
Na: Nihifadhi Abdulla.
ZANZIBAR ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda inayolinda haki ya uhuru wa habari. Hata hivyo, hali halisi inaonesha kuwa utekelezaji wa mikataba hiyo uko mbali na matarajio.
Vikwazo vya kisheria, ukosefu wa dhamira ya kisiasa, na mazingira ya hofu vinazidi kuifanya tasnia ya habari kuwa ya kuhatarisha kwa waandishi na vyombo vyao.
Miongoni mwa mikataba muhimu iliyoridhiwa ni Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu (UDHR) ambalo katika Kifungu cha 19 linaeleza kuwa kila mtu ana haki ya kutoa maoni na kupata taarifa bila kuingiliwa. Pia kuna Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (ACHPR), ambao katika Kifungu cha 9 unasema wazi kuwa kila mtu ana haki ya kupokea taarifa na kutoa maoni yake.
Aidha, Azimio la CEDAW, pamoja na kutetea haki za wanawake, linatambua kwamba haki ya kupata taarifa ni msingi wa usawa na ushiriki wa wanawake katika maendeleo. Zanzibar kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano, imeridhia yote haya lakini, vipi utekelezaji wake?
Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu, unaoeleza kwenye Kifungu cha 9, unalinda haki ya kutoa maoni na kupata taarifa, lakini katika hali halisi ya Zanzibar, haki hizi zimebanwa kwa kiasi kikubwa kupitia sheria kandamizi za habari.
Kwa mujibu wa Zaina Abdalla, Afisa Program wa Boresha Habari Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA-Zanzibar, anasema hali bado ni tete. “Zanzibar inaonekana kuridhia kwa jina tu haki ya kupata habari, bado ni changamoto kubwa, Tunakosa taarifa muhimu kuhusu huduma za afya, ustawi wa jamii, na hata fursa za kiuchumi kwa sababu mazingira ya habari ni ya hofu.”
Zaina anaeleza kwamba kwa miaka mingi TAMWA imekuwa mstari wa mbele katika kutetea mazingira huru ya upatikanaji wa habari. “Tumeendesha warsha nyingi za kuwajengea uwezo waandishi wa habari wanawake, tumefanya tafiti kuhusu hali ya uhuru wa habari, na pia tumekuwa tukishirikiana na vyombo vya Serikali kushinikiza mabadiliko ya sera.”
Anasisitiza kuwa bila uhuru ya habari, hakuna uwajibikaji wa viongozi wala maendeleo ya kweli. “Tunaamini kuwa mwananchi mwenye taarifa sahihi ana nguvu ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa, ndio maana tunasisitiza utekelezaji wa mikataba hii.”
Mwandishi wa habari mwandamizi na mwanaharakati wa haki za vyombo vya habari, Salim Said Salim, anakiri katika miaka yake ya taaluma ya habari imemfunza kuwa uhuru wa vyombo vya habari Zanzibar ni wa msimu. “ kila kada au tasnia inajisimamia wenyewe lakini sio kwa tasnia ya uwandishi kumejaa mazonge kuna ya ahadi za kila siku kesho kuhusu marekebisho ya sheria maajabu ”
Anataja kwamba changamoto kubwa ni kuwapo kwa sheria kandamizi ikiwemo Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho sheria namba 8 ya mwaka1997 na Sheria ya Tume ya Utangazaji namba 7 ya mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebisho na Sheria namba 1 ya 2010 za Habari ya mwaka 2016 “Hizi sheria zimekuwa zikilenga kudhibiti badala ya kuendeleza uhuru wa habari. Zimekuwa zikitumika kama fimbo ya kisiasa,” anasema Salim kwa masikitiko.
Salma Said, mwandishi wa habari za Maendeleo WAHAMAZA anasema kuwa mazingira ya Zanzibar si rafiki kwa uandishi wa habari huru. “Mara kadhaa nimeshuhudia waandishi wakiitwa polisi, kutishwa, au hata kufungiwa kwa vyombo vyao kwa kuandika habari zinazowakosoa viongozi,” anasema.
Salma anaeleza kuwa waandishi wa habari wanakumbana na changamoto nyingi zinazokwamisha uhodari wa kujituma na hivyo kuwa waandishi wa kumsemea mtu badala ya kuisemea jamii “Hii inakujakutokanana kukithiri vitisho na hakuna sheria inayomtetea mwandishi licha ya kuwepo mikataba na matamko dhidi yao.
Mwanaharakati wa Demokrasia Almas Mohamed anasema kuwa uhuru wa habari ni kigezo muhimu cha kuwepo kwa utawala bora. “Huwezi kusema una demokrasia kama wananchi hawana uhuru wa kuhoji, kukosoa, na kuelewa kinachoendelea Serikalini, vyombo vya habari vinapobanwa, basi hata wananchi wanabanwa,” anasema kwa msisitizo.
Almas anaongeza kuwa mikataba kama UDHR na ACHPR haipaswi kuwa ya kusaini tu, bali ya kutekeleza. “Nini faida ya kuwa na mikataba yote hii kama wananchi hawawezi kusoma ripoti ya uchunguzi, kusikiliza hoja mbadala, au hata kupost maoni yao bila hofu ya kutiwa mbaroni? hili ni suala la haki za binadamu na sio siasa,” anasema
Zanzibar Press Club (ZPC) kupitia mwakilishi wake Abdalla Mfaume pia inataka mabadiliko ya dhati. “Vyombo vya habari vinafanya kazi katika mazingira ya mashaka. hii si hali nzuri kwa maendeleo ya Taifa letu,” anasema Abdalla.
Wanaharakati, waandishi wa habari, na taasisi za kiraia wanasisitiza kuwekwa mazingira bora, huru na salama ya kufanyia kazi huku wakishinikiza utekelezaji wa mikataba iliyosainiwa, siyo ya kuiacha kuwa maandishi tu kwenye karatasi kufanya hivyo uhuru wa habari utabaki kuwa ndoto ya mbali visiwani humu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...