NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuongeza wigo wa kuimarisha upatikanaji wa vitabu kwa kushirikisha kampuni za uchapishaji na wadau wa sekta binafsi ili kupunguza gharama za uchapishaji.

Amesema anafahamu kuwa TET imedhamiria kuchapa vitabu kwa wingi ili kufikia uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja, jambo ambalo litaleta manufaa makubwa katika elimu na Taifa kwa ujumla.

Ameyasema hayo leo baada ya kumalizika kwa matembezi ya hisani katika ofisi za TET Jijini Dar es Salaam.

Amesema ushiriki wa wadau katika uchapishaji wa vitabu utasaidia kutatua changamoto ya upungufu wa vitabu shuleni, na kufikia lengo la kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja.

"Vitabu ni chanzo cha maarifa na maendeleo, na ni muhimu katika kuhakikisha elimu bora kwa wanafunzi". Amesema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba amesema maadhimisho ya miaka 50 TET pamoja na kampeni ya kitabu kimoja mwanafunzi mmoja yanatarajiwa kuhitimishwa Juni mwaka huu.

Amesema matembenzi hayo yamejikita katika kukusanya fedha kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwemo serikali, wadau binafsi, mashirika ya dini na watu binafsi, ili kuchangia zaidi ya Sh. Bilioni 297, zitakazotumika kununua vitabu na kompyuta kwaajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

"Katika fedha hizo zitakazokusanjwa Sh. Bilioni sita zitatumika kununua Kompyuta mpakato 15,935 na kupakiwa vitabu laini (soft copy) na maudhui mbalimbali ya kujifunzia kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika mikoa 10 Tanzania Bara na Zanzibar.

"Mikoa hii ya awali itasaidia kujifuna na kuendelea na mikoa mingine iliyobaki, pia vitabu vyote vya masomo ya sayansi vinavyochapwa ni kwa uwiano wa kimoja kwa mwanafunzi mmoja. Kupitia matembezi haya na kampeni inayoendelea kufanyika iliyoanza Februari 25, mwaka huu tumefanikiwa kukusanya fedha hizo zitakazoenda kusaidia mpango wetu kwa hatua za awali," amesema Dkt. Komba






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...