa ujumla.
Ameongeza kuwa lengo la maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani ni kupanua wigo wa kuelezea masuala mbalimbali katika tasnia hiyo ikiwemo mafanikio yake nchini, kutoa elimu kwa wadau, hususan wakulima na wafanyabiashara na kwamba kwa mwaka huu kauli mbiu ya Siku ya Mbolea Duniani ni "Tuongee Mbolea, Kilimo ni Mbolea".
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku Kitaifa Louis Kasera amesema kwa mwaka huu mpango ni kuingiza tani milioni moja ya mbolea ambapo amebainisha kuwa lengo la Serikali la kuongeza tija na matumizi ya mbolea limefanikiwa kwani wakulima milioni 1.5 wameongezeka katika matumizi ya mbolea.
Hata hivyo amewaomba wakulima kuendelea kujiandikisha na kuhuisha taarifa zao na kununua mbolea.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...