MTENDAJI Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, Novemba 29, 2024 ameongoza timu ya TANROADS kupokea Tuzo ya Uwasilishaji Bora wa Taarifa za Kifedha kwa kufuata Viwango vya Kimataifa vya uhasibu katika Sekta ya Umma (IPSAS) iliyotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).

Tuzo hiyo ni ushahidi wa utendaji bora wa taasisi hiyo katika utayarishaji wa taarifa za fedha kwa kufuata viwango vya kitaifa na kimataifa.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Mhandisi Besta amesema "Ni furaha kubwa kwangu na timu yangu kupata tuzo hii. Hii inadhihirisha kwamba TANROADS inafuata vigezo vyote muhimu vya utayarishaji wa taarifa za kifedha zinazokidhi viwango vya ndani na vya kimataifa."

TANROADS imeshika nafasi ya pili katika kundi la mawakala wa Serikali, hatua ambayo Mhandisi Besta ameeleza kuwa ni mwanzo mzuri.

Ameongeza kwa kusema kuwa, taasisi hiyo imejipanga kupanda hadi nafasi ya kwanza mwaka 2024 kwa kuimarisha zaidi utayarishaji wa taarifa za kifedha na kuwapatia mafunzo wahasibu wake.

Vilevile amewapongeza watumishi wa TANROADS kwa kazi kubwa waliyoifanya kuhakikisha taarifa zao zinakaguliwa na kupitishwa na wakaguzi wa nje kwa viwango bora.

"Tumejipanga vizuri na tutaendelea kufanya kazi kama timu. Ushirikiano huu ndiyo nguzo kuu ya mafanikio yetu," alisema Mhandisi Besta.

TANROADS, ambayo inasimamia miradi mikubwa ya miundombinu nchini, inatambua umuhimu wa uwazi na uwajibikaji katika utunzaji wa fedha za umma hivyo ushindi huo ni ishara ya kuaminika kwa taasisi hiyo na heshima kwa taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mhasibu Mkuu wa TANROADS, CPA Henry Mwakibete, amesema, TANROADS imeshika nafasi ya pili kati ya taasisi saba zilizoshiriki kwenye kundi la Wakala za Serikali (Government Agency Categories) .

CPA Mwakibete amebainisha kuwa, hii ni mara ya kwanza kwa TANROADS kushiriki mashindano hayo, jambo linaloongeza uzito wa ushindi huo.

"Sababu kubwa ya sisi kushika nafasi ya pili ni uwajibikaji na kujitoa kwa timu yetu pamoja na Menejimenti ya TANROADS. Tumekuwa tukitoa mafunzo kwa Wahasibu wetu na kufuata miongozo ya viwango vya kimataifa," alisema CPA Mwakibete.

Ameendelea kwa kusema kuwa, miaka 10 iliyopita, idara ya uhasibu ya TANROADS ilikuwa na Wahasibu sita wenye CPA, lakini sasa idara hiyo ina zaidi ya Wahasibu 30 waliothibitishwa ambapo pia huwa wanashiriki mafunzo ya mara kwa mara kuhusu uandaaji wa taarifa za za fedha kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Kwa upande wake, CPA Gift Gacharo ambaye ni mhasibu wa TANROADS Mkoa wa Kagera, amesema Mkoa wa Kagera umechangia mafanikio ya taasisi hiyo kwa kuandaa taarifa bora za kifedha ambazo hujumuishwa katika ripoti ya jumla ya TANROADS.

"Tumekuwa wa pili katika taasisi za umma zinazotumia IPSA. Tutaendelea kufanya kazi kama timu na tunaamini kuwa mwakani tutakuwa wa kwanza," alisema CPA Gacharo.

Katika hafla hiyo, mgeni rasmi alikuwa ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba aliyewakilishwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali CPA Benjamin Mashauri.

Kwa mwaka 2023, taasisi 86 zilikaguliwa na kushiriki katika tuzo za uandaaji wa hesabu bora. Tuzo hizi hutolewa kwa taasisi zinazokidhi vigezo vya kitaifa na kimataifa katika uandaaji wa taarifa za fedha na kihasibu.

Masharti muhimu ya kushinda tuzo hizi ni pamoja na taasisi kuwa imesajiliwa na NBAA, hesabu zake kuwa zimekaguliwa na kupewa hati safi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Zaidi ya hayo, taasisi hizo zinatathminiwa kwa kufuata viwango vya utayarishaji wa hesabu, sheria za utawala bora, na miongozo ya ukaguzi na uandaaji wa hesabu kama ilivyotolewa na NBAA.

Kufuata na kukidhi vigezo vyote hivyo ni hatua muhimu inayothibitisha uwazi, uaminifu, na ubora wa taarifa za fedha na kihasibu za taasisi husika.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...