Na Diana Byera – Ngara

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Bi. Fatma Mwassa, ametangaza ujio wa kambi maalum ya madaktari bingwa waliotumwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa wananchi wa mkoa wa Kagera kuanzia tarehe 5 hadi 9 Mei, 2025.

Akizungumza na vyombo vya habari katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Bi. Mwassa alisema kuwa timu hiyo kubwa ya madaktari bingwa itatoa huduma mbalimbali za matibabu kwa kutumia vifaa vya kisasa na vipimo vilivyokamilika.

Lengo kuu la kambi hiyo ni kuwapunguzia wananchi gharama za kusafiri kufuata matibabu kwenye hospitali kubwa zilizopo Dar es Salaam, Mwanza na Arusha.

“Rais wetu ametambua changamoto za wananchi, hasa wale wasio na uwezo wa kusafiri kutafuta matibabu. Hii ni fursa ya kipekee. Ikiwa unaumwa au una mtoto anayehitaji matibabu, njoo upate huduma bora karibu na nyumbani,” alisema Bi. Mwassa.

Huduma za kibingwa zitakazotolewa ni pamoja na matibabu ya magonjwa ya upasuaji, magonjwa ya wanawake, magonjwa ya akili, magonjwa ya ndani, ini, figo, pua, koo, mfumo wa fahamu, mfumo wa mkojo, pamoja na huduma za mazoezi ya viungo na utengamano. Madaktari waliobobea katika kila eneo watakuwepo kutoa huduma hizo kwa ufanisi.

Huduma hizo zitapatikana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera – Bukoba, na zitakuwa wazi kwa wananchi kutoka wilaya zote za Kagera, mikoa jirani kama Kigoma na Geita, pamoja na nchi jirani zinazopakana na mkoa huo.

Bi. Mwassa alibainisha kuwa wagonjwa wenye bima ya afya watatumia bima zao kupata huduma, huku wale wasio na bima wakichangia gharama nafuu ukilinganisha na zile zinazohitajika kwa safari na matibabu katika hospitali za kitaifa.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Dkt. Mseleta Nyakiroto, alisema kuwa maandalizi yote kwa ajili ya kupokea madaktari hao yamekamilika, na tayari wananchi 900 wamekwishaandikishwa kupokea huduma hizo tangu Aprili 28 hadi 30.

“Tunakusudia kuhudumia zaidi ya wananchi 1,500 kutoka mkoa wa Kagera na maeneo ya jirani. Madaktari bingwa na mabobezi 41 kutoka timu ya Rais Samia wataungana na madaktari wetu wa ndani kutoa huduma bora,” alisema Dkt. Nyakiroto.

Aliongeza kuwa kambi hiyo pia ni fursa kwa madaktari wa ndani kujifunza na kuongeza weledi wao katika utoaji wa huduma za kibingwa, jambo linalochangia kuboresha huduma za afya kwa muda mrefu.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...