Na Said Mwishehe, Michuzi TV

NAJARIBU kutafakari kuhusu mwenendo wa siasa zetu nchini Tanzania na hasa siasa za vyama vya upinzani.Ndio natafakari sana na ninazo sababu, ziwe za msingi au za kijinga lakini zote sababu tu,kwani shida iko wapi.

Katika maisha kila mwanadamu amepewa uwezo wake wa kujadili na kuchambua mambo. Ndio ukweli ulivyo na hakuna anayeweza kupinga, toa hoja yako itasikilizwa na bahati nzuri hakuna aliyelishwa kiapo,ukizikubali poa,ukikataa shega.Ngoja nijadili kuhusu siasa za upinzani kwa jinsi ninavyoziona.

Tena nataka kuizungumzia CHADEMA ndio Chama kikuu cha upinzani kwa mtazamo wa wengi,hata mimi naamini hivyo hivyo tu,nani ambaye hajui ukubwa wa CHADEMA hapa nataka nitoe angalizo na huu ni mtazamo wangu Kuna CHADEMA ilee halafu kuna hii ya sasa.

Unaweza kujiuliza CHADEMA ile ni ipi halafu CHADEMA hii ni ipi? Jibu fupi kuna Ile CHADEMA ya Katibu Mkuu akiwa Dk.Wilbroad Slaa halafu kuna hii ya Katibu Mkuu John Mnyika. Ni CHADEMA mbili tofauti lakini kwa mujibu wa Msajili wa Vyama vya Siasa CHADEMA ni moja na hilo ndilo la kubakia nalo.

Nimeamka kuzitofautisha kwa lengo la kujenga hoja, binafsi ukiniambia CHADEMA ipi ilikuwa mpinzani wa kweli na anayejali maslahi mapana ya Taifa la Tanzania, basi nitakwambia ni CHADEMA ile ya Katibu Mkuu Dk.Slaa halafu pale juu akiwa Freeman Mbowe ambaye ndio Mwenyekiti wake.

Ilikuwa CHADEMA ya amsha amsha sana, ilikuwa CHADEMA kweli kweli yenye kusema na kutenda.Ilikuwa moto wa kuotea mbali. Wana CCM wananielewa vizuri lakini hata Watanzania wanajua nazungumza nini.Asiyenielewa hiyo sio shida yangu.

CHADEMA ya Katibu Mkuu akiwa Dk.Slaa ilikuwa inajua nini inafanya,ilikuwa na dhamira ya kweli ya kuchukua Nchi kwa maana ya kushika dola. Ilipendwa kila mahali,vijana wa Kitanzania wakaona hicho ndio Chama chao.

Kijana akisema yeye ni CHADEMA anazungumza kwa kujiamini. Ilikuwa hatari faya.Wanafunzi wa Elimu ya juu walikimbilia huko wa kutafuta mabadiliko.

Kila kona habari ilikuwa ni CHADEMA tu, vijana waliosoma na wasiosoma ilikuwa huwaambii kitu kuhusu CHADEMA. Ilikuwa CHADEMA na wao wao na CHADEMA.Ujue wanaoifahamu CHADEMA ile wanajua ninachozungumza.

CHADEMA ya wakati ule hata Mwenyekiti wake Freeman Mbowe alikuwa Mbowe haswa.Ngoja ni kwambie kitu hata huyu Mbowe wa sasa ni tofauti na Mbowe wa zamani.Hakika nyakati zinakwendakwa kwa kasi sana.

Kabla ya kuendelea zaidi tufanye hivi; meza mate kwanza halafu angalia mbele kidogo na kama ukiweza kujinyoosha sawa tu.Sasa endelea kunisoma tena kwa umakini utanielewa kama sio sasa basi mwishoni.Nawaza kwa mtazamo wangu wa kijinga kwa jinsi ninavyoitazama CHADEMA ya sasa.

Sasa tuendelee na nasema hivi CHADEMA ile ya Katibu Mkuu akiwa Dk.Slaa na Makamu Mwenyekiti akiwa Said Arfi huku Naibu Katibu Mkuu Bara akiwa Zitto Kabwe ilikuwa CHADEMA ya moto kweli.Mwenyekiti ni Mbowe huyu huyu lakini alikuwa ni mwenye mawazo mapya na yenye tija kwa Taifa.

