Na Seif Mangwangi, Arusha

VIGOGO wakuu wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini wamekutana Jijini Arusha lengo mojawapo likiwa ni kuweka mikakati ya kukabiliana na wanasiasa watakaotoa rushwa katika uchaguzi Mkuu mwakani 2025.

Akifungua mkutano huo mkuu wa mwaka wa Takukuru, Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango amesema rushwa ni adui mkubwa ambaye bila kudhibitiwa wananchi wataendelea kukosa haki.

Aidha amesema pamoja na Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), kufanikiwa kuokoa bilioni 172.3 za Serikali kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo mwaka 2022/2023, sekta ya Ardhi na jeshi la Polisi zimeendelea kulalamikiwa kujaa matendo ya rushwa  nchini.

Makamu wa Rais amesema  wananchi wameendelea kuwa na malalamiko mengi juu ya rushwa na kunyimwa haki na kuzitaja taasisi zingine zinazolalamikiwa ni pamoja na mahakama za mwanzo na wilaya na kutoa wito kwa taasisi hiyo kubuni mbinu ya kuweza kukabiliana na rushwa za mahakamani.

“Mwaka 2023, REPOA ilitoa taarifa inayoonesha kuanza kupungua kwa vitendo vya rushwa katika mahakama za juu. Hata hivyo, Taarifa ilionesha kuwa bado kuna vitendo vya rushwa katika Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo ambako ndiko wananchi wengi wanakotafuta haki zao,”amesema na kuendelea:

“ Nashauri Mkutano huu usaidie kubuni mbinu na mikakati ya kukabiliana na rushwa katika mahakama za chini, mabaraza ya ardhi, na vyombo vingine vya haki jinai ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao,”amesema.

Aidha amesema vitendo vya rushwa vimekithiri katika taasisi za Serikali hasa zinazotoa zabuni mbalimbali ambapo utoaji wa zabuni hizo umekuwa ukikiukwa kwa makusudi ili kuhalalisha rushwa kwa watoa zabuni.

“ Taarifa ya ukaguzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa taasisi 44 za umma zilizokaguliwa mwaka 2022/23, inaonesha zabuni 15 zenye thamani ya Tshs 67.27 bilioni zilitolewa kwa kutumia maelezo ya zabuni (tender specifications) yenye kubagua baadhi ya wazabuni,”amesema Dkt Mpango.

Amesema taaria hiyo pia inaonyesha kuwa 2022/2023 wazabuni waliochaguliwa (shortlisted) na kupewa mikataba 25 yenye thamani ya billioni 56.70 pasipo kuidhinishwa na Bodi ya Zabuni jambo ambalo ni kinyume na taratibu za PPRA na hiyo ni rushwa.

Dkt Mpango amesema majadiliano ya mikataba 23 ya taasisi 7 yenye thamani ya billioni 64.51 yalifanyika bila kuwepo kwa mpango wa majadiliano, mikataba 60 yenye thamani ya billioni 54.07 ilisainiwa pasipo kuidhinishwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali; na, mikataba 10 ya manunuzi kwenye taasisi 5 yenye thamani ya billioni 7.48 iliongezwa muda bila kufuata utaratibu.

“ Ni wazi kuwa dosari hizi katika taratibu za manunuzi zinaashiria uwepo wa rushwa. Hivyo, ni vema TAKUKURU ifanyie kazi taarifa hizi na kuchukua hatua stahiki,”amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Francis Chalamila amesema taasisi yake imejipanga kuongeza jitihada kwenye mapambano ya rushwa nchini na kuhakikisha watu wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo watafikishwa mahakamani.

Amesema kuelekea uchaguzi Mkuu mwakani 2025 TAKUKURU imejipanga kukabiliana na vitendo vyovyote vya rushwa na kwamba watatumia mkutano huo kuweka mikakati ya kukabiliana na wote watakaohusika na utoaji wa rushwa ili waweze kuchaguliwa.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...