Na Albano Midelo

Mji wa Songea mkoani Ruvuma umeanza kuandika historia mpya ya elimu ya juu baada ya miongo ya kusubiri Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ameshuhudia makabidhiano ya mradi mkubwa wa ujenzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha, kampasi ya Songea, mradi utakaogharimu shilingi bilioni 18 na kuibua matumaini mapya kwa maelfu ya vijana wa Kusini mwa Tanzania. Hafla hiyo muhimu imefanyika katika kata ya Tanga, mtaa wa Pambazuko – eneo rasmi litakalojengwa chuo hicho. 

Kanali Ahmed amesema ujenzi huo ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ya kuleta mageuzi ya kielimu na kiuchumi katika maeneo ya pembezoni. 

“Ujenzi wa chuo hiki siyo tu kwamba unawapa vijana wetu fursa ya elimu ya juu karibu na nyumbani, bali pia unaleta neema ya ajira, unachochea biashara na kuinua pato la mji wa Songea,” amesema Kanali Ahmed kwa msisitizo, huku akihamasisha ushirikiano kutoka kwa wananchi kuhakikisha mradi unakamilika kwa mafanikio.

 Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Prof. Eliamani Sedoyeka, amesema kati ya shilingi bilioni 45 zilizotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya chuo hicho, bilioni 18 zimetengwa kwa ajili ya kampasi ya Songea – chuo ambacho kitaweza kuhudumia wanafunzi zaidi ya 10,000 pindi kitakapokamilika.

 “Ni mradi mkubwa usio na mfano katika mkoa wa Ruvuma, hivyo tunalo jukumu la kuhakikisha fedha hizi zinasimamiwa kwa uwazi na ufanisi,” amesema Prof. Sedoyeka akitoa wito kwa wasimamizi na wadau wote wa maendeleo. 

Katibu Tawala wa Mkoa, Bi. Mary Makondo, ameahidi ushirikiano wa karibu kwa taasisi zote husika, akisisitiza kuwa ujenzi huo ni chachu ya maendeleo si tu kwa Songea bali kwa mkoa mzima wa Ruvuma.

 Nao wananchi wa Songea waliofurika kushuhudia tukio hilo, wakielezea furaha yao huku wakitaja ujio wa chuo hicho kuwa ni “mwanga wa matumaini mapya” kwa kizazi cha sasa na kijacho. Naye , Mbunge wa Songea Mjini ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, amesema:

 “Hii ni ndoto ya muda mrefu ya wananchi wa Songea ambayo sasa tunashuhudia ikitimia. Ni mwanzo wa enzi mpya ya kielimu na kiuchumi.” Mradi huu mkubwa si tu unaweka alama ya maendeleo ya mkoa wa Ruvuma, bali pia unaandika ukurasa mpya katika historia ya elimu ya juu nchini Tanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed akizungumza kwenye hafla ya Makabidhiano eneo la ujenzi wa chuo cha Uhasibu Kampasi ya Songea. 
Picha ya Makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha kampasi ya Songea 
Muonekano wa baadhi ya majengo ya Chuo cha Uhasibu Kampasi ya Songea kitakapokamilika kwa asilimia 100

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...