JOPO la majaji waliobobea kwenye tasnia ya habari limeanza rasmi kuchambua kazi za waandishi wa habari wanaowania Tuzo za Uwiano wa Kijinsia kwa mwaka 2025, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usawa wa kijinsia kupitia vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Chama Cha Waandishi wa habari Wanawake TAMWA Zanzibar kimesema Majaji hao pia wameanza ukaguzi wa moja kwa moja katika vyombo vya habari, lengo likiwa ni kutathmini namna vinavyopaza sauti za wanawake na kushughulikia masuala ya kijinsia kwa mtazamo wa kina na jumuishi.
Kwa mwaka huu, jumla ya kazi 120 zimewasilishwa kutoka katika vyombo mbalimbali vikiwemo magazeti, redio, televisheni pamoja na mitandao ya kijamii kutoka Unguja na Pemba ikiwa ni idadi kubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Tofauti na miaka mingine, mwaka huu vyombo vyenyewe vya habari navyo vinashiriki moja kwa moja kwenye mchakato wa tuzo hizo, hatua inayolenga kutambua juhudi za ndani za vyombo hivyo katika kukuza usawa wa kijinsia.
Vigezo vya tathmini kwa waandishi wa habari ni pamoja na ubunifu wa mada, matumizi sahihi ya takwimu, mtazamo wa kijinsia, athari kwa jamii, pamoja na kuzingatia maadili ya kitaaluma na ustadi wa lugha.
Kwa upande wa vyombo vya habari, majaji wanapima uwepo wa sera za jinsia, nafasi za wanawake katika uongozi wa vyombo hivyo, pamoja na ufuatiliaji wa utekelezaji wa masuala ya kijinsia kwa vitendo.
Waandaaji wa tuzo hizi wanatoa wito kwa waandishi na vyombo vya habari kuendelea kutumia kalamu zao kuleta mabadiliko chanya, kwa kuwa ni kupitia habari zenye ushahidi na mtazamo wa kijinsia ndipo jamii inaweza kufikia usawa wa kweli katika uongozi.
Mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya kuwawezesha wanawake katika uongozi na Demokrasia maarufu kama SWIL kwa ushirikiano wa mashirika ya TAMWA ZNZ, ZAFELA, PEGAO na JUWAUZA, kwa msaada kutoka Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...