Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete akipata maelezo ya matumizi ya gesi asilia kwenye magari kutoka kwa Mhandisi Nachael Mwanga pindi alipotembelea banda la GASCO.

Katika kuadhimisha Wiki ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi kitaifa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete ametembelea banda la Kampuni ya GASCO lililopo katika viwanja vya maonyesho mkoani Singida.

Waziri Ridhiwani alipata maelezo ya kina kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na GASCO kuhakikisha usalama wa wafanyakazi na mazingira katika shughuli za uzalishaji na uendelezaji wa gesi asilia nchini. Maelezo hayo yalijumuisha mifumo ya usimamizi wa afya na usalama kazini, matumizi ya vifaa vya kisasa vya kujikinga, na hatua za dharura wanazozifuata endapo hali ya hatari itajitokeza.

Katika mazungumzo yake na maafisa wa GASCO, Mhe. Ridhiwani alipongeza juhudi za kampuni hiyo katika kuweka usalama wa wafanyakazi kuwa kipaumbele cha juu. Alisisitiza kuwa maendeleo ya sekta ya gesi asilia yanahitaji kuambatana na viwango bora vya usalama na mazingira ili kulinda rasilimali watu na mazingira ya nchi kwa ujumla.

‘‘Nafurahishwa kuona GASCO wakizingatia viwango vya kimataifa katika shughuli zao," alisema Waziri Ridhiwani.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete akifurahi pamoja na watumishi wa GASCO katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi.

Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi huadhimishwa kila mwaka kama sehemu ya jitihada za serikali na wadau mbalimbali katika kuhamasisha umuhimu wa kuhakikisha kwamba maeneo ya kazi yanakuwa salama, yenye mazingira bora ya afya, na rafiki kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.


Kwa upande wao, maafisa wa GASCO walielezea dhamira ya kampuni hiyo ya kuendelea kuboresha mifumo ya usalama ili kuchangia maendeleo endelevu ya sekta ya nishati nchini Tanzania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...