Safu ya CHADEMA katika uongozi ilikuwa imesheheni wanasiasa wenye uwezo mkubwa, wenye ushawishi na zaidi walikuwa na uwezo mkubwa wa kujenga hoja. Ukienda kwenye wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama kulikuwa na watu makini sana, halafu Mungu aliwapa akili na maarifa.

Walikuwa wanajua kujipanga halafu wako smati sana katika kufanya siasa za upinzani. Wakiitisha maandamano ujue maandamano kweli.Nchi ilikuwa inasimama.Wakitangaza maandamano shughuli zinasimama, sio siku hivi hata Wakiitisha maandamano wanajikuta wako viongozi tena familia zao.

Watu hawana Mpango nao, wanaona kama vile hawana jipya ukijumlisha na hali ya kiuchumi kila mtu yuko bize na mishe zake za kusaka fuba a.k.a fedha. Bungeni nako kuliwaka moto,kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni alikuwa Mbowe, lakini ni Mbowe yule wa zamani...wacha kabisa.

Hoja ya mkataba wa Buzwagi najua wengi wanaikumbuka.Ni hoja iliyosababisha Zitto Kabwe asimamishwe Bungeni. CHADEMA walisimama kidete na kujenga hoja,asikwambie mtu Bungeni palikuwa pachungu kwa Serikali.

CHADEMA kwa uwezo wa viongozi wake na wakati huo na Bungeni hasa Bunge la mwaka 2005 walikuwa 11 tu lakini moto wake uliwafanya Wabunge wa CCM kuwa wapole.CHADEMA ilijua kusimamia maslahi ya Taifa,walipokuja na hoja za ufisadi au rushwa walisimama imara kujenga hoja.

Najua pia tunakumbuka CHADEMA ile ilivyopambana na sakata la ESCROW. Walifanya mengi sana na bahati nzuri walikuwa na mtaji wa watu.

Acha nirudi katika hoja yangu, Ni hoja ya kuzungumza kwa ujumla kuhusu CHADEMA bila kujali CHADEMA ile au Chadema hii ya sasa.Kwa kifupi na huu ndio mtazamo wangu hata kama ni wa kijinga nasema hivi CHADEMA imefika mwisho ni kama imegota katika kila kitu.

Imegota katika kuwaza,imegota katika kufikiria na imegota katika kupanga mambo.Huenda naiangalia CHADEMA kwa mtazamo hasi lakini ukweli unabakia chama hicho kimepoteza ile nguvu yake. CHADEMA kwa sasa inawakatisha tamaa hata wanachama wake.

Wanaogopa hata kujitambulisha huko mtaani.Wajitambulishe mtaani kwa lipi kubwa walilofanya? Tatizo letu ukiamua kuzungumza ukweli uonenakana mbaya, unaonekana umetumwa, utaambiwa umelipwa.Acha niseme kwanza sina aliyenituma wala aliyenilipa.Nimeiangalia CHADEMA naiona sio ile.Acha niwachane tu,potelea mbali.

Narudia tena ni hivi naizungumzia CHADEMA hii ya sasa ambayo hata kauli za viongozi wake zimekuwa zikitofautiana, wanapambana wao kwa wao.Ukimsikia Makamu Mwenyekiti wake Tundu Lissu utaona kuna kupishana kukubwa na viongozi wengine wa Chama hicho akiwemo Mwenyekiti wao Freeman Mbowe.

Zamani CHADEMA walikuwa wanaitisha mkutano wa vyombo vya habari kujibu hoja za CCM lakini sasa si ajabu siku hizi kuita vyombo vya habari kujibu hoja za wao kwa wao .Nikisema CHADEMA

imefika mwisho unielewe.

Kwa mfano halisi kabisa ukitaka kujua CHADEMA imefika mwisho angalia viongozi wake wanavyolumbana katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.Lissu amekuja na hoja kuwa ndani ya Chama chake kuna fedha chafu lakini na rushwa zimekithiri katika chaguzi ndani ya Chama.

Ni maneno ya Lissu hayo sio mimi.Msije mkataka niwape ushahidi .Acha nimwagike tu halafu ni mawazo yangu,sio yako.Ila ukweli Chadema ile ya Pipooooozi halafu Wana huku kitaaani wanaitikia pawaaaaaaaaa haipo tena.

Ukweli CHADEMA ile ya zamani ilikuwa tamu sana.Sio hii ya sasa ambayo mtaani hakuna anayeizungumzia kabisa na kibaya zaidi hakuna cha PIPO wala PAWA .

