Na Mwandishi Wetu
Benki ya Stanbic Tanzania (SBT) na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) zimeungana kwa pamoja kuiwezesha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupata mikopo ya kibenki, ili kusaidia kufadhili miradi ya maendeleo endelevu visiwani humo. Kupitia makubaliano haya, benki hizi zitatoa Shilingi Bilioni 185 katika awamu ya kwanza ya mkopo huu kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Benki hizo jana zilitia saini mkataba wa ushrikiano na mkopo huo mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dkt. Saada Mkuya, ambaye alisema kuwa ufadhili huo utasaidia kuimarisha uchumi wa Visiwa vya Zanzibar na kuchochea maendeleo yake kwa ujumla.
“Utiaji wa saini wa mkopo huu umekuja wakati muafaka, kwani utatusaidia kuharakisha ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 7.3 ya sasa hadi zaidi ya asilimia 7.4. Pia utatoa fedha zinazohitajika kwa ajili ya uwekezaji katika miundombinu ya kiuchumi, kuboresha sekta muhimu kama utalii, ambayo iliathirika sana na misukosuko ya janga la COVID-19,” alisema Dkt Mkuya.
Vilevile, kiongozi huyo alieleza kuwa uchumi wa Zanzibar ulishuka hadi asilimia 1.2 mwaka 2022 kutokana na athari za COVID-19, lakini sasa unazidi kuimarika na utaendelea kuboreka zaidi endapo mikopo ya aina ya Stanbic na PBZ itapatikana.
Kutokana na kuzidi kuimarika na kuboreka kwa uchumi huo, Dkt. Mkuya amesema kuwa sasa hivi kuna ongezeko la hamasa kutoka kwa benki za biashara za Tanzania Bara kuwekeza Zanzibar, ikiwemo Benki ya Stanbic, ambayo inatarajia kufungua tawi lake la kwanza visiwani humo mwaka huu.
Akizungumza hapo awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango ya Zanzibar, Dkt Juma Malik Akil, alisema kuwa mkopo huo wa pamoja ni sehemu muhimu ya mkakati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kukopa ndani ya nchi ili kukidhi TZS trilioni 1.7 katika bajeti ya maendeleo ya mwaka huu wa fedha.
“Bado tunakabiliwa na pengo kubwa la ufadhili wa miradi ya maendeleo, ambalo linahitaji msaada wa aina hii na ushirikiano wa kimkakati, kama huu wa leo kati ya Benki ya Stanbic na PBZ Bank,” alisema Dkt Akil.
Katika hotuba zao, viongozi wa benki hizo mbili walisema kuwa mkopo huo hautainufaisha tu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), bali pia utachochea kuboresha maisha ya wananchi.
Bw. Manzi Rwegasira, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, alielezea kuwa mkataba huo ni hatua muhimu katika kudhihirisha dhamira thabiti ya benki hiyo ya kuunga mkono ustawi wa Zanzibar na maendeleo ya uchumi wa Tanzania kwa ujumla.
Katika kuthibitisha azma hiyo, Bw. Rwegasira alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita, Stanbic imefanikisha kupatikana kwa zaidi ya dola bilioni 1 za Marekani (sawa na takriban TZS trilioni 2.6) kwa ajili ya kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akisisitiza umuhimu wa ukopeshaji wa pamoja, kiongozi huyo alieleza kuwa mkopo huu utawezesha utekelezaji wa miradi muhimu ya kijamii na kiuchumi, ambayo itakuwa na athari chanya za moja kwa moja kwa maisha ya watu wengi na kuchochea maendeleo endelevu ya Zanzibar.
"Sisi, kama Benki ya Stanbic, tuna dhamira ya dhati ya kuchangia maendeleo ya Tanzania kwa sababu hapa ni nyumbani kwetu. Tunawajibika kuwa sehemu ya ukuaji wa taifa letu kwa kuhakikisha upatikanaji wa ufadhili wa kimkakati kama huu tulioshirikiana na PBZ.”
Bw. Rwegasira alisema kuwa mkopo huu ni zaidi ya mtaji na utazinufaisha sekta kuu kama vile uvuvi, uchukuzi wa baharini, nishati, utalii, na miundombinu, huku uchumi wa buluu ukinufaika kwa njia nyingi na katika namna tofauti.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya PBZ, Bw. Arafat Ally Haji, alieleza kuwa mkopo huu wa maendeleo utasaidia miradi mikubwa ya kimkakati na miundombinu ya serikali, ikiwemo uboreshaji na upanuzi wa bandari ya Zanzibar.
Alisema kuwa mkopo wa pamoja una lengo la kuharakisha mwelekeo wa ukuaji wa Zanzibar na kuimarisha maendeleo yake kwa ujumla kwa kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi.
“Fedha hizi zitawezesha kukamilika kwa miradi ya kijamii na kiuchumi inayoendelea, huku pia zikifadhili mipango mipya inayopangwa na mamlakaili kuhakikisha ustawi wa kudumu kwa wananchi wa Zanzibar,” alisema Bw Haji.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi (wapili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Stanbic Bank Tanzania, Bw. Manzi Rwegasira (wapili kushoto) alipomtembelea Ikulu Zanzibar Jumatano. Manzi ameambatana na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa, Ester Manase (kushoto) na Noella Kimaro (kulia), Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano ya Sekta ya Umma, Stanbic Bank.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Saada Mkuya (katikati) akionyesha mkataba uliosainiwa baina ya Benki ya Stanbic Tanzania (SBT) na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kuiwezesha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupata mikopo ya kibenki, ili kusaidia kufadhili miradi ya maendeleo endelevu visiwani humo. Kupitia makubaliano haya, benki hizi zitatoa Shilingi Bilioni 185 katika awamu ya kwanza ya mkopo huu kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ameambatana na Mtendaji Mkuu wa Stanbic Bank, Manzi Rwegasira (watatu kulia); Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ, Arafat Haji(wapili kushoto); Katibu mkuu wa wizara hiyo, Dr. Akil Juma Malik (watatu kushoto) pamoja na wadau wengine kutoka pande zote. Hafla ya utiaji Saini imefanyika Jumatano Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Stanbic Bank Tanzania, Bw. Manzi Rwegasira alipomtembelea Ikulu Zanzibar Jumatano. Manzi ameambatana na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa, Ester Manase (kulia) na Noella Kimaro, Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano ya Sekta ya Umma, Stanbic Bank.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Saada Mkuya (katikati) akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini baina ya Benki ya Stanbic Tanzania (SBT) na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kuiwezesha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupata mikopo ya kibenki, ili kusaidia kufadhili miradi ya maendeleo endelevu visiwani humo. Kupitia makubaliano haya, benki hizi zitatoa Shilingi Bilioni 185 katika awamu ya kwanza ya mkopo huu kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ameambatana na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa, Ester Manase (kulia); Mtendaji Mkuu wa Stanbic Bank, Manzi Rwegasira (wapili kulia) na Katibu mkuu wa wizara hiyo, Dr. Akil Juma Malik (kushoto) pamoja na wadau wengine kutoka pande zote. Hafla ya utiaji Saini imefanyika Jumatano Zanzibar.
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...