Na. Josephine Majura, WF, Ukerewe, Mwanza
Serikali
imesema inatambua mchango mkubwa wa watoa huduma za kifedha nchini
katika kuwahudumia wananchi ili kuhakikisha wanapata fursa ya kufanya
miamala ya kifedha kwa urahisi, hasa katika maeneo ambayo benki
hazijafika.
Hayo
yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mkoa wa Mwanza, Mhe.
Christopher Ngubiagai, alipokutana na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya
Fedha na Taasisi zake, ambayo ipo mkoani Mwanza kutoa elimu ya fedha
kwa makundi mbalimbali.
Aliongeza
kuwa watoa huduma za fedha wamekua na mchango katika kukuza uchumi wa
wananchi kwa kuwa kupitia watoa huduma hao wananchi wameweza kupata
mikopo, kujiwekea akiba na kufanya malipo kwa njia za kidijitali.
“Serikali
itaendelea kushirikiana na watoa huduma za fedha nchini ili kuhakikisha
kuwa huduma hizi zinaimarishwa na kuwafikia wananchi wengi zaidi,
hususan waliopo vijijini na maeneo ya mbali.” Alisema Mhe. Ngubiagai.
Alifafanua
kuwa pamoja na kazi nzuri inayofanywa na watoa huduma za fedha nchini,
aliwataka kufuata sheria, kanuni na taratibu katika kutekeleza majukumu
yao ili kuhakikisha usalama wa mifumo ya kifedha, ulinzi wa watumiaji wa
huduma za kifedha na kukuza uaminifu katika sekta hiyo.
Kwa
upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ukerewe, Bw. Goodlucky Mtigandi, alisema mafunzo ya elimu ya fedha
yamefika wakati muafaka kipindi ambacho wanashughulikia migogoro
mbalimbali ya mikopo umiza.
“Tuamini
mafunzo haya yatawasaidia wananchi kutambua umuhimu wa matumizi sahihi
ya fedha kwa maisha ya leo na kesho”, alisema Bw. Mtigandi.
Naye
Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara
ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, alizisisitiza Taasisi za Fedha zinazotoa
mikopo kwa wananchi kuhakikisha wanarudisha dhamana kwa wakopaji mara
tu wanapomaliza marejesho ya mikopo.
Akizungumza
baada ya kupatiwa mafunzo ya fedha mmoja wa washiriki, ambaye ni
Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara Wilaya ya Ukerewe, Bw. Baraka Jeremiah,
aliiomba Serikali kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa mkopaji na
mkopeshaji ili pande zote mbili zijue haki, wajibu na sheria
zinazotakiwa kufuatwa.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Ukerewe, Mwanza)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...