Tuwe wakweli CHADEMA hata kujenga hoja sasa imekuwa changamoto, wamebakia tu na ajenda ya Katiba mpya .Hoja ya rushwa imepitwa na wakati.Kibaya zaidi na wao wenyewe wanatuhumiana kwa Arusha Wana CHADEMA wamezichapa ukumbini .Wamefikia hapo eti.

Leo hii hii ukiwauliza CHADEMA wana mipango gani kwa Watanzania hawatakuwa na majibu.Yaani wamefikia hapo. Wakijitahidi sana wanakwenda na hoja za matukio.Ishu ya kutekwa ndio angalau wanashikilia hapo lakini utekaji unapigwa vita na kila Mtanzania.Unapigwa vita na kila mtu, hata mimi nachukia matukio ya utekaji.

Viongozi wa CHADEMA wengi wao wamepoteza muelekeo kabisa,hata wenyewe hawajui wanataka nini.Mbowe amekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho kwa zaidi ya miaka 20, unategemea mawazo mapya hapo?Hakuna jipya.

Namheshimu kaka Freeman Mbowe lakini kwa maoni yangu naye amefika mwisho .Najua CHADEMA ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo nadhani angeonesha demokrasia kwa kukaa kando na nafasi yake ipate mtu mwingine huenda akaja na mawazo mapya ya kufufua Chama hicho.

Kukosekana kwa mawazo mapya ya Mwenyekiti na viongozi wengine kumekifanya Chama kubaki njiapanda. Naandika huku naikumbuka ile CHADEMA ya Operesheni Sangara maana ilikuwa inajua ilikotoka ,iliko na inakokwenda lakini CHADEMA ya sasa imepwaya hata ukiangalia sura za viongozi wa juu na wanaongoza Kamati Kuu.

Ngoja nikukumbushe tu ile Kamati kuu ya 2010-2015 ilivyokuwa na Mbowe, Said Arfi, Dk.Lwaitama, Prof Baregu, Mdee, Zitto, Profesa Kitila, Dk Slaa. Hii Chadema ya sasa ambayo imepoteza muelekeo unakutana na Tundu Lissu ambaye hata busara ni kama zimeanza kupungua, Salum Mwalimu anaendelea kukomaa,John Mrema najua uwezo lakini naye ndio hivyo tena.Mnyika huyu sio yule wa kipindi kile.Kuna Munisi, Kigaila, Sugu.

Hebu angalia mwaka 2015-2020 sekretarieti na Kamati ilikuwa ina Lowassa, Kingunge, Sumaye, Mashinji, mzee Mutembei, Mzee Kimesera.Ilikuwa na watu wenye mawazo yenye kujenga zaidi na ndio maana ilikubalika na kupendwa.

Ukitaka kujua CHADEMA hii imepoteza mvuto msikilize Mchungaji Peter Msigwa aliyekuwa Mbunge wa Iringa Mjini.Baada ya kuona Chama kimepoteza muelekeo ameamua kujiunga na CCM, anawapiga ndugu zake hatari.

Kimsingi CHADEMA ya sasa si tu imekosa mvuto na imefika mwisho bali haina watu imara wanaoweza kumkabili Mbowe asifanye mambo ambayo wanaona yanakidhoofisha Chama.

Chini ya Mbowe huyu wa sasa CHADEMA imepoteza watu mahiri waliyoifanya Chama kiwe bora zaidi. Imewapoteza Zitto, Kitila, Mgamba, Sumaye,, Silinde, Waitara, Mdee, Mwambe, Msigwa, Nyalandu na wengineo.

Katika mazingira haya ya sasa ambayo haina watu mahiri na makini itawezaje kutoboa mbele ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ndio Rais wetu halafu pembeni yake yuko Katibu Mkuu Dk.Emmanuel Nchimbi?

Hata hivyo niwashauri CHADEMA hatma ya Chama chenu iko katika mikono yenu, mnayo nafasi ya kubadilika na kurejea katika makali yenu lakini kwa ukweli sio kwa viongozi waliopo sasa.Wengi wao ni kama na wenyewe wamekata tamaa.Poleni aisee.

Naomba nihitimishe hivi hayo ni mawazo yangu, ni mtazamo wangu kuhusu CHADEMA hii ambayo kila mmoja akiamua kuielezea atakuwa na namna ya kuielezea.Halafu basi nikukumbushe tu kutekana sio poa, maana isije tena ikawa ndio hivyo tena.




Povu ruksa

0713833822.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...