NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limechukua hatua ya kuandaa viwango vya ubora kwa bidhaa za nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha usalama wa afya ya wananchi na kuhifadhi mazingira.

Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa bidhaa hizo (nishati na teknolojia) zinazotumika nchini zinazingatia ubora na usalama wa watumiaji, pamoja na kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo yamekuwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira na matatizo ya kiafya kwa watanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 13, 2025 Jijini Dar es Salaam, Afisa Viwango TBS, Mhandisi Spiradson Kagaba amesema kuwa matumizi ya bidhaa zisizo na viwango huweza kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo ajali za moto, uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba, na madhara ya kiafya.

"Ni muhimu kuelewa kuwa si kila bidhaa za nishati ya kupikia, ikiwa ni pamoja na majiko na nishati yenyewe,  zinazodaiwa  kuwa safi zina ubora unaohitajika. Majiko yanayothibitishwa na TBS hupitia hatua za kina za ukaguzi na majaribio ya kitaalamu ili kuhakikisha kuwa yanatumia nishati kwa ufanisi, hayatoi vumbi chembe na monoksidi ya kaboni inayodhuru afya, yanadumu na ni salama kwa matumizi ya nyumbani," Amesema Mhandisi Kagaba.

Amesema kuwa kwa majiko ya nishati safi ya kupikia ambayo yanatoka nje ya nchi, mpaka yanamfikia mtumiaji, tayari wameshajiridhisha na kuthibitisha ubora kwa kutoa alama ya ubora ambayo ni muhimu kwa mtumiaji anaponunua jiko hilo kujiridhisha kama limethibitishwa.

"Mpaka unaenda sokoni unakuta kuna jiko la umeme la kupikia, unakuta kuna mkaa mbadala, TBS kashahakikisha kwamba yako salama". Amesema 

Amesema matumizi ya majiko ya nishati safi ya kupikia yanaweza kusababisha mlipuko wa moto, kupigwa shoti ya umeme kwa wale wanaotumia majiko ya umeme, hivyo basi kuna umuhimu wa TBS kuandaa viwango ili kuhakikisha mtumiaji anakuwa salama.

Kwa upande wake Afisa Viwango, Mhandisi Mohamed Kaila amesema jukumu lao ni kuhakikisha nishati safi ya kupikia inakuwa ni salama kwa watumiaji bila kumletea madhara yoyote ya kiafya.

"Nishati inaweza kuendelea kuwa safi kama mtumiaji atakuwa salama pindi atakapokuwa na matumizi ya majiko haya ya nishati safi ya kupikia, hivyo basi ni muhimi sisi kama TBS kuhakikisha usalama kwa mtumiaji wa bidhaa hii". Amesema

Hatua hii ya TBS inakwenda sambamba na malengo ya Mpango wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, ambao unalenga kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi kufikia mwaka 2034.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...