Na Diana Byera, Bukoba.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, amewasilisha mpango maalumu wa kuhakikisha vijana na wanawake mkoani Kagera wanashiriki kikamilifu kilimo cha zao la kahawa ili kuongeza uzalishaji kutoka tani 60,000 zinazozalishwa kwa sasa hadi kufikia tani 200,000 ifikapo mwaka 2030.

Aliwasilisha taarifa hizo katika kikao cha wadau wa kahawa mkoani Kagera, ambapo wadau walijadili na kutambua fursa, changamoto zinazolikabili zao la kahawa, na jinsi ya kuongeza mavuno. Amepongeza msimu wa mwaka 2024/2025 kwa kuingiza zaidi ya shilingi bilioni 250 kupitia zao la kahawa, huku halmashauri za mkoa wa Kagera zikinufaika na shilingi bilioni 7 kama mapato ya ndani.

Alisema kuwa ili kuongeza uzalishaji, mkoa wa Kagera umetenga eneo la hekta 10,000 kwa ajili ya vijana na wanawake. Kwa kuanzia Wilaya ya Karagwe itapata hekta 2,000 na Wilaya ya Muleba hekta 2,000, huku wilaya nyingine zikifuata baadaye kwa ajili ya kusaidia vijana kupata maeneo mapya ya kilimo.

Aidha, alisema kuwa mpaka sasa mkoa wa Kagera tayari umeanzisha shamba la mfano katika Kijiji cha Makongora, Wilaya ya Muleba, ambapo vijana na wanawake 300 kila mmoja amepata ekari moja iliyowekewa miundombinu yote kwa ajili ya kuitunza na kuisimamia ili baada ya muda mfupi waweze kuvuna kahawa na kuongeza kipato.

“Serikali imeongeza bei ya kahawa kutoka shilingi 1,200 hadi 5,000 – hii haijawahi kutokea. Tayari serikali imetoa trekta tano za kilimo ambazo zinasaidia kuandaa miundombinu na mashamba darasa ya vijana ambao baadaye wataongeza tija katika uzalishaji. Kwa sasa pesa ya kilimo cha kahawa iko nje nje, tujikite katika kilimo,” alisema Mwassa.

Kupitia kikao hicho, aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote na wakuu wa wilaya kuhakikisha wanasimamia asilimia 20 ya mapato yanayotokana na kahawa ili yarudi kusaidia kilimo cha kahawa na kuzalisha miche yenye ubora. Aidha, alipiga marufuku uvunaji wa kahawa mbichi unaoharibu ubora wa zao hilo sokoni.

Meneja wa Bodi ya Kahawa mkoani Kagera, Edmond Zani, alisema kuwa uhitaji wa kahawa aina ya Robusta katika masoko ya nje ni mkubwa sana. Hivyo jitihada za wananchi na wadau wote kuhamasisha kilimo cha kahawa zinahitajika. Aliwahakikishia wadau kuwa kutokana na mipango iliyowekwa katika mkutano wa nchi 25 zinazolima kahawa barani Afrika, bado bei ya kahawa itaendelea kuimarika katika masoko ya dunia.

Alisema kuwa kwa mwaka 2024/2025, malengo yalikuwa kukusanya tani 74.8 za kahawa kutoka kwa wakulima wa Mkoa wa Kagera, lakini tani zilizokusanywa ni 54.2 sawa na asilimia 72.4, akieleza kuwa jitihada zaidi za uzalishaji bado zinahitajika ili kuongeza pato la mkoa na uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.

Bodi ya kahawa inatarajia kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Zao la Kahawa (TACRI) kugawa miche bure kwa wakulima wa kahawa 17,164,000 ili kuongeza uzalishaji. Aidha, alisema kuwa tayari bodi ya kahawa nchini imetangaza kufungua msimu wa ununuzi wa kahawa kwa bei ya shilingi 5,000 kwa kahawa ya maganda.

Changamoto zilizojitokeza katika msimu uliopita wa kahawa ni pamoja na vyama vya msingi kuwasilisha kahawa hewa katika mnada, ambapo wanunuzi walipofika katika vyama hivyo walikuta maghala yakiwa tupu. Changamoto nyingine ni utoroshaji wa kahawa inayovunwa mapema kabla ya mnada kufunguliwa, uvunaji wa kahawa mbichi inayopoteza ubora, pamoja na matumizi madogo ya kahawa katika soko la ndani.

Alberth Katagira, mmoja wa wazalishaji wa miche ya kahawa, ameiomba serikali na bodi ya kahawa kufanya utafiti kwa wakulima wanaopewa miche ya kahawa kama kweli wanaisimamia, inastawi au inakabiliwa na changamoto nyingine, kuliko kuongeza miche mipya kila msimu bila kubaini changamoto za awali.

Aidha, aliomba serikali kutoa elimu kubwa kwa wakulima wa Mkoa wa Kagera kuhusu matumizi ya mbolea, kwani baadhi yao wana mawazo tofauti kuhusu matumizi ya mbolea inayotolewa kwa ruzuku na serikali kwa kuhofia kuwa itaharibu mashamba yao ya migomba.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...