Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani linamshilia mtuhumiwa mmoja aliyetengeneza na kusambaza picha chafu za utupu, akiziunganisha na picha mbalimbali za Shule ya Baobab iliyopo mkoani Pwani. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishina Msaidizi wa Polisi Salim Morcase, alizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kusema kwamba mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na kifaa cha kielektroniki alichokuwa akikitumia kusambaza picha hizo chafu katika mitandao ya kijamii.

"Januari 3,2025 tulipokea taarifa kutoka kwa uongozi wa shule ya baobab iliyopo Bagamoyo, ya kutengenezwa na kisambazwa katika mitandao ya kijamii picha mjongeo za utupu zenye maudhui machafu kimaadili lakini pia ni kinyume cha sheria za nchi""

"Picha hizo chafu na zisizo za kimaadili waliotengeneza waliunganisha na baadhi ya majengo ya shule ya baobab ili kuaminisha umma kuwa vitendo hivyo vinafanyika shuleni hapo"alifafanua Morcase.

Morcase alitoa onyo kwa watu wenye tabia kama hizo za kutengeneza na kusambaza picha kama hizo kwa malengo ya kuchafua wengine au Taasisi.

Anaeleza, mkono wa sheria lazima utawafikia na hata kama haitawafikia mapema wataendelea kupata shida ya kujificha na kuacha kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo.

Nae Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari Baobab, Shani Swai, alilishukuru Jeshi la Polisi kwa ufanisi wao katika kufuatilia tukio hilo na kubaini kuwa wanafunzi wa shule hiyo hawakuwa na uhusiano nalo, bali walikuwa wahanga wa kuchafuliwa.

"Kwa hakika kulikuwa na taharuki kwa wazazi na wafanyakazi wa shule, lakini tunashukuru kuwa kipindi hicho cha mpito kimepita," alisema Shani.

Aliongeza kuwa, anawaomba wazazi na jamii kuendelea kuiamini shule hiyo, kwani inatoa malezi bora na maadili kwa wanafunzi, hivyo kuwataka waendelee kupeleka watoto wao shuleni.

Shani alikemea vikali tabia ya kutengeneza matukio ya udhalilishaji kwa lengo la kuchafua watu au taasisi, akisema kuwa hiyo ni tabia potofu, na kwamba riziki hutolewa na Mungu.

Kwa upande wake, Mhandisi Fredy Joshua Ntevi, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Baobab (Taaluma), alieleza kuwa shule hiyo ina mfumo maalum kwa wanafunzi wa kike, ambapo wanaruhusiwa kubadili nywele tu kwa mtindo wa "twende kilioni".

Ntevi pia alifafanua kuwa, katika shule hiyo, wanafunzi hawaruhusiwi kumiliki simu za mkononi.

Alphonce Kamisa, Makamu Mkuu wa Shule (Taaluma), alieleza kuwa shule hiyo ilianzishwa miaka 20 iliyopita na sasa ina jumla ya wanafunzi 1,700, ambapo 730 ni wavulana. Hadi Januari 19, 2025, wanafunzi 1,600 wamesharipoti.

Tukio la kudhalilisha Shule ya Sekondari Baobab lilitokea Desemba 31, 2024

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...